Mzozo wa Ukraine: Silaha ya Uturuki inayoipa Urusi tumbo joto Ukraine

Mzozo kati ya Ukraine na Urusi umesababisha kuongeza kwa hali ya wasi wasi katika eneo la mashariki mwa Ukraine ambapo wapiganaji wanaotaka kujitenga katika eneo la Donbas wamekuwa wakipambana na wanajeshi wa serikali.
Wapiganaji hao wanategemea msaada wa Urusi ambayo imekuwa pia na wanajeshi wake katika mpaka wake na Ukraine tangu ilipochukua kwa lazima eneo la Crimea .
Hata hivyo Ukraine imepata nguvu ya kuweza kukabiliana na ubabe wa Urusi kwa kufanya ushirikiano na Uturuki ambayo imeonekana kuipa upinzani Urusi katika ulingo wa kimataifa huku viongozi wa mataifa hayo Vladmir Putin na Recep Tayyip Erdogan wakipigania kuongeza ushawishi wao ulimwenguni na kushiriki vita vya chini kwa chini dhidi ya mwingine .
Droni ya Bayraktar TB2
Kinachoipa nguvu Ukraine, ni silaha ambayo Uturuki sasa imejikita kama ngome ya utengezaji wa silaha hiyo kote duniani na ufanisi wake vitani unaipa matumaini Ukraine kwamba silaha hiyo inaweza kuipunguza kasi Urusi katika mpango wake kuwa na usemi katika eneo zima la Baltic kupitia kuwaunga mkono viongozi wanaotii na kushirikiana na Moscow .
Silaha yenyewe ni droni ama ndege zisizo na marubani ambazo zimejihami kwa silaha kali kali na kutumika vitani.Droni ya Bayraktar TB2 ambayo Uturuki imekuwa ikiitengeza na kuiuza kwa nchi mbali mbali imejitokeza kama silaha tosha ya kuweza kukabiliana na maadui hasa katika vita visivyo vya kawaida ambapo wanajeshi anakutana ana kwa ana uwanjani .
Katika kinachodhihirisha kujitolea kwa Ukraine kuboresha uhusiano wake na Uturuki kwa lengo la kuweza kupata msaada wake endapo itavamiwa na Urusi au wapinagaji wanaoungwa mkono na Moscow, rais wa Ukraine mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili alizuru Uturuki kusherehekea miaka 10 ya ushirikiano wa kimkakati baina ya nchi hizo mbili.
Ziara hiyo ni wazi kwamba haikuwapendeza wengi huko Moscow lakini wadadisi wanafahamu kwanini ilikuwa ni ya umuhimu mkubwa kwa mataifa yote mawili .
Kujihami vya kutosha
Mnamo mwaka wa 2018 Ukraine ilinunua droni sita za Bayraktar TB2 na makombora 200 yenye uwezo mkubwa sana wa kulenga . Ununuzi huo wa dola milioni 69 ulikuwa sehemu ya mkataba wa ulinzi kati ya nchi hizo mbili .

Wataalam wa jeshi la Ukraine walichunguza kwa karibu matumizi ya droni hizo huko Nagorno-Karabakh. Wanasema kufanana kati ya mapigano ya
Azabaijani dhidi ya Armenia katika mzozo huo, na mapambano ya Ukraine ya kuchukua udhibiti wa mkoa wake uliojitenga kwa kusaidiwa na vikosi vya Urusi vinaonyesha Kyv ipo katika uwezo mkubwa wa kufaulu vitani kutumia droni hizo za Uturuki .
Baada ya kupambana na waasi hao kwa miaka saba ,wengi huko Kyiv wanangoja sana kwa hamu kuijaribu teknlojia hiyo ya Uturuki vitani ili kuona Iwapo itawasaidia kujishindia baadhi ya maeneo iliyopoteza kwa wapiganaji wanaoungwa mkono na Moscow.
Russia inasema Ukraine inajaribu kuchochea mgogoro ilhali Kyiv Inawashtumu wapiganaji mashariki mwa nchi hiyo kwa kuzidisha mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa serikali . Urusi pia imekuwa ikiwapeleka wanajeshi wake wengi mipkana .
Rais Erdogan ametoa himizo la kuwepo utulivu mashariki mwa Ukraine lakini amesema nchi yake iko tayari kuisaidia Kyiv .
Iwapo mapigano kati ya nchi hizo yatazuka Ankara huenda ikapata fursa ya kuifedhehesha Moscow kama ilivyofanyiwa na Urusi nchini Syria.Droni za Uturuki zilizopelekwa mashariki mwa Ukraine zinaipa Ankara nafasi ya kuthibitisha uwezo wake wa kijeshi katika vita vinavyoendelea katika mpaka wa Urusi.

Chanzo cha picha, EPA
Nafasi ya kuiga mazuri yaliyojitokeza kutumia droni za Uturuki na wataalam wake wa kijeshi katika vita vya Nagorno-Karabakh hakika vinawapa nguvu baadhi ya viongozi wa Kyiv katika mgogoro wao na Urusi .
Teknolojia ya kijeshi
Ankara inaiona Ukraine kama ngao muhimu dhidi ya Urusi na imekuwa mtetezi wake mkubwa ili ikubalike kujiunga na muungano wa NATO.Nchi hizi mbili zinashirikiana katika miradi na mikataba mbali mbali ya ulinzi.
Mwaka jana, Ukraine ilikubali kununua karveti nne-meli ndogo za kivita zinazojulikana kwa uwezo wao.
Nchi hizo kwa pamoja zinazalisha vyombo hivyo.
Inapokabiliwa na uhasama katika miji mikuu ya nchi za Magharibi, Ankara inaiona Ukraine kama mshirika katika maendeleo ya teknolojia ya kijeshi katika kila kitu kutoka kwa satelaiti na rada hadi makombora.
Wataalam wanasema moja ya maeneo ya juu zaidi ya ushirikiano ni utengenezaji wa injini na muundo. Uturuki inafanya kazi na kampuni za Ukraine kutengeneza injini za dizeli kwa ndege yake ya kivita ya kizazi cha tano na manowari ya kivita
Lakini ni ununuzi wa Ukraine wa ndege zisizo na rubani za Uturuki, ambazo wataalam wa kijeshi na wachambuzi wanaangalia kwa karibu, haswa wakati mvutano katika mashariki mwa Ukraine unapozidi kupamba moto.
Uturuki imejiweka kama muuzaji mkuu wa UCAVs (ndege za angani zisizo na rubani ) kuzitumia kwa mafanikio kwenye vita huko Syria, Libya, na Nagorno-Karabakh. Katika mzozo wa mwisho, droni ya Uturuki ya Bayraktar TB2 inasifiwa sana kwa kuisaidia Azerbaijan katika vita vya nchi hiyo na Armenia.












