Mzozo wa Ukraine: Nato ni nini na kwa nini Urusi ina wasiwasi kuhusu muungano huo wa kijeshi?

Nato soldiers in Serbia, 2021

Chanzo cha picha, Getty Images

Wanachama wa Nato wanatathmini ni kwa kiwango gani wanastahili kusaidia Ukraine inayokabiliwa na tishio la kuvamiwa na Urusi.

Muungano huo - ambao unajumuisha Marekani , Uingereza, Ufaransa na Ujerumani - unajiandaa kijeshi kusaidia Ukraine.

Nato ni nini?

Nato - Shirika la Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini - ni muungano wa kijeshi ulioundwa mwaka 1949 na nchi 12, ikiwemo Marekani, Canada, Uingereza na Ufaransa.

Wanachama walikubali kusaidiana iwapo kutatokea shambulio la silaha dhidi ya nchi yoyote mwanachama.

Lengo lake awali lilikuwa kukabiliana na tishio la upanuzi wa Urusi baada ya vita barani Ulaya.

Mnamo 1955 Urusi ya Soviet ilijibu NATO kwa kuunda muungano wake wa kijeshi wa nchi za Kikomunisti za Ulaya Mashariki, uliofahamika kama Mkataba wa Warsaw.

Kufuatia kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti mwaka wa 1991, nchi kadhaa za zamani za Mkataba wa Warsaw zikawa wanachama wa Nato. Muungano huo sasa una wanachama 30.

Je sula la sasa la Urusi dhidi ya Nato na Ukraine ni lipi?

Ukraine ni jamhuri ya zamani ya Soviet inayopakana na Urusi na EU.

Sio mwanachama wa Nato, lakini ni "nchi mshirika" - hii inamaanisha kuna maelewano kwamba inaweza kuruhusiwa kujiunga na muungano huo wakati fulani siku zijazo.

Urusi inataka hakikisho kutoka kwa madola ya Magharibi kwamba hili halitatokea kamwe - jambo ambalo nchi za Magharibi haziko tayari kukubali.

Ukraine ina idadi kubwa ya Warusi na uhusiano wa karibu wa kijamii na kitamaduni na Urusi. Kimkakati, Kremlin inaiona kama sehemu ya nyuma ya ua ya Urusi.

Ni nini kingine ambacho Urusi inajali?

Rais Putin anadai mataifa ya Magharibi yanatumia muungano huo kuizingira Urusi, na anataka Nato kusitisha shughuli zake za kijeshi mashariki mwa Ulaya.

Kwa muda mrefu amekuwa akisema Marekani ilivunja hakikisho ililoweka mwaka 1990 kwamba Nato haitapanua shughuli zake upande wa mashariki.

Nato inapinga madai ya Urusi na kusema ni idadi ndogo tu ya nchi wanachama wake zinazopakana na Urusi, na kwamba ni muungano wa kujihami.

Wengi wanaamini kwamba kukusanyika kwa sasa kwa wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka wa Ukraine kunaweza kuwa jaribio la kuzilazimisha nchi za Magharibi kuchukulia matakwa ya usalama ya Urusi kwa uzito.

Nato imefanya nini siku za nyuma kuhusu Urusi na Ukraine?

Waukraine walipomuondoa madarakani rais wao anayeiunga mkono Urusi mapema mwaka wa 2014, Urusi iliteka rasi ya Crimea ya kusini mwa Ukraine. Pia iliunga mkono wafuasi wanaotaka kujitena wanaounga mkono Urusi ambao waliteka maeneo makubwa ya mashariki mwa Ukraine.

Nato haikuingilia kati, lakini ilijibu kwa kuweka wanajeshi katika nchi kadhaa za mashariki mwa Ulaya kwa mara ya kwanza.

Tangu Urusi ichukue eneo la Crimea, Nato imeweka vikundi vya vita mashariki mwa Ulaya

Chanzo cha picha, Getty Imges

Maelezo ya picha, Tangu Urusi ichukue eneo la Crimea, Nato imekuwa ikipeleka vikosi mashariki mwa Ulaya

Ina makundi manne ya vita yenye ukubwa wa vita vya kimataifa huko Estonia, Latvia, Lithuania na Poland, na brigedi ya kimataifa huko Rumania.

Pia imepanua ulinzi wake wa anga katika mataifa ya Baltic na Ulaya mashariki ili kuzuia ndege yoyote ya Urusi ambayo inakiuka mipaka ya nchi wanachama.

Urusi imesema inataka vikosi hivi viondolewe.

Ni ahadi gani ina NATO kupewa Ukraine?

Rais wa Marekani Joe Biden amesema Urusi italipa "gharama kubwa" kwa uvamizi.

Marekani imeweka askari 8,500 walio tayari kupambana katika hali ya tahadhari, lakini Pentagon inasema watatumwa tu ikiwa Nato itaamua kuamsha kikosi cha kukabiliana na haraka.

Imeongeza kuwa hakuna mipango ya kupeleka wanajeshi katika Ukraine yenyewe.

Nato imeongeza ulinzi wake wa kijeshi mashariki mwa Ulaya

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty

Maelezo ya picha, Nato imeongeza ulinzi wake wa kijeshi mashariki mwa Ulaya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameonya ongezeko lolote zaidi la kijeshi "itabeba bei ya juu kwa utawala wa Urusi - kiuchumi, kisiasa na kimkakati".

Downing Street ilisema Uingereza inakubali kwamba "washirika lazima watoe majibu ya haraka ya kulipiza kisasi ikiwa ni pamoja na kifurushi cha vikwazo ambacho hakijawahi kutokea".

Je, Nato imeungana juu ya Ukraine?

Rais Biden amesema kuna "umoja kamili" na viongozi wa Ulaya kuhusu Ukraine, lakini kumekuwa na tofauti katika uungwaji mkono ambao nchi mbalimbali zimetoa.

Marekani inasema imetuma tani 90 za "msaada hatari" ikiwa ni pamoja na risasi kwa Ukraine kwa "watetezi wa mstari wa mbele". Uingereza inaipatia Ukraine makombora ya masafa mafupi ya kuzuia vifaru.

Baadhi ya nchi wanachama wa Nato, zikiwemo Denmark, Uhispania, Ufaransa na Uholanzi, wanatuma ndege za kivita na meli za kivita mashariki mwa Ulaya ili kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.

Hata hivyo Ujerumani imekataa ombi la Ukraine la kutaka silaha za kujihami, sambamba na sera yake ya kutopeleka silaha hatari katika maeneo yenye mizozo. Badala yake itatuma msaada wa matibabu.

Rais Macron wa Ufaransa wakati huo huo amekuwa akitoa wito wa kufanyika mazungumzo na Urusi ili kupunguza hali hiyo.