Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Hajira Bibi: Alimsubiri mume wake kwa miaka 33 licha ya kutojulikana alipo
"Mara ya kwanza kumtia machoni, nilimtambua niliyekuwa nikimsubiri kwa miaka 33 lakini yeye hakunitambua wala nyumbani kwake pia hakukujua".
Hayo ni maneno ya Hajira Bibi ambaye mume wake alirejea hivi karibuni nchini Pakistan kutoka Muscat Oman baada ya kutojulikana alipo tangu miaka ya 1980.
Lakini cha kusikitisha zaidi ni kwamba siku ana kutana na familia yake baada ya kipindi chote hicho, hakuweza kuitambua na wale waliokuwa wanampenda na kutamani angalau siku moja arejee, bado kwake, wao ni watu asiowajua.
Hajira Bibi aliolewa na binamu yake Karim Bakhsh zaidi ya miaka 30 iliyopita wakati huo, Karim alikuwa akifanya kazi katika hoteli moja ya eneo.
Lakini kama ilivyo kwa familia nyengine yoyote ile, mwaka 1988, wakaamua kwamba Karim atahamia eneo la Karachi kutafuta maisha.
Wakati huo tayari alikuwa ameshafunga pingu za maisha na mchumba wake ambaye alikuwa binamu yake aliyetafutiwa na wazazi wake.
Lakini usichokijua ni usiku wa kiza. Karim alipowasili Karachi, miezi ya kwanza alikuwa ana wasiliana na familia yake na aliwaandikia barua kila wakati kuwafahaisha anavyoendelea.
Ila mawasaliano hayo hayakudumu kwa muda mrefu.
Na baada ya kimya cha muda mrefu, familia yake iliamua kufunga safari na kwenda kumtafuta alipo.
Lakini kwa bahati mbaya, juhudi zao ziligonga mwamba na familia hiyo ikaamua kutoa tangazo kwamba Bwana Karim amepotea na atakayetoa taarifa kumhusu kuna zawadi nono atakayopata.
Ila vivyo hivyo, hakuna kilichobainika juu ya aliko Karim.
Kwa kipindi kirefu kupita bila yeyote kuwa na taarifa za aliko Karim, wengi wakiwemo wazazi wa Karim, walimshaur Hajira Bibi kuolewa tena na mtu mwingine.
Wasijue kwamba Hajira Bibi alikuwa ameshakata shauri kwamba hakuna atakayemsikiliza, badala yake, atamsubiri mume wake Karim Bakhsh hadi siku yake ya mwisho duniani.
Miongo kadhaa ikapita na siku moja mpwa wa Karim, Muhammad Qasim akaona video mtandaono iliyokuwa imewekwa na mtu kwa jina Sarem Burney. Katika video hiyo, Sarem Burney alikuwa anazungumzia mwanamume aliye kando yake ambaye alikuwa anatafuta familia yake.
Miongo kadhaa baadaye Muhammad Qasim amesema: "Nilijua simulizi ya mjomba wangu Karim Bakhsh. Na baada ya kuona video ile ghafla nikamkumbuka na kutaka kujua zaidi."
Kulingana na Qasim, alishuku kuwa huyo anaweza kuwa mjomba wake Karim baada ya kumuangalia alivyo kwenye video na kulinganisha na picha zake halisi akiwa mtoto na kijana alizokuwa nazo.
"Nilipowaonesha wakuu wangu na mkaza wangu (Hajira Bibi) kila mmoja alikubaliana nami kwamba alikuwa Karim Bakhsh."
Shah Nawaz ni binamu ya Karim na kaka wa Hajira Bibi. Anasema: "Baada ya kutazama video ile, karibu kila moja katika familia yetu aliwasiliana na Sarem Burney iliyekuwa Karachi na akatuongoza tutakapo kutana na ndugu yetu karim Bakhsh."
Lakini tulichogundua baada ya kukutana na ndugu yetu ni kwamba hafahamu lolote kuhusu maisha yake ya nyuma. Angejaribu kusema kitu kwa lugha yetu lakini matamshi yake hayakuwa sahihi.
Kulingana na Shah Nawaz, "Karim ni mpishi mzuri. Atakuarifu viungo vyote vya mapishi unayotaka kuanzia mwanzo hadi mwisho."
Anasema kuwa Karim alipelekwa hospitalini na kampuni ya Sarim kupata matibabu.
Sarim iliiarifu BBC kuwa kampuni yake ilifahamishwa kumhusu Karim Bakhsh na shirika la upepelezi nchini humo.
"Maafisa wa shirika la upelelezi walisema kuwa alirejeshwa nchini Pakistan kutoka Muscat katika hali ya dharura na pasipoti aliyokuwa nayo pia ilikuwa ni ile inayotolewa kwa dharura tu".
Hakukuwa na taarifa zingine za kina zilizotolewa kumhusu au hata kuhusiana na kilichopelekea kutengenezewa pasipoti ya dharura.
Kulingana na Sarem Burney, Karim alipoletwa hali yake ilikuwa mahututi.
"Baada ya kumfuatilia tuliona ishara zilizoashiria kuwa kuna mateso fulani aliyopitia hasa mwilini. Lakini hana matatizo yoyote ya akili zaidi ni kupoteza fahamu."
Karim alipata matibabu ya kina baada ya kurejea nchini mwao Pakistan na madaktari waliomtibu walisema hawana uhakika ikiwa Karim ataweza kurejesha tena kumbukumbu zake.
Pia kampuni hiyo imesema ilikuwa vigumu kutafuta famila yake kwasababu hakuwa na rekodi yoyote serikalini kwahiyo, kukawa hakuna njia nyengine zaidi ya kugeukia mtandao wa kijamii.
Baada ya video hiyo kusambaa, Sarem ilipata taarifa kuhusu maisha ya nyuma ya Karim.
"Tuliambiwa kuwa alikuwa amefungwa jela huko Muscat. Raia wawili wa Pakistan ambao walikuwa wamefungwa naye walipiga simu na kutuarifu kwamba walikuwa naye lakini hata wakati huo, kumbukumbu zake zilikuwa tayari zimepotea."
Kampuni ya Sarem imesema ilijaribu kuzungumza na Karim mara kadhaa lakini hakuna taarifa zozote za msingi walizopata kutoka kwake, alichokuwa akisema hakikuleta maana.
Lakini swali la kuwa je, Karim alikuwa wapi katika kipindi cha miaka 33 huenda likapata jawabu, Karim atakaporejesha kumbukumbu zake.
Wajomba zake Karim na jamaa zake wengine walipokwenda Karachi na kumtafuta alipokuwa akifanya kazi, wasimamizi wa kampuni iliyojulikana na familia yake walisema kuwa Karim aliacha kazi kitambo.
Hakuna aliyejua alikuwa amekwenda wapi. Wazazi wake walikuwa wakimkumbuka hadi siku zao za mwisho maishani.
Na baada ya kumtafuta kwa miezi kadhaa mjini Karachi bila mafanikio yoyote, waliamua kupiga ripoti kwa polisi.
Hata hivyo mke wake Hajira Bibi aliyemsubiri kwa miaka 30, licha ya aliyopitia na hali ya sasa ya Karim, ana imani kwamba ikiwa mume wake atapata upendo hata kidogo tu, kutunzwa vizuri na kupata matibabu, ipo siku kumbukubu zake zitarejea.
"Nitaendelea kumsubiri," Hajira Bibi amesema.