Kirusi Kipya cha Covid-19: Israeli kuweka marufuku kwa wageni wote kuingia nchini humo

Chanzo cha picha, Reuters
Israel itapiga marufuku wageni kuingia nchini kwa siku 14 na kufanya ufuatiliaji ili kuzuia kuenea kwa aina mpya ya virusi vya Covid, vyombo vya habari vya ndani vimeeleza .
Marufuku hiyo inatarajiwa kuanza kutekelezwa saa sita usiku siku ya Jumapili, baada ya idhini kamili ya baraza la mawaziri.
Israel hadi sasa imethibitisha kuwa na mtu mmoja mwenye maambukizi ya kirusi aina ya Omicron inayoweza kuambukiza zaidi iliyogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini.
Nchi nyingi tangu wakati huo zimepiga marufuku kusafiri kwenda Afrika Kusini na nchi jirani zake.
Afrika Kusini imelalamika kwamba inaadhibiwa - badala ya kupongezwa - kwa kugundua kirusi cha Omicron mapema mwezi huu.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeonya aina hiyo mpya "ni ya wasiwasi", na ushahidi wa mapema unaonesha hatari kubwa ya maambukizi tena.
Hata hivyo, WHO imeonya dhidi ya nchi zinazoweka vikwazo vya usafiri kwa haraka, ikisema zinapaswa kuzingatia "mbinu za kisayansi".
Baraza la mawaziri linaloshughulikia janga la corona nchini Israeli lilikubaliana kuhusu msururu wa vizuizi vipya katika mkutano wa Jumamosi na linangoja idhini ya mwisho ya baraza kubwa la mawaziri.
Mbali na marufuku ya kuingia kwa wasio Waisraeli, karantini ya lazima ya siku tatu itahitajika kwa raia wote wa Israeli waliochanjwa, na karantini ya siku saba kwa wale ambao hawajachanjwa.
Baraza la mawaziri pia liliidhinisha uchunguzi wa wagonjwa waliothibitishwa kuwa na maambukizi kufanywa na wakala wa usalama wa Shin Bet wa Israeli.
Katika taarifa yake, Waziri Mkuu Naftali Bennett alisema teknolojia ya kufuatilia kwa simu simu itatumika.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapema siku ya Jumamosi, viongozi wa Israel walikuwa wameweka mataifa 50 ya Kiafrika kwenye orodha ya "hatari''.
Raia wote wa Israeli wanaorudi kutoka nchi hizo lazima wawekwe kwenye hoteli zilizoidhinishwa na serikali na kupimwa Covid.
Marufuku kwa wageni kuingia Israel kutoka nchi nyingi za Afrika iliwekwa Ijumaa.
Israel imethibitisha zaidi ya maambukizi milioni 1.3 ya Covid tangu kuanza kwa janga hilo, na zaidi ya vifo 8,100, kulingana na chuo kikuu cha Johns Hopkins cha Marekani.
Uchambuzi wa James Gallagher, mwanahabari wa masuala ya afya na sayansi
Ni hali inayoendelea kwa kasi. Wasifu wa kinasaba wa Omicron umeibua wasiwasi, lakini kuna uhaba wa data halisi ya ulimwengu ambayo inamaanisha hakuna mtu aliye na picha kamili ya kile aina hii ya kirusi inaweza kufanya.
Haijulikani ni tishio kubwa kiasi gani.
Hata hivyo, ni katika hatua hii ya awali, kwa kukosekana kwa ukweli wa uhakika na kunapokuwa na hatari ndipo serikali zinapaswa kuchukua hatua.
Tunachojua ni kwamba Omicron ina mabadiliko ambayo kinadharia yanaisaidia kuenea kwa haraka zaidi na kuna ushahidi unaoongezeka wa hilo kutokea Afrika Kusini.
Pia ina mabadiliko ambayo kinadharia hufanya chanjo kuwa na ufanisi mdogo.
Lakini hatujui inaambukiza kwa kiasi gani. Hatujui ni nini kitakachotokea wakati inakuja dhidi ya ukuta wetu muhimu wa kinga uliojengwa kupitia chanjo.
Baada ya mkutano wa dharura siku ya Ijumaa, WHO ilisema kwamba maambukizi ya kwanza yaliyothibitishwa kutoka kwa aina hii yalikusanywa tarehe 9 Novemba, yalikuwa na "idadi kubwa ya mabadiliko, ambayo yanatia wasiwasi".
WHO ilisema itachukua wiki chache kuelewa athari za aina hii mpya, kwani wanasayansi walifanya kazi kubaini jinsi inavyoweza kuambukizwa.
Mkuu wa Chama cha Madaktari cha Afrika Kusini aliiambia BBC kwamba kesi zilizopatikana hadi sasa nchini Afrika Kusini - ambapo ni takriban 24% ya watu wote wamepatiwa chanjo kamili - hazikuwa kali, lakini alisema uchunguzi kuhusu aina mpya ya kirusi bado uko katika hatua ya awali. .













