Shambulio la Septemba 11: Milima ya ajabu iliyomficha Osama Bin Laden dhidi ya Marekani na Soviet

Osama Bin Laden

Chanzo cha picha, PA Media

Maelezo ya picha, Kuvuja kwa siri ya Osama kujificha katika Milima ya Tora Bora

Baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani, Osama bin Laden, kiongozi wa kundi la Al-Qaeda alikuwa akisakwa kwa udi na uvumba na Marekani iliyooamini ndiye aliyekuwa kinara wa mashambulizi hayo katika majengo marefu pacha ya biashara jijini New York na makao makuu ya jeshi, Pentagon.

Rais wa Marekani wakati huo George Bush alitangaza siku ya Oktoba 7, 2001 kuanza kwa vita dhidi ya ugaidi na kuwasaka waliohusika na mashambulizi hayo yaliyoua watu zaidi ya 3,000.

Mlengwa mkubwa alikuwa Osama bin laden aliyekuwa nchini Afghanistan na kundi lake la Al-qaeda waliokuwa wanaungwa mkono na kundi la Taliban waliokuwa wanaongoza sehemu kubwa ya Afghanistan.

Osama aliuawa Mei 2, 2011 huko Abbottabad, Pakistan katika operesheni maalumu ya kimya kimya iliyoendeshwa na vikosi vya Marekani, chini ya Utawala wa Barack Obama, miaka 10 tangu operesheni iliyoanzishwa na Bush kuanza.

Kwa miaka zaidi ya 10 Osama aliwasumbua sana majeshi ya Marekani na washirika wake wakimtafuta. Tangu tukio la Septemba 11, 2001, Osama alikuwa lulu na kuonekana kwake kulikuwa kwa nadra sana tofauti na awali.

Osama Bin Laden
Maelezo ya picha, Osama Bin Laden

Taarifa kutoka kwa Jeshi la Marekani, waandishi wanaoaminika na baadhi ya wananchi wa Afghanistan walithibitisha kiongozi huyo wa Al-Qaeda ameonekana katika maeneo kadhaa ya Tora bora.

Alionekana huko Khost, Mashariki mwa Afghanistan siku ya Septemba 11, 2001. Novemba 8, 2001 akiwa na kiongozi mwingine wa Alqaeda Ayman Mohamed Rabie al-Zawahiri walikutana huko Kabul na Hamid Mir, mwandishi anayeheshimika Pakistan. Wakati huo Vikosi vya jeshi la Marekani vilikuwa vinakaribia kuingia mji wa Kabul.

Viongozi hao wa Al qaeda walienda kwenye maziko ya kiongozi wa wapiganaji wa Uzbek, Juma Khan Namangani, aliyeuawa na mashambulizi ya ndege ya Marekani.

Baada ya hapo , Osama alikuwa kama mzimu, hakuonekana tena na ikaelezwa alienda kujificha kwenye milima ya Tora Bora.

Kwa nini Milima ya Tora bora?

Katika vita vya miaka ya 1980s, Osama alipokuwa anakabiliana na wasoviet nchini Afghanistan, aliitumia milima hii kama sehemu muhimu ya kujificha na kuendesha mapambano.

Alitengeneza barabara ya vumbi kutoka Jalalabad mpaka Torabora na alitumia mitambo mikubwa kuboresha mapango ya asili na kuchimba mengine mapya.

t

Chanzo cha picha, Getty Images

Alisimamia mwenyewe zoezi hilo la kutengeneza miundo mbinu ya milima hiyo na kuunganisha mahandaki ambayo wapiganaji wake wanaweza kutoka eneo moja mpaka eneo lingine bila kujulikana na bila kulazimika kutoka nje.

Walitumia mapango haya dhidi ya vikosi vya wasoviet.

Siri kubwa ya milima hii ni kwamba unaweza kuifikia na usione njia ya kuingia kwenye mapango. Zilitengenezwa njia nyembamba sana katika miamba ambayo kwa mgeni unaweza kupuuza uwepo wake.

