Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Baye Modou Fall: Mfungwa wa Senegal aliyetoroka jela mara 12
Mfungwa mmoja nchini Senegal amezua gumzo katika taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya kudai kwamba alitoroka jela mara 12.
Baye Modou Fall alisimulia Televisheni ya Senegal jinsi alivyofanikiwa kutoroka jela.
Anasema amekuwa akisubiri kufunguliwa mashtaka kwa takriban miaka tisa. Baadhi ya mawakili wanasema kisa hicho ni ishara kwamba mfumo wa haki nchini Senegal unahitaji kufanyiwa marekebisho.
Lakini je Baye Modou Fall ni nani?
Mwanamume huyo aliye na umri wa miaka 32-anajieleza kuwa mfanyabiashara, baada ya kurithi mali kutoka kwa marehemu baba yake.
Lakini amekuwa akiingia na kutoka jela tangu alipokuwa mtoto mdogo, hasa kutokana na tuhuma za wizi.
Anasisitiza kwamba hana fujo na wala hatumii silaha.
Hajasoma lakini aliwahi kupata mafunzo ya kidini (madrasa) kabla ya kujifunza kompyuta katika taasisi tofauti.
Mara ya kwanza alikamatwa nyumbani kwao Diourbel, kilomita 160 sawa na (maili 100) mashariki mwa mji mkuu wa Dakar.
Na mara ya kwanza alitoroka katika kituo cha Diourbel.
Alijipata mashakani mara kadhaa kabla ya kukamatwa mwaka 2015 lakini mwaka uliofuatia alifanikiwa kutorokea Gambia. Huko pia alizuiliwa lakini serikali ilikataa kumrudisha nchini Senegal.
Baada ya miezi mitano chini Gambia, alikamatwa tena Senegal, karibu na mpaka wa Guinea.
Miaka minne baadaye alikamatwa baada ya kupatikana na kosa la wizi mwezi Novemba mwaka 2020. Lakini alisubiri kufunguliwa mashtaka kadhaa wakati alipotoroka jela wiki iliyopita.
Mamlaka haijathibitisha madai ya Fall kwamba alitoroka jela mara 12. Wakili wake wa zamani, Abdoulaye Babou, ameiambia BBC huenda ametoroka karibu mara 10.
'Sio superman'
Nchini Senegal amepewa jina la utani la Boy Djinné, linalomaanisha Kijana wa Kiajabu katika lugha ya Wolof, lakini wakili wake wa zamani anadhani jina hilo haliendani na tabia yake.
"Vyombo vya habari vimemfanya kuwa superman. Hana uwezo wowote wa kiajabu," Bw Babou anasema.
"Hana muonekano wa ''kibabe''. Ni mwembamba sana, mfupi na mwenye haya sana.
"Hawezi kukuangalia machoni. Sio jambazi. Hajawahi kumuua mtu yeyote," anasisitiza Bw. Babou, ambaye amemtetea Fall kwa miaka 10.
Baada ya kutoroka mara ya mwisho, Fall alisema katika mahojiano ya televisheni kuwa alitoroka kwasababu kesi dhidi yake ilichukua muda mrefu sana kuamuliwa.
Anasema alikuwa jela kwa miaka tisa akisubiri mashataka ya wizi na kukwepa mamlaka.
"Kosa la kutoroka ni kesi nyingine, Najua hilo. Lakini kwa sababu nimezuiliwa kwa miaka tisa bila kufanyiwa lolote, sikuwa na budi kutoroka. Napigania ukweli ujulikane. Niliamua kuchukua hatua mikononi mwangu.
"Nimekuwa nikijua kwamba naweza kutoka jela wakati wowote, mchana au usiku," aliambia runinga ya ITV nchini Senegal..
"Hakuna usalama katika jela ninapozuiliwa, ijapokuwa watu wanapinga hilo.
Pia alitoa maelezo ya jinsi alivyotoroka, kwa kuvunja na kukata uzio wa chuma na kuruka ukuta wa jela kwa kutumia kamba iliyounganishwa na mlingoti wa umeme.
Anasisitiza hana washirika.
Mamlaka hata hivyo inapinga madai hayo.
Mkaguzi wa Kanda wa Usimamizi wa Mahabusu wa Dakar, Mbaye Sarr anasisitiza kwamba alikuwa katika eneo lenye usalama mkubwa wa gereza na kwamba lazima alisaidiwa kutoroka.
Anasema ameanzicha uchunguzi na walinzi waliyokuwa zamu kati ya saa kumi na moja na saa kumu na mbili (05:00 na 06:00) majira ya Afrika Magharibu, wanahojiwa.
Mkurugenzi wa gereza hilo pia amepewa majukumu mengine akisubiri uchunguzi.
Fall hatimaye alikamatwa tena siku ya Alhamisi karibu na mpaka wa nchi hiyo na Mali, ambako aliripotiwa kujaribu kutoroka kwa kutumia piki piki.
'Mhasiriwa wa mfumo mbovu'
Kisa cha Fall kinaangazia changamoto zinazokabili mfumo wa haki wa Senegal.
Kanuni za adhabu za Senegal hazitoi kikomo cha muda ambao mtuhumiwa anaweza kuzuiliwa, akingojea kesi.
"Mtu akizuiliwa, anatakiwa kuachiliwa huru au kufungwa, la sivyo wanastahili kupewa dhamana," anasema wakili wa Senegal Ousmane Sèye.
Anasema kuwa baadhi ya watu wamezuiliwa kwa kwa muda mrefu hata kabla ya kesi yao kusikizwa na kuamuliwa.
"Hii ndio sababu mfumo wa mahakama wa Senegal unahitaji kufanyiwa mageuzi."
Bw. Babou anadhani mteja wake wa zamani ni mhasiriwa na mfumo mbovu.
Kwa miaka kadhaa watetezi wa haki za binadamu wamekosoa msongamano unaoshuhudiwa katika magereza ya Senegala na kutoa wito wa kuwapunguza muda wa kuwazuilia watuhumiwa.