Kirusi Kipya cha Covid-19: Aina ya mpya ya kirusi yatajwa kuwa ni 'ya kutia hofu' na kuitwa Omicron

Train used as vaccination centre in East Rand, South Africa

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Ni Waafrika Kusini wapatao 24% tu ambao wamepata chanjo kamili hadi sasa

Shirika la afya duniani (WHO) limetangaza aina mpya ya kirusi cha corona kuwa "ya kutia hofu" na kuipatia jina Omicron.

Kina orodha ndefu ya mabadiliko ya kimaumbile, na tayari Ushahidi unaonyesha kuongezeka kwa hatari ya ongezeko la maambukizi mengine tena imesema WHO.

Kwa mara ya kwanza aina hii iliripotiwa kwa WHO kutoka Afrika Kusini tarehe 24 Novemba, na imebainika pia katika mataifa ya Botswana, Ubelgiji, Hong Kong na Israeli.

Nchi kadhaa duniani sasa zimeamua kuweka marufuku au kuweka masharti ya usafiri ya kutoka au kuelekea nchini Afrika Kusini.

Wasafiri kutoka Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe, Lesotho na Eswatini hawataweza kuingia nchini Uingereza isipokuwa kama watakuwa ni raia wa Uingereza na Ireland au wakazi wa Uingereza.

Maafisa wa Marekani wamesema kuwa safari za kutoka Afrika Kusini, Botswana, Zimbabwe, Namibia, Lesotho, Eswatini, Msumbiji na Malawi zitazuiwa, uamuazi huu ukiwa ni sawa na ule uliochukuliwa awali na Muungano wa Ulaya (EU). Hatua hii itaanza kutekelezwa kuanzia Jumatatu.

Brazil na Australia pia zimeanzisha masharti ya usafiri.

'Habari mbaya - lakini sio siku ya mwisho'

Ijumaa, WHO ilisema idadi ya visa vya aina mpya ya virusi vya corona, ambavyo awali vilipewa jina la B.1.1.529, inaonekana kuongezeka katika karibu majimbo yote ya Afrika Kusini.

"Aina hii ina orodha ndefu ya mabadiriko, ambayo baadhi yake ni ya kuhofia," lilisema shirika hilo la Umoja wa Mataifa la afya.

Virusi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Virusi vya corona

WHO imesema itachukua wiki kadhaa kuelewa athari za kirusi kipya, huku wanasayansi wakifanya juhudi za kubaini ni kwa jinsi gani kinasambaa.

Afisa wa ngazi ya juu wa Uingereza alionya kuwa chanjo ''huenda'' zisiwe na ufanisi dhidi ya aina mpya ya virusi vya corona.

Lakini Profesa James Naismith, mwanabaiolojia wa mmaumbile kutoka Chuo kikuu cha Oxford, aliongeza kuwa: "Ni habari mbaya lakini sio mwisho wa dunia ."

Alisema mabadiliko ya muundo au maumbile katika aina mpya ya kirusi yanaonyesha kuwa kinaweza kusambaa haraka zaidi-lakini usambaaji "sio rahisi wa njia rahisi kama 'inavyosambaa amino acid '" na usambaaji wake ulitegemea ni jinsi gani mabadiliko haya yanavyofanya kazi pamoja.

Ni takriban 24% ya watu Afrika Kusini waliopata chanjo kamili, jambo linaloweza kuchochea ongezeko la haraka la visa huku, Dkt Mike Tildesley, mjumbe wa kikundi cha Scientific Pandemic Influenza Modelling (Spi-M), aliiambia BBC Ijumaa.

Wakati huo huo ,Mkuu wa masuala ya magonjwa ya maambukizi nchini Marekani Dkt Anthony Fauci alisema kuwa huku ripoti kuhusu aina mpya ya kirusi zikiashiria ''hatari'' kuna uwezekano kwamba bado chanjo inaweza kuzuwia kuugua.

"Hadi kitakapopimwa vyema…hatufahamu iwapo kinaweza kuvamia au kutovamia kinga ambayo inakulinda dhidi ya virusi", Dkt Fauci aliiambia CNN.

WHO imeonya dhidi ya nchi kuweka masharti ya kusafiri, ikisema zinapaswa kuangalia " Udhibiti wa maambukizi kwa kuzingatia mbinu za kisayansi na hatari ".

Hatahivyo, zaidi ya Uingereza, na Marekani na nchi za EU, nchi nyingine kadhaa pia zimetangaza masharti ya usafiri:

  • Australia imetangaza Jumamosi kwamba safari za ndege kutoka Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe, Botswana, Lesotho, Eswatini, the Seychelles, Malawi, na Msumbiji zitaahirishwa kwa siku 14. Raia wasio wa ambao wamekuwa katika nchi hizo watazuiwa kuingia Australia
  • Japan imetangaza kwamba kuanzia Jumamosi, wasafiri kutoka nchi nyingi za Kusini mwa Afrika watahitaji kuwekwa katika karantini kwa siku 10 na kuchukua vipimo vinne katika kipindi hicho
  • India imeagiza uchunguzi na upimaji kwa wasafiri wanaowasili kutoka katika mataifa ya Afrika Kusini, Botswana na Hong Kong
  • Iran itaweka marufuku ya wasafiri watakaotoka nchi sita ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini. Wairan watakaowasili kutoka katika eneo hilo watapokelewa baada ya kutopatikana na virusi baada ya kupimwa mara mbili, imesema televisheni ya taifa
  • •Brazil pia ilisema kuwa inaweka masharti ya kusafiri katika eneo hilo la nchi sita za Afrika

Waziri wa afya wa Afrika Kusini Joe Phaahla aliwambia aliwambia waandishi wa habari kwamba marufuku za safari za ndege "hazina sababu".