Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya Corona: WHO yasema chanjo ya corona inaweza kufika Tanzania ndani ya wiki mbili
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa limepokea taarifa rasmi ya Tanzania kuomba kujiunga na mpango wa COVAX unaolenga kuhakikisha nchi masikini kote duniani zinapata mgao sawa wa chanjo.
Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika Dkt Matshidiso Moeti amesema hii leo kuwa chanjo hizo zinaweza kuingia Tanzania katika kipindi cha wiki mbili.
"Tumepata taarifa kuwa sasa ni rasmi Tanzania ipo katika mchakato wa kujiunga na mpango wa chanjo wa COVAX," Dkt Moeti ameuleza mkutano wa waandishi wa habari hii leo.
Hatua hiyo inaendana na mapendekezo ya kamati maalumu ya ushauri ambayo iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan punde tu baada ya kuingia madarakani mwezi Machi mwaka huu.
Mwezi mmoja uliopita, Mei 17 kamati hiyo ilitoa mukhtasari wa taarifa yake na kushauri serikali kupitia vyombo vyake kulishughulikia suala la chanjo kwa kujiunga na mpango wa covax ulio chini ya mwamvuli wa Gavi.
Mpango wa covax unalenga kuhakikisha nchi masikini kote duniani zinapata mgao sawa wa chanjo licha ya ufinyu wa uwezo wao wa kiuchumi. Mwamvuli wa Gavi unaundwa na mashirika mbalimbali ikiwemo Shirika la Afya Duniani na baadhi ya serikali za nchi tajiri duniani.
"Kamati inashauri Serikali kwa kutumia vyombo vyake iendelee na hatua kuelekea kuruhusu matumizi huru ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kwa kutumia chanjo zilizoorodheshwa na Shirika la Afya Duniani ili kuwapa fursa ya kinga wananchi wake kwa kuwa kupitia uchambuzi wa Kamati, chanjo hizo zina ufanisi na usalama unaokubalika kisayansi," alieleza Profesa Said Aboud kutoka Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili na Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Rais Samia amechukua mkondo tofauti na wa mtangulizi wake hayati John Magufuli katika kulishughulikia janga la corona. Wakati Rais Magufuli alikosolewa kwa kutokufuata moja kwa moja mapendekezo ya kisayansi yaliyothibitishwa na WHO, Rais Samia amejipambanua kutaka kuendana na ulimwengu katika kufuata njia zinazopigiwa chapuo na WHO.
Afisa Mwandamizi wa mpango wa chanjo wa WHO kwa kanda ya Afrika Richard Mihigo amewaambia wanahabari katika mkutano wa leo uliofanyika mtandaoni kuwa tayari Tanzania imekamilisha hatua za awali za kutuma maombi ya chanjo kutoka COVAX na inaandaa mpango wa kupokea na kugawa chanjo.
Msemaji wa Serikali ya Tanzania Gerson Msigwa hata hivyo hakukanusha au kuthibitisha suala hilo alipozungumza na BBC akisisitiza kuwa serikali itatoa taarifa rasmi kwa umma muda muafaka utakapofika juu ya suala hilo.