Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afungwa jela 'kimakosa' kwa miaka 68
'Kijana mdogo aliyekaa jela kwa miaka mingi zaidi Marekani' hivi karibuni alitoka gerezani na sasa ni mtu huru.
Joe Ligon alizungumza na BBC kuhusu hali ilivyokuwa katika maisha yake ya jela ya karibu miongo saba, huku akisubiri kwa muda ili aweze kupata uhuru, na mipango yake kwa siku zilizosalia za maisha yake.
"Sijawahi kuwa peke yangu, lakini kwa sasa ni mpweke zaidi. Ninapendelea kuwa peke yangu kadri itakavyowezekana. Gerezani nilikuwa katika seli ya peke yangu kuanzia siku nilipofungwa hadi kuachiliwa kwangu."
"Hii inawasaidia watu kama mimi, wanaotaka kuwa peke yao. Nilikuwa mtu ambaye, nilipoingia seli yangu na kufunga mlango, sikuona au kusikia kitu chochote kilichokua kikiendelea. Walipoturuhusu kuwa na radio na televisheni, hivyo ndivyo nilikaa navyo."
Labda ni sawa kusema kwamba maisha jela yalimfaa Ligon, kwa kiasi.
Yalimuwezesha kutofahamika, kunyamaza na kutojipata katika matatizo. Yalikuwa masomo, anasema kwamba alijifunza sana katika miaka 68 akiwa gerezani.
Na ukweli ni kwamba kukaa mbali na watu lilikuwa ni chaguo alilolifikiria.
"Sikuwa na marafiki kando yangu. Sikuwa na marafiki nje.
"Lakini watu wengi nilizungumza nao…niliwatendea kama marafiki. Na tulikuwa sawa kuwa hivyo, tulikuwa tunaelewana," anasema.
"Lakini sikutumia neno rafiki, nilijifunza kuwa kutumia neno hilo ilimaanisha mengi kwa mtu kama mimi. Na watu wengi wanasema kuwa kama wewe ni rafiki…unaweza kuwa unafanya kosa kubwa ."
Ligon anakubali kwamba amekuwa mpweke wakati wote.
Alilelewana babu na bibi yake wazaa mama huko Birmingham, Alabama na hakuwa na marafiki wengi. Lakini anakumbuka nyakati nzuri akiwa na familia yake, kama vile siku za Jumapili walikuwa wakikutana pamoja wakimtazama babu yake mwingine akihubiri katika kanisa la kwao.
Alikuwa na umri wa miaka 13 alipohamia kusini mwa Philadelphia kuishi katika mazingira ya watu wa kipato cha kati na mama yake ambaye alikuwa muuguzi, baba yake ambaye alikuwa fundi wa magari, na wadogo zake wawili mmoja wa kiume na mwengine wa kike.
Alikuwa na matatizo shuleni na hakuweza kusoma wala kuandika. Hakucheza michezo na marafiki hawakuelewa mengi kuhusu maisha yake.
"Nilikuwa ni aina ya mtu ambaye alikuwa na rafiki mmoja au wawili, hao walikuwa wanatosha, sikuwa natafuta umati wa watu."
Wakati Ligon 'alipoingia matatizoni' Ijumaa moja usiku mwaka 1953, hakujua kwa hakika watu aliokuwa nao.
Alikimbilia katika kundi la watu aliowafahamu tu kawaida na walikuwa wanatembea tu mtaani, walikutana na watu wengine ambao walikuwa wanakunywa pombe.
"Tulianza kuwaomba watu pesa ili tuweze kupata mvinyo zaidi na tukaendelea hivyo mpaka mambo mengine yakatokea..."
Haina maana tena. Lakini ni ukweli uliokubalika kwamba usiku ule uliishia katika vitendo vya udungwaji wa visu wa watu na yeye alihusika. Wimbi hilo la ghasia liliwaua watu wawili na wengine sita kujeruhiwa.
Ligon alikuwa wa kwanza kukamatwa. Anasema kwamba hakuweza kuwaambia maafisa katika kituo cha polisi ni nani hasa aliyokuwa nao usiku ule.
