Vita vya Afghanistan : Hakuna uhakika kama Taliban watabadilika

Jenerali Mark Milley

Chanzo cha picha, Getty Images

Jenerali Mkuu wa Marekani amewaelezea Taliban kama "kundi lisilo na huruma" na anasema haijulikani ikiwa watabadilika.

Jenerali Mark Milley amesema, hata hivyo, ilikuwa "inawezekana" kwamba Marekani ingeweza kushirikiana na wanamgambo wa Kiislamu kwenya operesheni za baadaye za kupambana na ugaidi.

Vikosi vya Marekani vilijiondoa kutoka Afghanistan Jumanne, na kumaliza vita virefu zaidi vya Marekani miaka 20 baada ya kuanzisha uvamizi wa kuwaondoa Wataliban.

Wanamgambo wa Kiislamu sasa wanadhibiti nchi hiyo na wanatarajiwa kutangaza serikali mpya.

Jenerali Milley alikuwa akizungumza pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Merika Lloyd Austin, katika matamshi yao ya kwanza ya umma tangu wanajeshi wa mwisho waliondoka Afghanistan.

Rais wa Marekani Joe Biden amekosolewa sana kuhusu kuondoka 'ghafla' , ambako kulisababisha kuporomoka bila kutarajiwa kwa vikosi vya usalama vya Afghanistan ambavyo Marekani ilikuwa imevifundisha na kuvifadhili kwa miaka.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano, Jenerali Milley na Katibu Austin waliwasifu wanajeshi ambao walikuwa wamehudumu Afghanistan na ujumbe mkubwa wa uokoaji.

Mwanamgambo wa Taliban

Chanzo cha picha, EPA

Alipoulizwa juu ya uratibu kati yao na Taliban katika kufanikisha watu wanaoondoka kwenda uwanja wa ndege, Bwana Austin alisema: "Tulikuwa tukifanya kazi na Taliban juu ya suala hilo tu -kuwaondosha watu wengi kadiri iwezekanavyo.''

"Katika vita unafanya kile cha lazima ili kupunguza hatari ya matumzizi ya nguvu, sio lazima kile unachotaka kufanya," Jenerali Milley aliongeza.

Alisema kuwa inawezekana kwamba Marekani ingeweza kushirikiana na Taliban juu ya hatua ya baadaye dhidi ya mshirika wa IS, IS-K, kundi ambalo lilikiri kufanya shambulio nje ya uwanja wa ndege wa Kabul wiki iliyopita ambalo liliwauwa watu 170, pamoja na wafanyakazi 13 wa jeshi la Marekani.

IS-K kikundi kibaya zaidi cha wapiganaji wa jihadi nchini Afghanistan. Ina tofauti kubwa na Taliban, ikiwashutumu kwa kuacha jihadi na uwanja wa vita.

Bwana Austin, wakati huo huo, alisema "hatataka kutoa utabiri wowote" juu ya ushirikiano wa baadaye. Lakini akaongeza kuwa maafisa "watafanya kila tuwezalo kuhakikisha tunabaki tukizingatia [IS-K], kuelewa mtandao huo, na wakati wa kuchagua kwetu siku za usoni, wawajibike kwa kile walichofanya" .

Kwa jumla, shughuli ya uokoaji ilishuhudia zaidi ya watu 123,000 waliotaka kukimbia Taliban wakiondoshwa nchini humo kwa ndege.

Marekani inakadiria kuwa kuna Wamarekani kati ya 100 na 200 bado wako Afghanistan.

Marekani chini ya Waziri wa nchi wa mambo ya Kisiasa Victoria Nuland alisema "chaguzi zote zinazowezekana" zinaangaliwa ili kuwapata raia wa Marekani waliosalia na watu ambao walifanya kazi na Maekani nje ya nchi.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab alisema hakuwa na uhakika ni raia wangapi wa Uingereza waliobaki Afghanistan lakini kwamba inaaminika kuwa ''chini ya 100''.

Taliban wamesherehekea kuondolewa kwa mwisho kwa vikosi vya kigeni, na sasa wanalenga kuunda serikali.

Naibu mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Taliban huko Qatar, Sher Abbas Stanekza, aliiambia BBC idhaa ya Pashto kwamba serikali mpya inaweza kutangazwa katika siku mbili zijazo.

Alisema kutakuwa na jukumu kwa wanawake katika nafasi za chini lakini sio katika nafasi za juu.

Alisema pia kwamba wale walioitumikia serikali katika miongo miwili iliyopita hawatajumuishwa.