Mapinduzi ya Sudan: Waandamanaji wauawa na makumi wengine kujeruhiwa

Angalau watu watatu wameripotiwa kufariki dunia na wengine 80 kujeruhiwa baada ya wanajeshi kufyatua risasi kwenye umati wa watu wanaopinga Jeshi kuchukua hatamu ya mamlaka Sudan. Waandamanaji waliingia mtaani baada ya vikosi vya jeshi kuuondoa utawala wa kiraia, kuwakamata viongozi wa kisiasa na kuitisha hali ya hatari siku ya Jumatatu.

Vikosi vya wanajeshi wanaripotiwa kupita nyumba kwa nyumba katika mji mkuu Khartoum wakiwakamata waandaji wa maandamano. Mapinduzi hayo yamelaaniwa kote duniani, na Marekani ilisitisha msaada wa $700m. Kiongozi wa mapinduzi hayo, Jenerali Abdel Fattah Burhan, alilaumu mizozo ya nyuma ya pazia ya kisiasa kwa hatua hiyo ya kijeshi.

Viongozi wa kiraia na wenzao wa kijeshi wamekuwa katika mzozo tangu mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir alipopinduliwa miaka miwili iliyopita. Usiku wa Jumatatu, idadi kubwa ya waandamanaji walikuwa kwenye mitaa ya Khartoum - na miji mingine - wakidai kurejeshwa kwa utawala wa kiraia, mwandishi wa BBC Kiarabu Mohamed Osman anaripoti kutoka mji mkuu.

Mwandamanaji mmoja aliyejeruhiwa aliwaambia waandishi wa habari kwamba alipigwa risasi mguuni na jeshi nje ya makao makuu ya jeshi, huku mtu mwingine akielezea wanajeshi kurusha maguruneti kwanza, kisha risasi za moto.

"Watu wawili walipoteza maisha, niliwaona kwa macho yangu," alisema Al-Tayeb Mohamed Ahmed. Muungano wa madaktari wa Sudan na wizara ya habari pia waliandika kwenye mtandao wa Facebook kwamba mauaji hayo ya risasi yalitokea nje ya kambi ya kijeshi.

Picha kutoka hospitali moja mjini humo zilionyesha watu wakiwa na mavazi yenye damu na majeraha mbalimbali. Mwanahabari wetu anasema licha ya vurugu hizo, maandamano hayo yanaonyesha dalili chache za kukoma.

Waandamanaji wamefunga barabara kwa matofali na kuwasha moto matairi. Wanawake wengi pia wanashiriki katika maandamano hayo, wakipiga kelele wakisema "hapana kwa utawala wa kijeshi". Hawataki kutawaliwa kijeshi. Uwanja wa ndege wa jiji hilo umefungwa na safari za ndege za kimataifa zimesitishwa. Mtandao na laini nyingi za simu pia ziko chini.

Wafanyakazi wa Benki Kuu wameripotiwa kugoma na kote nchini madaktari wanasemekana kukataa kufanya kazi katika hospitali zinazoendeshwa na jeshi isipokuwa katika dharura.

Viongozi wa dunia wamepokea kwa mshtuko habari za jeshi kutwaa madaraka.

Marekani imeungana na Uingereza, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, ambayo Sudan ni mwanachama, kutaka viongozi wa kisiasa ambao sasa wako katika vizuizi vya nyumbani katika maeneo yasiyojulikana waachiliwe. Miongoni mwao ni Waziri Mkuu Abdalla Hamdok na mkewe, pamoja na wajumbe wa baraza lake la mawaziri na viongozi wengine wa kiraia.

Mwandishi wetu alisema kitengo maalum cha usalama cha jeshi kilifika nyumbani kwa Waziri Mkuu mapema Jumatatu asubuhi, na kujaribu kumshawishi Bw. Hamdok akubaliane na mapinduzi, lakini alikataa. Sudan imekuwa katika makubaliano ya kugawana madaraka kati ya viongozi wa kiraia na kijeshi tangu mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir alipopinduliwa mwaka 2019.

Makubaliano hayo yamewekwa ili kuielekeza Sudan kuelekea kwenye demokrasia, lakini tangu awali kumekuwa na misukosuko na majaribio kadhaa ya mapinduzi, jaribio la mwisho ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

Jenerali Abdel Fattah Burhan, ambaye alikuwa mkuu wa makubaliano ya kugawana madaraka, lakini sasa anaongoza mapinduzi ya hivi punde zaidi, amesema kuchukua nafasi hiyo kulihitajika ili "kurekebisha mkondo wa mapinduzi" kwa sababu ya mizozo ya kisiasa. Alisema Sudan bado inathamini na kuheshimu utawala wa mpito kuelekea kwenye utawala wa kiraia, huku uchaguzi ukipangwa kufanyika Julai 2023, lakini waandamanaji hawajakubali hoja yake.