Mabadiliko ya tabia nchi yachochea Jamii hii kupata elimu

ff
Maelezo ya picha, Mwalimu Emwau Daniel mkuu wa Shule ya Msingi ya Moroto, Uganda

Kila mara msemo 'mabadiliko ya tabia nchi' unapotajwa, hisia hasi huandamana, wengi wakiwazia athari za hali ya anga zikiambatana na mambo mabaya tu. Lakini je, mabadiliko ya tabia nchi yanaweza kuwa na matokeo chanya kwa jamii?

Karibu wilayani Moroto, Karamoja, mashariki mwa Uganda. Kwa muda mrefu eneo hili lilikuwa na wakaazi maskini, jamii ya wafugaji wanaohama hama. Na kutokana na mtindo huo wa maisha, wengi wa wenyeji wa Moroto hawakuthamini elimu.

Emwau Daniel ni mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Moroto Municipal Council, iliyoasisiwa mwaka 1962. Anasema zamani shule hiyo ingekuwa na idadi ndogo tu ya wanafunzi, wengi wao wakiwa wavulana.

'Katika jami yetu, watoto wavulana walipaswa kujifunza kuchunga mifugo, na wasichana waliolewa mapema ili kuletea mali familia zao,' anaeleza Mwalimu Daniel.

Kwa miaka mingi, eneo la Moroto na Karamoja kwa ujumla lilishuhudia viwango vya juu vya joto, na mvua ilikuwa nadra sana. Hivyo hapakuwa na shughuli nyingi za kilimo. Idara ya hali ya hewa nchini Uganda imebainisha kuwa eneo hilo lilikuwa likipokea kiasi kidogo sana cha mvua, na wakati mvua iliponyesha, kulikuwa na mafuriko makubwa.

Lakini mabadiliko ya tabia nchi, yamegeuza mkondo wa hali ya maisha katika eneo lote la Karamoja, mashariki mwa Uganda. Sasa mvua inanyesha angalau mara mbili kwa mwaka. Na hii imefanya wazazi wengi kugeukia kilimo cha upanzi wa mahindi, ndizi na pia maharagwe.

'Sasa wazazi wengi wana mifugo michache sana, familia moja labda ina ng'ombe 5 tu, na wengi sasa ni wakulima,' anaeleza Mwalimu Daniel.

Kauli ya Mwalimu Emwau Daniel inaungwa mkono na Halima Cheruto, mama ya watoto 6 anayeishi wilayani Moroto, mashariki mwa Uganda.

'Siku hizi maisha yamebadilika, hatuna mifugo sana kama zamani. Mifugo iliibiwa, na pia sasa tumeanza kulima,' anasema Bi Cheruto.

oo
Maelezo ya picha, Halima Cheruto, mmoja wa wazazi wa Moroto, Uganda anayekiri maisha kubadilika kwa sasa

Mwalimu Aboyo Sarah wa shule ya msingi ya Moroto KDA anasema ni furaha sana kuona idadi ya wanafunzi wasichana ikiongezeka katika shule wilayani Moroto.

'Nikiwa mwalimu wa kike, ni shangwe sana kuona idadi ya wasichana ikiongezeka hapa shuleni, tofauti na ilivyokuwa zamani.'

Na ili kukidhi mahitaji ya jamii kadri yanavyobadilika, idadi kubwa ya wazazi wa eneo hili wamebadili mawazo na sasa idadi ya watoto wanaokwenda shuleni imeongezeka sana.

'Tofauti na ilivyokuwa zamani, sasa wavulana pamoja na wasichana wamerudi shuleni,' anasema mkurugenzi wa elimu katika wilaya ya Soroti, Paul Oputa.

ff
Maelezo ya picha, Mkurugenzi wa elimu katika wilaya ya Soroti, Uganda Paul Oputa.

Oputa anasema idadi ya wanafunzi katika shule za msingi na upili imeongezeka maradufu na hali hii huenda ikaendelea zaidi kutokana na mikakati za serikali ya Uganda ya kujenga shule zaidi na taasisi mbali za elimu kupitia wizara ya maendeleo ya eneo la Karamoja.

Na kama walivyonena wahenga, hakuna masika yasiyo na mbu, mabadiliko ya hali ya anga katika eneo hili kame la Karamoja limesababisha mabadiliko mema, na wengi wanatarajia kuwa elimu inayotolewa sasa itachangia pakubwa katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa katika eneo hili siku za usoni.