Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya Corona: IMF yathibitisha itatoa mkopo Tanzania ikitoa takwimu za hali ya corona
Shirika la Fedha Duniani (IMF) limethibitisha kwamba litaipatia Tanzania mkopo wa dharura wa takribani dola milioni 574, itakapokamilisha mambo muhimu ikiwemo utoaji wa takwimu kuhusu maambukizi ya virusi vya Corona.
Mara ya mwisho Tanzania kutoa takwimu kuhusu maambukizi ya virusi hivyo na ugonjwa wa Covid 19 kwa ujumla ilikuwa mwezi Mei mwaka 2020.
Mwakilishi mkazi wa IMF nchini Tanzania, Jens Reinke ameiambia BBC kwamba, moja ya vigezo vya utoaji wa mkopo wa aina hiyo ni pamoja na takwimu muhimu kuhusu Covid 19 ili kujua hali halisi ya maambuziki ya ugonjwa huo ikoje kwa sasa nchini Tanzania.
"Uwepo wa takwimu ni nyenzo muhimu sana katika kukabiliana na janga hili, na zitawasilishwa kwenye bodi ya IMF kabla ya kuthibitisha, kwa hiyo kuwa na takwimu za msingi, ni kigezo cha moja kwa moja", alisema Reinke.
Mwezi Machi 2020 Serikali ya Tanzania iliiomba IMF mkopo huo wa dharura kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo bila mafanikio, kufuatia mazungumzo hayo kuishia njiani. Mwezi Machi mwaka huu, serikali ya Tanzania ilihuisha tena ombi hilo.
Hata hivyo, mwakilishi huyo wa IMF, Reinke amesema bado mchakato ni mrefu kabla ya kuidhinishwa kwa mkopo huo kwa Tanzania, akisema yapo mambo mengi ya kuzingatiwa mbali na utoaji wa takwimu.
"Hatuko karibu sana kuidhinisha chochote kwa Tanzania, tunaendelea na majadiliano," alisisitiza.
Baada ya kuingia madarakani mwezi Machi mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha nia ya wazi ya kushughulikia janga la Corona, kwa kuanza kuunda Kamati Maalumu iliyowasilisha ripoti yake hivi karibuni, ambapo pamoja na mambo mengine kamati hiyo ilipendekeza kuhusu uingizwaji wa chanjo na utolewaji wa takwimu za maambukizi ya ugonjwa huo.
"Serikali itoe takwimu sahihi za ugonjwa wa COVID-19 kwa umma na Shirika la Afya Duniani ili wananchi wapate taarifa sahihi toka Mamlaka za Serikali na kuheshimu makubaliano na kanuni ambazo nchi iliridhia," ilishauri kamati hiyo chini ya Mwenyekiti, Profesa Said Aboud kutoka Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili.
Tanzania iliacha kutoa takwimu mwaka jana, baada ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, hayati John Magufuli kusema kwamba, nchi hiyo haina maambukizi ya Corona, kufuatia maombi maalumu ya siku tatu yaliyofanywa kitaifa ili kuondokana na ugonjwa wa Covid 19.
Shirika la Afya Duniani WHO, nalo mapema mwaka huu lilitoa wito kwa mamlaka nchini humo kuanza kutoa takwimu za watu waliambukizwa ugonjwa wa Covid 19 likisema itasaidia kuwakinga Watanzania na wale wanaotangamana nao.
Kama alivyonukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari hivi karibuni, Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, alisema serikali hiyo inatarajiwa kutoa muongozo wake kuhusu ugonjwa huo wakati wowote ikiwemo masuala ya chanjo na takwimu.