Biden na Putin:Kinachotarajiwa kuzungumzwa katika mkutano wa marais wa mataifa mawili hasimu yenye nguvu kubwa za kijeshi

Chanzo cha picha, Reuters
Joe Biden alisema mwezi uliopita kwamba atakutana ana kwa ana na rais wa Urusi Vladimir Putin kwa wakati fulani hivi karibuni. Sasa tunaijua tarehe na ni wapi watakapokutana.
Mkutano wa kwanza wa Marekani na Urusi chini ya Rais wa sasa wa Marekani Biden utafanyika mjini Geneva, nchini Uswizi tarehe 16 Juni.
Mkutano huo utafanyika mwisho, baada ya ziara ambayo tayari Bw Biden amezipanga za Uingereza kwa ajili ya kikao cha G7 na ile ya Brussels kwa ajili ya mkutano na viongozi wa Muungano wa Nato, ili kuwa na muda wa kutosha wa kuwasikiliza washirika wa Marekani kabla ya kuketi chini na Putin.
Katika taarifa ya katibu wa habari wa Ikulu ya White House Jen Psaki, iliyotangaza mkutano huo wa Biden na Putin, alisema mkutano huo utaangazia "Masuala yote kamili yanayohitaji kushughulikiwa haraka " huku Marekani ikitaka "kurejesha hali ya kutabiriwa na utulivu" katika mahusiano yake na Urusi.
Hayo yanafanana na kauli alizozitoa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken wakati wa mkutano na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, huko Iceland wiki iliyopita, aliposema kuwa lengo la Biden ni kuwa na " Uhusiano wa kutabirika, na imara na Urusi".
Mada kamili zilizopangwa - na wasi wasi
Wakati Biden na Putin watakapokutana, watakuwa na mengi ya kuzungumzia.
Orodha fupi ya mada hizo ni pamoja na udhibiti wa silaha, mabadiliko ya hali ya hewa, uhusika wa jeshi la Urusi nchini Ukraine, shughuli za udukuzi wa kimtandao za Urusi, ikiwa ni pamoja na shambulio la mwaka 2020 linalofahamika kama SolarWinds dhidi ya serikali ya Marekani na mitandao binafsi ya kompyuta, na jaribio la kumuua kwa sumu na kumfunga mpinzani wa Putin Alexei Navalny.
Mazungumzo hayo yanaonekana kuishia kuwa na hatma ambayo haitapendwa, kwani Biden na Putin wamekuwa wakibadilishana maneno makali huku hali ya wasi wasi ikiongezeka katika miezi iliyopita.
Katika mahojiano mwezi Machi, Bw Biden alikubali moja ya maswali kwa kumuelezea Putin kama "muuaji", jambo lililoichochea Urusi kumuita nyumbani kwa muda balozi wake nchini Marekani na Putin kujibu akisema inahitaji mtu mmoja kumfahamu mwingine, kabla ya kumtakia Biden "afya njema" kwa shingo upande.
Kuna matarajio machache ya upatikanaji wa matokeo yanayoonekana kutokana na mkutano huu, kando na matumaini kuwa utawezesha kuboreka kwauhusiano na uelewano baina ya viongozi hao wawili.
Vikwazo viliwekwa na vikaondolewa
Adhabu mpya za utawala wa Biden dhidi ya Urusi zinachangia kuwepo kwa hali ya mvutano baina ya Urusi na Marekani. Mwezi uliopita Biden aliiadhibu Urusi kwa udukuzi wa kimtandao wa Solar Winds, adhabu hizo zikiwa ni pamoja na ukomo mpya wa usafirishaji wa pesa baina ya taasisi za kifedha za Marekani na serikali ya Urusi pamoja na vikwazo dhidi ya wafanyabiashara wa Urusi na kuwafukuza baadhi ya wanadiplomasia wa Urusi chini Marekani.
Kama vikwazo hivyo vilikuwa "fimbo " ya kidiplomasia, tangazo la wiki iliyopita kwamba utawala wa Biden utaondoa vikwazo vilivyowekwa na congress dhidi ya mtango wa gesi unaokaribia kukamilika kati ya Urusi na Ujerumaniinaweza kupunguza uhasama uliopo baina ya Marekani na Urusi kabla ya kikao cha mwezi Juni.
(Pia inaepuka kuiudhi Ujerumani, ambayo inaweza kuwa na umuhimu sawa kwa utawala wa Biden, ambao unalenga kuondoa dosari katika uhusiano kati ya Marekani na Muungano wa Ulaya.)
Suala la Trump
Kama kutabiriwa na utulivu ni sehemu ya lengo la Biden, litakuwa ni kinyume sana na miaka minne ya utawala wa rais Trump , ambao ulianza kwa madai-yaliyothibitishwa na majasusi wa Marekani -kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 na iilihusika na mashambulio ya kimtandao dhidi ya chama Democrat na mgombea wake Hillary Clinton.
Mashambulio hayo yalitawala sehemu kubwa ya urais wa Trump, na kufanya baraza maalum la uchunguzi la Robert Mueller kufichua mawasiliano baina ya wajumbe wa kampeni ya Trump na raia wa Urusi( ingawa uchunguzi ulibaini kuwa hapakuwa na ushahidi wa uratibu baina ya kambi mbili).
Wakati Trump na Putin walipokuwa na kikao chao cha kwanza na pekee cha ana kwa ana mjini Helsinki, Finland, Julai 2018, katika jambo lililoibua utata Trump alisema kuwa anaamini kusisitiza kwa Putin kwamba Urusi haikuhusika katika udukuzi wa uchaguzi, licha ya kwamba ujasusi wa Marekani ulibainii kinyume.
Katika kampeni zake za uchaguzi na katika kipindi chote akiwa madarakani, Trump alionesha kumpongeza na kumpa sikio la huruma Putin, ingawa utawala wake -japo kwa kuchelewa ulifuata na kuvitekelezavikwazo vilivyoamrishwa na congress dhidi ya Urusi.












