Vita vya Afghanistan: Wanadiplomasia waharakisha kuondoka, Taliban wakaribia Kabul

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amelihutubia taifa hilo linalokumbwa na mapigano mapema Jumamosi.

"Kama rais wenu, lengo langu ni kuzuia vurugu zaidi na kufurushwa makwao kwa watu wangu," aliwaambia raia wa Afghanistan.

"Katika mazingira ya sasa, tumepatia kipaumbele hatua ya kuimarisha usalama na vikosi vya ulinzi, na juhudi zimefanywa kufikia lengo hili," alisema.

Bwana Ghani amesema hatakubali vita ambavyo "vilielekezwa" kwa watu wake "kusababisha maafa zaidi," na kupongeza "ujasiri" wa vikosi vya usalama ambavyo vimekuwa vikijaribu kulinda miji dhidi ya mashambulio ya Taliban.

Hotuba yake inakuja kukiwa na minong'ono kutoka kwa baadhi ya wandani wake kwamba huenda akatangaza kujiuzulu.

Tayari wanajeshi wa Marekani wanaelekea nchini Afghanistan kuwasaidia wafanyakazi wa kidiplomasia na wengine kuondoka huku mataifa mengine pia yaking'ang'ana kuwaondoa wafanyakazi na raia wao kuondoka licha ya wanamgambo wa Taliban kuzidisha mashambulio.

Siku ya Ijumaa, wanamgambo waliuteka mji wa Pul-e-Alam, ambao ni makao makuu ya mkoa wa Loghar, mwendo wa kilomita 80 tu (maili 50) kutoka mji mkuu wa Kabul.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema hali inaendelea kuwa mbaya hasa kwa raia ndio hatarini.

Zaidi ya watu 250,000 wamelazimika kuondoka makwao kufikia sasa.

Mashambulio ya Taliban yaliongezeka baada ya vikosi vya kigeni vikiongozwa na Marekani kuondoka nchini humo baada ya oparesheni ya kijeshi ya miaka 20.

Mapigano hayo yameibua hofu kwamba yatarudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika juhudi za kulinda haki za binadamu tangu wanamgambo hao waondolewe mamlakani mnamo 2001.

Maisha chini ya uongozi wa Taliban miaka ya 1990 yaliwalazimu wanawake kuvaa mavazi ya burka yanayofunika mwili mzima, kudhibiti elimu kwa watoto wa kike walio na zaidi ya miaka 10,na adhabu ya kikatili kiwa ni pamoja na kuuawa hadharani.

Siku ya Ijumaa pia, Taliban waliuteka mji wa Kandahar ambao ni wa pili kwa ukubwa. Wanamgambo hao sasa wanadhibiti karibu thuluthi tatu ya makao makuu ya mikoa ya Afghanistan.

Msemaji wa John Kirby ameelezea ''wasiwas wake'' kuhusu mashambulio ya hivi karibuni nchi humo na kuashiria kuwa mji mkuu wa Kabul unakabiliwa na hatari ya kutekwa na kundi hilo.

Wengi wa wanajeshi 3,000 wanaopelekwa Afghanistana wanaenda kusaidia shughuli ya kuwaondoa wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani na wanatarajiwa kuwasili nchini humo wikendi hii. Marekani inaazimia kuwaonda maelfu ya watu kutoka mjini Kabul ndani ya siku moja.

Uingereza imewapeleka wanajeshi 600 kusaidia kuwaondao raia wake na wafanyakazi wake wa zamani ambao ni raia wa Afghanistan. Pia imesema idadi ya wafanyakazi katika ubalozi wake nchini humo itapunguzw - kama ilivyofanya Ujerumani.

Denmark na Norway zinafunga balozi zao nchini Afghanistan.