"Hata wale wawili aliokuwa anawafahamu, hakuwajua majina yao rasmi, aliwafahamu kwa majina yao ya bandia."
Ligon anasema alipekekwa kwenye kituo cha polisi mbali na nyumbani kwao na kuzuiwa kwa siku tano bila kuwa na usaidizi wa kisheria.
Anasema alisikitishwa sana na muda mrefu ambao wazazi wake walizuiwa kumtembelea.
Wiki ile, akiwa na umri wa miaka 15 alishitakiwa kwa mauaji, shutuma ambayo amekuwa akiikana kila mara, ingawa amekubali katika mahojiano na mtangazaji wa runinga ya PBS kwamba aliwadunga visu watu wawili walionusurika na akaelezea kujutia kitendo hicho.
"Wao [polisi] walinipatia waraka wa kusaini ambao ulinihusisha katika mauaji. Sikumuua yeyote," anasema.
Pennsylvania ni moja majimbo sita ya Marekani ambako wafungwa waliofungwa maisha hawana uwezekano wowote wa kupewa msamaha.
Ligon alikabiliwa na kile kinachoitwa sheria ya kesi ya mtu mwenye makosa, ambapo alikubwali ukweli wa kesi yake na jaji alimpata na hatia ya makosa mawili ya mauaji.
Hakuwepo mahakamani kusikiliza hukumu yake, kwamba alitakiwa afungwe kifungo cha maisha bila uwezekano wa kupewa msamaha, jambo ambalo sio la kawaida kutolewa na pia bila rufaa.
Hii ilimamaanisha kuwa alikwenda jela bila kufahamu hukumu yake na haikutokea kwake kuwa na hamu ya kumuuliza mtu yeyote juu ya hukumu hiyo.
"Sikujua hata niulize nini. Najua ni vigumu kuamini, lakini huo ndio ukweli," anasema Ligon.
Miaka 53 baada ya hukumu yake, Ligon aliambiwa kuwa kuna wakili anataka kumuona.
Akitiwa moyo na uamuazi wa Mahakama ya juu zaidi ya Marekani ya mwaka 2005 kwamba watoto hawawezi kuuawa, Bradley S Bridge alianza kuchunguza kile alichokiamini kuwa kitakuwa ni tatizo kubwa la kisheria litakalojitokeza: Watoto ambao walipewa hukumu ya maisha gerezani bila msamaha.
Wakati huo, Pennsylvania ilikuwa na wafungwa 525 chini ya hali hizo, ambayo ilikuwa ni idadi ya juu zaidi katika nchi, kulingana na Bridge.
Philadelphia ilikuwa na 325, na Ligon alikuwa ndiye mfungwa mtoto aliyetumikia kifungo kwa muda mrefu zaidi. Wakili alikubali kukutana nae.
"Hakuwa anafahamu kusema kweli hukumu yake," anasema Bridge wa chama cha mawaliki wa watetezi wa Philadelphia - Philadelphia Defenders Association.
"Sikujua chochote kuihusu hukumu yangu hadi nilipokutana naye. Inashangaza kuwa hakuwahi kukosa tamaa ya kuwa na matumaini; alikuwa mwenye matumaini kabisa kwamba kitu fulani kitafanyika."
Kwa Ligon, kukutana kwake na wakili kulimfungua macho. Wakati Bridge alipomuonesha nakala ya rufaa iliyokosoa kisheria hukumu dhidi yake, ilikuwa mara ya kwanza Ligon kufahamu ni kwanini alifungwa.
"Nilibaini kuwa kesi yangu ilishugulikiwa vibaya tangu wakati alipokamatwa. Nilifundishwa na kujifunza kwamba ilikuwa ni kinyume cha katiba kufungwa (kama mtoto) bila uwezekano wa kusamehewa."
