Mwaka mmoja tangu kifo cha Maalim Seif: Ipi hali ya Zanzibar na upinzani?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi Tanzania
- Muda wa kusoma: Dakika 4
"Ndugu wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla, kwa masikitiko makubwa nakujulisheni leo tarehe 17 Februari, 2021, majira ya saa tano asubuhi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amefariki dunia."
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akitangaza kifo cha Maali Seif, kilichotokea mwaka mmoja uliopita katika hospitali ya taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Aliondoka duniani akiwa ameziacha harakati zake za upinzani zikizidi kumea kwa kasi. Kwa hakika mjadala ungekuwa tofauti kama angefariki wakati ule chama chake cha zamani cha wananchi (CUF) kikiwa katikati ya mgogoro.
Pengine hati kubwa katika magazeti zingesomeka, 'Maalim Seif afariki, aacha mfarakano ndani ya chama.' Leo hii baada ya mwaka kukatika mjadala sio kuhusu mgororo wa kisiasa, bali waliomrithi wana-zisukumaje mbele harakati alizowachia.
Mpigania mageuzi ya kidemokrasia, aliyekuwa muhimili muhimu kwa siasa za upinzani. Fauka ya hayo, huwezi kuzungumza siasa za Zanzibar baada ya kurudi kwa mfumo wa vyama vingi 1992, bila ya kutaja jina la Maalim Seif.
Nguvu zake za kisiasa zilikuwa kubwa. Hata washindani wake ndani ya Zanzibar walielewa hilo. Nyakati za taharuki za kisiasa kuwa kubwa, hawakuacha kukaa nae mezani kutafuta miafaka ili mambo yasizidi kwenda mrama.
Kaacha upinzani dhaifu au imara?
Baada ya siku saba za maombolezo ya kifo chake na bendera kupepea nusu mlingoti. Shughuli za kisiasa na kitawala zilibidi zirudi kama kawaida. Kazi kubwa ilikuwa ni kumpata mrithi wake kuziba nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Kumpata mrithi wa Maalim Seif ulikuwa mtihani wa kwanza kwa upinzani Zanzibar tangu kifo chake. Kuna mifano mingi inayoonesha mifarakano ya kisiasa huanzia katika ngazi ya juu, pale kila mmoja anapozongwa na uchu wa kutaka kuwa kiongozi.
Othman Masoud, Makamu wa kwanza wa Rais wa sasa, hakuwa na mizizi katika siasa za upinzani na katika ACT Wazalendo kwa ujumla; ila jina lake ndilo lililopitishwa na kuridhiwa na wanachama wenzake bila ya kutokea mivutano ya waziwazi.
Upinzani aliouacha mwendazake ulipasi vyema mtihani huu. Chama chake cha ACT Wazalendo kilithibitisha kwamba kimeachiwa misingi madhubutu yatakayo kipeleka mbele wakati Maalim Seif hayupo tena duniani
Januari 30, 2022 katika Mkutano Mkuu wa ACT Wazalendo, ulifanyika uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti na Makamu mwenyekiti wa chama, ulikuwa ni mtihani wa pili katika ngazi ya kiutawala. Uchaguzi huo umeleta mawimbi ndani ya ACT Wazalendo.
Katika mkutano na waandishi wa habari kisiwani Zanzibar, siku chache tangu kupitishwa jina la Juma Duni Haji kuwa Mwenyekiti, ndugu Hamad Masoud aliyekuwa akichuana na Mwenyekiti huyo, alieleza:
"Kuanzia leo mimi sio mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo wala sio mwanachama tena wa ACT. Kama wanasema Hamad wa nini, wengine wanasema tutampata lini. Wacha nitulie nitafakari."
Kuondoka kwa Hamad na baadhi ya wafuasi wachache hakuja onesha kukigawa chama hicho kwa kiwango cha kuita 'mgogoro wa ACT Wazalendo'. Mapokezi makubwa ya Juma Duni Haji na Othman Masoud, Zanzibar, hasa kule kisiwani Pemba; yaliashiria kwamba mawimbi ya kujiondoa kwao hayakuyumbisha safari ya chama.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter mwanasiasa mkongwe wa upinzani Zanzibar, Ismail Jussa aliandika Februari 11, 2022, "tulijifunza masomo ya siasa na uongozi kutoka kwa aliye bora (Maalim Seif). Hatukumwendea kinyume akiwa hai, hatukumwendea kinyume baada ya kuondoka kwake duniani."
Msururu wa mapito haya ya kisiasa ndani ya mwaka mmoja tangu kuondoka kwake, yanatoa matumaini juu ya uimara aliouacha katika siasa za upinzani visiwani Zanzibar. Swali la kulitafakari ni hili; nguvu hizo zitaendelea kudumu hadi 2025!
Kubwa zaidi ya yote, uimara unao-onekana sasa sio kipimo panapohusika siasa za ushindani dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kabla ya kupambana na CCM katika uwanja wa kisiasa, kwanza ni kupambania mageuzi katika taasisi zinazosimamia hayo mapambano.
Mwaka mmoja Zanzibar bila Maalim
Upinzani chini ya ACT Wazalendo ulipoamua kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kulikuwa na wakosoaji wa hatua hiyo. Na bado wapo wanaoendelea kukosoa. Hoja kubwa ya wakosoaji; kwanini upinzani ukukubali kuingia katika serikali na adui wao kisiasa!

Chanzo cha picha, IKulu ya Rais Tanzania
Hasa kwa kuzingatia uvunjifu mkubwa wa haki za binaadamu uliotokea, kama ulivyoelezwa katika ripoti ya Human Rights Watch. Pia, uchaguzi huo ulikuja na matokeo ya ajabu ambayo hayakuwahi kutokea tangu chaguzi za vyama vingi kuanza.
Uamuzi wa Maalim Seif kujiunga na SUK una pande mbili. Mosi, ni takwa la kikatiba. Julai 2010 Wazanzibari walipiga kura ya maoni kutaka mabadiliko ya kuitawala. Asilimia 66.4 waliunga mkono kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Pili, ulikuwa ni uamuzi wa kisiasa kwa manufaa ya Wazanzibari. Upinzani ulikuwa na uwezo wa kukataa kujiunga. Ila kujiunga kwao kumeleta utulivu mkubwa katika visiwa hivyo vya bahari ya Hindi.
Bila shaka upinzani ungekuwa nje ya serikali, hata baada ya kifo cha Maalim, mjadala mkubwa ungekuwa kama ule wa mwaka 2015 hadi 2020: 'Zanzibar inaondoka vipi katika mkwamo wa kisiasa.'
Maamuzi ya Wazanzibari kutaka serikali ya umoja wa kitafa, hayawezi kuitwa ya ajabu. Na uamuzi wa Maalim kukubali kuingia katika serikali hiyo, manufaa yake yanaonekana sasa. Kaiacha Zanzibar ikijitutumua kwa pamoja kukuza uchumi na sio kujitutumua katika mivutano ya kisiasa.












