Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Abdel Fattah al-Burhan: Jenerali aliyetengaza mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye Jumatatu alivunja mamlaka zinazoongoza mageuzi kuelekea demokrasia nchini Sudan, aliingia madarakani baada kupinduliwa kwa Omar al Bashir mwaka 2019 na sasa anaashiria kurejea kwa utawala unoogopewa sana wa kijeshi
Wakati wa taaluma ya miaka mingi chini ya utawala wake Bashir, Burhan alipanda vyeo huku akisalia mtu asiye maarufu sana. Aliongoza kikosi cha ardhini cha Sudan kabla ya Bashir kumteua kuwa inspekta jenerali wa jeshi Februari mwaka 2019 miezi miwili kabla ya jeshi kumuondoa Bashir mamlakani.
Vyombo vya habari nchini Sudan vinasema Burhan alishiriki katika kutumwa vikosi vya Sudan nchini Yemen kama sehemu ya muungano ulioongozwa na Saudi Arabia kuanzia mwaka 2015 kupiga vita dhidi ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.
Lilikuwa jukumu muhimu lakini lililokuwa nyuma ya pazia nchini Yemen.
Willow Berridge, mwandishi wa kitabu cha "Civil Uprisings in Modern Sudan" na mhadhiri wa historia wa chuo cha Newcastle, alisema harakati nchini Yemen zilichangia Burhan kufanya kazi kwa karibu na kikosi kijulikanacho kama Rapid Support Forces au RSF.
Ilikuwa ni msaada wa RSF uliochangia Burhan kuchukua wadhifa wa juu mwaka 2019, kulingana na Berridge.
Bashir alituma wanajeshi wa Sudan nchini Yemen mwaka 2015 kama sehemu kubwa ya mabadiliko ya sera za kigeni ambapo Sudan ilivunja uhusiano wake wa muda mrefu na Iran na kujiunga na muungano ulioongozwa na Saudi Arabia.
Jeshi la Sudan lilikumbwa na maafa makubwa nchini Yemen.
Mwaka 2019 baada ya kuvunjika mazungumzo kati ya waandamanaji na baraza la mageuzi la Burhan, alizuru Misri, Milki ya Nchi za Kiarabu na Saudi Arabia.
Mataifa hayo ni wafadhili wakubwa wa Sudan na walituma dola milioni 500 kwa benki kuu kufuatia kuondolewa kwake Bashir kama sehemu ya ahadi ya msaada wa dola bilioni 3 kudumisha ushawishi wao nchini humo.
Kufuatia kupinduliwa kwake Bashir, Burhan aliapishwa kama kiongozi wa mpito nchini Sudan Aprili 11, 2019 na Agosti ya mwaka huo akakabidhiwa jukumu la kuongoza baraza lililoongoza la jeshi na raia kuelekea domokrasia kamili.
Lakini Jumatatu Burhan akiwa na sare zake za kawaida za jeshi alionekana kwenye runinga akiamrisha kuvunjwa kwa baraza la mawaziri na pia baraza huru. Alitangaza hali ya hatari nchi nzima.
Kama mwenyekiti wa baraza huru, Burhan aliye na zaidi ya miaka sitini aliboresha uhusiano kati ya Sudan na mataifa makubwa duniani na ya kikanda yakiwemo Marekani na Israel.
Februari 2020, alikutana na aliyekuwa waziri mkuu wa Israel wakati huo Benjamin Netanyahu nchini Uganda.
Hata baada ya kupinduliwa kwa Bashir, Burhan aliendelea kuwa afisa asiyejulikana, mara nyingi akiwaachia jukumu wanachama wengine wa baraza kuzungumza mbele ya kamera.
Burhan alipata mafunzo zaidi ya kijeshi nchini China.
Burhan alizaliwa mwaka 1960 katika kijiji cha Gandatu kaskazini mwa Khartoum, na kusomea taasisi ya jeshi ya Sudan na baadaye nchini Misri na Jordan.
Ameoa na ana watoto watatu.