Wasoviet waliiona milima lakini hawakuona wapiganaji, walikuwa wakikaribia wanasikia milio ya risasi ikishambulia, lakini hawaoni watu.

Waliona maajabu na Wasoveti wengi walisumbuka dhidi ya wapiganaji wa Mujahideen na ikawalazimu kutumia makombora lakini bado walikutana na upinzani mkali.

Makazi ya Bin

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Polisi wa Pakistani wakilinda makazi ya Bin Lade baada ya shambulio la 2011.

Baada ya vita vya Soviet nchini Afghanistan vilivyodumu karibu miaka 9, bin Laden ni kama alishinda kwa sababu kiongozi wa nane na wa mwisho wa muungano wa Soviet, Mikhail Sergeyevich Gorbachev aliamua kuondoa vikosi vya wasoviet alipogundua vinatumia fedha nyingi na kutikisa uchumi.

Akasaini mkataba wa Amani na kuondoa kikosi cha mwisho kwenye ardhi ya Afghanistan Februari 15, 1989.

Baada ya vita vya wasoviet mwaka 1989, Osama aliendelea na shughuli za kuimarisha kundi lake na sasa alielekeza nguvu nchini Sudan ambapo alilazimika kuondoka mwaka 1996 kurudi Jalalabad, Afghanistan kwa ndege binafsi kutokana na msukumo wa vikosi vya Marekani na NATO vilivyokuwa vinakabiliana na magaidi nchini Sudan.

Alivyorudi akaenda tena Tora bora, Osama alirudi na nguvu zaidi na kuanza kujenga kambi kubwa ya wapiganaji. Akajenga jengo kubwa kwa ajili yake, familia yake na viongozi wajuu wa Al-qaeda huko Torabora.

Kulikuwa na vyumba vingi vingine vimejengwa futi 350 ndani ya milima ya Tora bora.

Kuvuja kwa siri ya Osama kujificha katika Milima ya Tora Bora

Milima ya Tora bora, inapatikana kwenye wilaya inayoitwa Tora bora, iliyopo maili 30 kutoka kusini mashariki mwa mji wa Jalalabad. Milima hii inamuundo wa ajabu lakini pendwa kivita, ukiwa na mapango makubwa na mawe yanayotumika kama kificho cha wapiganaji wa Al-qaeda.

Milima hii imesambaa kwa urefu wa maili 6, ikiitwa milima mieupe kutokana na muonekano wake ukiwa na mabonde membamba. Milima hii ina vilele vinavyofikia urefu wa futi 14,000 kwa pamoja.

Marekani waliamini kabisa kwamba bin laden lazima akimbilie kwenye milima ya Tora bora. Lakini ilikua vigumu kwa Marekani kubaini ni lini ataenda kwenye milima hiyo licha ya ujasusi wa hali ya juu iliyokuwa nayo.

Baadaye Shirika la ujasui la Marekani (CIA) likapata ushahidi wa kutosha kwamba bina Laden amekimbilia kwenye milima hiyo mwishoni mwa mwezi Novemba.

t

Chanzo cha picha, Gety

Ukiacha CIA, Peter Bergen, Mmarekani wa mwisho kumuhoji bin Laden, alisema kwamba bina Laden alikimbilia Tora bora mwezi Novemba 2001, akiwa na wapiganaji na walinzi kati ya 1,000 na 1,500

Katika mahojiano ya televisheni Novemba 29, 2001, Makamu wa Rais wa Marekani wakati huo, Dick Cheney alisema anaamini kiongozi huyo wa Al Qaeda leader kajificha kwenye milima ya Tora Bora.

'Ameambatana na kundi kubwa la wapiganaji,kundi kubwa la walinzi binafsi analoliamini , na anatarajia kukimbia kuvuka nje ya mipaka, lakini hilo haliwezi kuwa rahisi kama ingekuwa miezi michache iliyopita', alisema Cheney.

