Virusi vya Corona Tanzania: Tanzania kuna wagonjwa zaidi ya 100 wa wimbi jipya la corona

Mama Samia

Chanzo cha picha, EPA

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema nchi hiyo ina zaidi ya wagonjwa 100 wa wimbi la tatu la ugonjwa wa virusi vya corona.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari leo Jumatatu Juni 28, Rais Samia amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni wagonjwa takribani sabini kwa sasa "wapo kwenye matibabu ya msaada wa oksijeni."

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kutoa takwimu za mwenendo wa ugonjwa wa corona kwa mara ya kwanza toka mwezi Mei mwaka jana. Kutokutoa takwimu za corona ilikuwa ni moja ya mambo ambayo Tanzania ilikosolewa vikali na mashirika ya ndani na ya kimataifa yakiongozwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Rais Samia amesisitiza kuwa wimbi la tatu la corona ambalo linaendelea kusumbua mataifa mbalimbali duniani limeingia pia Tanzania na kuwataka wananchi kuchukua hatua za tahadhari kama inavyoshauriwa na wataalamu.

"...Ukiangalia (wagonjwa) si wengi, lakini inabidi tufanye jitihada za kujikinga ili wasiongezeke...inabidi tuchukue hadhari zote kama tulivyofanya katika wimbi la kwanza," amesisitiza rais Samia.

Kuagizwa kwa chanjo Tanzania

Kwa mujibu wa Rais Samia, tayari Tanzania imeshatuma maombi ya kujiunga na mpango wa uagizaji wa chanjo kwa nchi zenye uchumi mdogo wa COVAX.

Kujiunga na mpango huo wa uagizwaji wa chanjo ulikuwa ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa na kamati aliyoiunda siku chache baada ya kuingia madarakani.

Chanjo

Chanzo cha picha, Getty Images

" Ilibidi tutume maombi ya kujiunga na COVAX kabla ya Juni 15 ili tuweze kupata chanjo kufikia mwaka 2022... kwa waliochelewa kutuma maombi mpaka tarehe hiyo maana yake wataingizwa kwenye mpango huo kufikia mwaka 2023. Kwa hiyo tuliona kwanza tujiunge na mpango," ameeleza Rais Samia.

Mkuu wa WHO kwa Kanda ya Afrika Dkt Matshidiso Moeti hivi karibuni aliwaambia wanahabari kuwa chanjo zinaweza kuingia Tanzania ndani ya wiki kadhaa baada ya nchi hiyo kujiunga rasmi na mpango wa COVAX. WHO ni moja ya waratibu wakuu wa mpango huo.

Rais Samia pia ameeleza kuwa hivi karibuni uongozi wa juu wa Tanzania umekubaliana kupitia kikao cha baraza la mawaziri kuwa chanjo itakuwa ya hiyari.

"Tutaenda na ulimwengu unavyotaka, tuchanje watu wetu, atakayetaka achanjwe, asiyetaka sawa. Hakuna atakayelazimishwa."

Rais huyo pia amesema kuna mashirika ya kimataifa na nchi kadhaa ambazo zimejitolea kuipa Tanzania msaada wa chanjo.

"Huu hautakua msaada tu wa kupokea, lazima wataalamu wetu wazikague chanjo hizo na kutushauri kabla ya kuzipokea," amesisitiza rais Samia.

Je, vipi kuhusu katiba mpya na mikutano ya hadhara ya kisiasa?

Katika mkutano huo na wahariri liliibuka pia suala la mikutano ya hadhara ya vymama vya siasa mabyo ilipigwa marufuku miaka mitano iliyopita na mtangulizi wake hayati Rais John Magufuli pamoja na mchakato wa katiba mpya.

Kuhusu lini atashughulikia masuala hayo, Rais Samia ametaka apewe muda kwanza kushughulikia masuala ya uchumi.

Maelezo ya video, Samia Suluhu Hassan: Mabadiliko ya sura ya kisiasa Tanzania

"Naomba nipeni muda kwanza nisimamishe nchi kiuchumi, tuite wawekezaji wawekeze, ajira zipatikane, halafu tutashughulikia masuala mengine," amesema na kuongeza: "Tutashughulikia katiba, tutashughulikia mikutano ya hadhara, wakati ukifika."

Hata hivyo amesema sasa vyama vya siasa vipo huru kufanya mikutano na watu wao, mikutano ya ndani, kamati kuu zinakaa, Halmashauri kuu za vyama vya siasa pia zinakutana. Sambamba na hilo wameruhusu pia wabunge kwenye maeneo yao kufanya mikutano ya hadhara.

''Uchumi wetu ni suala la maana zaidi kuliko mengine, sisemi kwamba katiba si ya maana, lakini ninaomba nipeni mud, niisimamishe Tanzania kiuchumi kwanza halafu tutatazama na mengine," alifafanua Rais Samia.