Israeli yafanya mashambulio mapya Gaza licha ya maombi ya kusitisha mapambano

A Palestinian firefighter participates in efforts to put out a fire at a sponge factory on Monday

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Vikosi vya zimamoto katika harakati za kuzima moto uliotokana na mashambulizi ya ndege ya alfajiri ya leo.

Israeli imefanya mashambulizi kadhaa alfajiri ya leo katika Ukanda wa Gaza, baada ya wanamgambo wa Palestina kurusha makombora ya roketi katika miji iliyopo kusini mwa Israeli.

Mashambulizi ya alfajiri ya Jumatatu ni makubwa zaidi tangu mapambano yaanze wiki moja iliyopita.

Israeli inasema imeshambulia majengo yanayomilikiwa na wanamgambo wa Hamas pamoja na nyumba kadhaa za makamanda wa kundi hilo, hata hivyo barabara kuu kadhaa na nyaya za umeme pia zimeharibiwa.

Mashambulio hayo yanatokea wakati jumuiya ya kimataifa ikitaka pande zote mbili katika mgogoro huo kusitisha mashambulizi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) lilifanya mkutano wa dharura jana Jumapili na Katibu Mkuu wa UN António Guterres ameonya kuwa mapambano zaidi "yanaweza kusababisha hali mbaya ya kiusalama na kibinaadamu."

Guterres pia ametaka mapambano hayo "mabaya" yasitishe haraka iwezekanavyo.

Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi ameeleza leo Jumatatu kuwa nchi yake "imepiga hatua kubwa katika kutafuta kusitishwa kwa mapambano...na matumaini bado yapo."

Lakini mpaka sasa hakuna dalili za hilo kutokea huku mapambano makali yakiingia wiki ya pili.

Ghasia hizo ni zao la wiki za hamaki na wasiwasi baina ya Israeli na Palestina katika eneo la Jerusalemu Mashariki ambapo hali hiyo iliishia katika mapambano katika eneo takatifu kwa Waislamu na Wayahudi.

Kundi la Hamas, ambalo linaongoza Ukanda wa Gaza, likaanza kurusha makombora ya roketi baada ya kuionya Israeli iondoke katika eneo hilo la Jerusalemu, na hapo ndipo Israeli ilipoanza kufanya mashambulizi ya anga ya kulipiza.

A Palestinian firefighter reacts as he participates in efforts to put out a fire at a sponge factory

Chanzo cha picha, Reuters

Jeshi la Israeli linasema zaidi ya ndege 50 za kivita zimefanya mashambulizi ya dakika 20 muda mfupi kabla ya alfajiri ya leo.

Ndege vita hizo zimepiga na kuteketeza "maeneo ya kigaidi" 35 na kuharibu zaidi ya kilomita 15 za mfumo wa mahandaki yanayomilikiwa na Hamas, linadai jeshi la Israeli.

Jeshi hilo pia linadai kuwa limezipiga nyumba tisa za makamanda "wa ngazi ya juu" wa Hamas.

Map showing Israel and the Gaza Strip
Presentational white space

Hata hivyo hakujakuwa na idadi rasmi kufikia sasa ya watu waliofariki na kueruhiwa, lakini mamlaka za Palestina katika Ukanda wa Gaza zinasema kuwa mashambulizi hayo yamesababisha umeme kukatika katika maeneo mengi na kuharibu mamia ya nyumbana majengo mengine.

"Hakujawahi kuwa na mashambulizi ya ukubwa huu," mkaazi mmoja wa Gaza ameliambia shirika la habari la kimataifa la AFP . Mad Abed Rabbo, 39, amesema alihisi "woga mkubwa na kutishika" wakati mashambulio hayo yakiendelea.

"Nilikuwa najiandaa kufariki dunia. Ilibidi nikubaliane na hali hiyo," Najla Shawa, mtoa misaada ya kibinaadamu na mama wa watoto wawili ameiambia BBC.

Mkaazi mwengine wa Gaza, Sarah Mahmoud, ameiambia BBC: "Bado tungali hai, lakini hatupo salama. Ndege zimeharibu barabara nzuri zaidi ya Gaza."

Kuufikia sasa idadi ya waliofariki katika Ukanda wa Gaza imefikia 200, ikiwemo watoto 59 na wanawake 35 huku waliojeruhiwa ni 1,305, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Hamas. Israeli inasema wapiganaji 130 wa Hamas ni miongoni mwa waliouawa.