Wakazi wa wilaya ya Tora bora waliokuwa wanawapelekea chakula na mahitaji mengine Al-qaeda katika mapango ya milima hiyo, pia walithibitisha uwepo wa Osama na kundi lake kwenye mapango ya Tora Bora

Vita vya Tora bora kumtoa mafichoni Osama

Kuonekana kwa Osama, kulikuwa kwa dhahabu. Taarifa za kuwepo kwake Tora bora ilikuwa taarifa muhimu kwa vikosi vya Marekani vilivyokuwa vinamtafuta kwa udi na uvumba.

Mmoja wa wanajeshi wa zamani wa Marekani Dalton Fury (sio jina lake halisi, akielezea uzoefu wake katika vita hiyo kupitia kitabu kinachoitwa 'Kill Bin Laden' kilichochapishwa mwaka 2008,Fury aliyekuwa anaongoza vikosi vya operesheni maalumu vipatavyo 90 anasema walijua bin Laden kajificha Tora bora.

Fury anasema walijua hivyo kwa sababu wapiganaji wa Ql qaeda walitumia mawasiliano ya simu ambayo hayakkuwa na udhibiti wowote, hivyo ikawa rahisi kuingilia mawasiliano yao na kuwasikiliza wakizungumza wakiwa ndani ya milima ya Tora bora.

Fury anasema walitumia baadhi ya wanajeshi kwa msaada wa wenyeji kuvaa na kuweka ndevu na kubeba silaha kuonekana kama wenyeji kumbe walikuwa wanajeshi wa Marekani. Waliambatana na kundi la wenyeji ili wasijulikane.

Wenyeji walipewa Vifaa maalumu vidogo (GPS) walivyoenda navyo kwenye milima hiyo kupeleka chakula. Walielekezwa wanapoona sehemu yenye wapiganaji wengi wabonyeze kifaa hicho, ambacho kilirekodi sehemu hiyo ili kuwasaidia wamarekani kuilenga kwa bomu.

Wenyeji hao walilipwa kwa kazi hiyo, ambayo ilifanikiwa na Marekani iliendesha mashambulio ya mabomu kwa kiwango kikumbwa na kusambaratisha eneo kubwa la milima hiyo. Lakini hawakufanikiwa kusambaratisha Al-qaeda.

Desemba 9, ndege iliyobeba mabomu ya C-130 ilidondosha bomu kubwa kwenye milima hiyo lenye uzito wa zaidi ya tani 6 na kusababisha vumbi kubwa karibu wilaya nzima ya Tora bora. Bomu hilo linaitwa Daisy Cutter, lilikuw alinatumika kwa mara ya kwanza tangu vita vya Vietnam.

Bomu hili, lilisaidia kuuua wapiganaji wengi wa Al-qaeda na wengine kukamatwa, kutokana na mapango hayo kushika moto, na kuwa na moto kubwa.

Kwa mujibu wa Furry Disemba 11, 2001, Osama alisikika kwenye radio akiwasiliana na wapiganaji wake, akiwaambia waendelee na mapambano ingawa aliwaomba radhi kwa kuwasababisha kukwama kwenye mtego wa Marekani.

Fury anasema mpaka katikati ya mwezi disemba bin Laden alikuwa amejificha ndani ya Tora bora. ``Hakuna mashaka kwamba bin Laden alikuwa Tora Bora

Wakati wa mapigano,'' aliandika katika kitabu hicho cha Kill Bin Laden.

Hata hivyo, baada ya bomu hilo lililoonekana kusambaratisha kundi hilo la Al-qaeda ikatangazwa vita vya Tora bora kumalizika, lakini kumbe ilikua ujanja wa baadhi ya wanajeshi wasiokuwa waaminifu kwa Marekani kuruhusu Osama bin Laden kutoroka na kukimbilia Pakistan.

Milima ya Tora bora iliyompakani mwa Pakistan ikawa salama ya bina Laden, iliyomsaidia kuvuka mpaka. Hakupatikana tena mpaka baada ya miaka 10 alipouawa huko Abbottabad, Pakistan na majeshi ya Marekani yaliyomfuata kimya kimya.