Ingawa kwa Ligon alikuwa na tumaini kuwa wakati mmoja atatoka gerezani, kwa miaka 15 alifanya maamuzi ambayo baadhi wanaona ni magumu kuyaelewa: alikataa fursa za kuachiliwa kwasababu alihisi zilikuja na kile alichokiita " kivuli cha maisha. "
"Bodi ya msamaha ilinitembelea mara mbili. Kukubali msamaha ingekuwa ni njia ya haraka ya kutoka nje ya gereza miaka iliyopita ," anasema.
"[Lakini kama ningekubali kusamehewa ningekuwa katika kipindi cha kiuchunguzwa kwa maisha yangu yote yaliyobakia na kesi yangu haikuhitaji kipindi cha kuchunguzwa . kama kesi yangui ingehitaji msamaha huo, isingekuwa na tatizo. Lakini hiyo ndio sababu nilikataa."
Mwaka 2016 Mahakama ya juu zaidi iliamua kuwa wafungwa wote watoto waliohukumiwa kifungo cha maisha wanapaswa kupewa hukumu mpya.
Mwaka uliofuatia Ligon alihukumiwa tena kifungo cha miaka 35, hii ikimaanisha kuwa angeweza kutuma maombi ya kusamehewa kutokana na muda ambao tayari alikuwa ametumikia kifungo.
Mimi maneno yangu yalikuwa: ''Ninataka kuwa huru''.
Ilimbidi Bridge kufungua kesi dhidi ya kifungo chake mwaka 2017 na hatimaye alipeleka kesi katika mahakama ya rufaa ambapo Novemba 2020 Jaji aliamua afunguliwe.
Wakati Bridge alipokwenda katika kaunti ya Montgomery kumchukua Ligon tarehe 11 Februari, alimpata mfungwa huyo akiwa mtulivu.
"Nilitarajia kumsikia akisema kwa ukakamavu sana 'oh mungu wangu' aliponiona. Lakini hakuonesha uchangamfu wowote. Hapakuwa na shamra shamra, haikuwepo.
"Labda kwasababu Ligon alikuwa akifanya kile alichokuwa akikifanya kwa miongo yote gerezani. Kuwaza maisha yake binafsi," anaeleza wakili wake.
Mwezi mmoja baada ya kuachiliwa, anatafakari kwa kiwango cha kushangaa siku aliyoondoka katika gerea la jimbo la Phoenix.
"Ilikuwa ni kama kuzaliwa tena. Kwasababu kila kitu kilikuwa ni kipyta kwangu, karibu kila kitu kilikuwa kimebadilika, mambo bado ni mapya kwangu."
"Ninaangalia baadhi ya haya magari mapya, magari haya hayana miundo kama niliyoiacha wakati nilipokuwa mitaani miaka mingi iliyopita. Ninaangalia majengo haya yote marefu…hapakuwa na majengo marefu kama haya yanayonizingira sasa ."
"Haya yote ni mapya," alisema, huku akionesha kila kitu kwa mkono ndani ya chumba chake..
"Na ninayazowea. Ninayapenda. Inanifurahisha, hii ni kweli kabisa ."
Miaka 68 iliyopita imekuja na gharama kwa Ligon.
Anafahamu fika kwamba amepoteza muda wa kusubiri bila msamaha, muda ambao angekuwa amekaa na familia yake, ambao wengi wao tayari walikufa.
"Mpwa wangu Valerie alizaliwa wakati nilipokuwa gerezani, dada yake mkubwa alizaliwa nilipokuwa gerezani, dada yake mdogo alizaliwa nilipokuwa gerezani," anakumbuka.
"Watu wa familia yangu ya karibu wamefariki, aliyebaki ni Valerie, mama yake Valerie na mimi."
Na ingawa mwanaume huyu mwenye umri wa miaka 83 anajaribu kuzoea maisha ambayo aliyatamani kwa muda mrefu, ana mipango michache.
Inaonekana kwamba atazingatia tu kile anachokifahamu zaidi.
"Nitafanya mambo sawa na ambayo nimekuwa nikiyafanya katika maisha yangu yote. Kupata kazi ya kufanya usafi katika majengo."