Tume huru kuchunguza shambulio la Capitol

Chanzo cha picha, Reuters
Spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi amesema bunge litaanzisha tume huru ya uchunguzi wa shambulio la Januari 06 katika jengo la bunge la Capitol, lililotekelezwa na wafuasi wa Donald Trump.
Katika barua hiyo ya wabunge, alisema tume hiyo itafanya uchunguzi mfano wa tukio la shambulio la Septemba 11 la mwaka 2001 lililotokea New York na Pentagon.
"Lazima tupate ukweli wa kile kilichotokea ," alisema.
Rais wa zamani wa Marekani Trump aliondolewa madai ya kuchochea ghasia na bunge la seneti.
Lakini Democrats na baadhi ya Republicans wanaunga mkono jitihada hizo za kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu ghasia ziizosababisha vifo vya watu watano.
Bi Pelosi amesema luteni jenerali wa jeshi la Marekani Russel Honoré kwa wiki zilizopita amekuwa akichunguza nini kinahitajika katika kuimarisha usalama wa eneo la Capitol baada kutokea kwa shambulio hilo.
"Ni wazi kutokana na uchunguzi wake na kesi ya kutokuwa na imani kwamba lazima ukweli wa kilichotokea ubainike," amesema.
Tume hiyo imesema , "tutachunguza na kuripoti ukweli na sababu ya kutokea kwa shambulizi; "kuvuruga utaratibu wa kukabidhiana madaraka kwa amani"; na utayari na vile polisi ilivyoshughulikia shambulizi la Capitol na wengine wanaohusika katika tekelezaji wa sheria.
Amesema kutokana na ripoti ya awali ya Luteni jenerali Honoré', bunge linahitaji kupata ufadhili wa ziada ili kuweza kuhakikisha usalama kwa wajumbe wake na usalama wa Capitol".
Bwana Trump ameweza kujinasua katika shitaka la pili dhidi yake - ni rais pekee aliyeweza kukabiliwa na mchakato wa mashitaka mara mbili - Siku ya Jumamosi baada ya mchunguzi wa Democrat kushindwa kupata kura za wengi zilizohitajika kupatikana na hatia.
Kura ziligawanyika kwa ukubwa kutokana na mgawanyiko wa chama, kura saba za Republicans ziliwaunga mkono maseneta 48 wa Democrats na wawili walipiga kura kumweka hatiani.
Kiongozi wa Republican katika bunge, Senata Mitch McConnell, alipiga kura dhidi ya hukumu hiyo kwa misingi ya kikatiba, lakini baada ya kura kumtangaza Bwana Trump kuhusika na shambulio lililotokea Capitol.
"Rais Trump bado anahusika na kila kitu kilichotokea wakati yuko madarakani ," Bwana McConnell aliliambia bunge. "Hajaweza kukwepa chochote mpaka sasa ."
Republicans wameonesha kuunga mkono uchunguzi huru kuhusu tukio hilo linalomuhusisha Bwana Trump, Seneta Lindsay Graham amesema.
Ameiambia Fox News siku ya Jumapili kuwa rais wa zamani alihusika na shambulio lililotokea Januari 6.
"Tabia yake baada ya uchaguzi ilikuwa ya ajabu sana," Sen Graham alisema. "tunahitaji tume ya tukio la 9/11 kuchunguza nini kilitokea na kuhakikisha kuwa hakijirudii tena."












