Jinsi watu wa jamii ya Igbo wanavyotumia mfumo wa kibiashara kuwa mabilionea Nigeria

Onyeka Orie anasema hakutarajia kupewa duka
Maelezo ya picha, Onyeka Orie anasema hakutarajia kupewa duka

Jamii ya Igbo nchni Nigeria ina sifa ya kufanikiwa kibiashara - kutokana na mfumo mmoja wa jamii hiyo uliobuniwa baada ya vita , kulingana na mwandishi wa BBC Chiagozie Nwonwu mjini Lagos.

Onyeka Orie anayetabasamu , 28 anatazama picha ya furaha katika duka lake la kuuza simu za rununu katika mji wa Lagos.

Duka hilo na kila kitu kilichopo ndani yake alipatiwa na mwajiri wake baada ya bwana Orie kumfanyia kazi bila malipo kwa miaka kadhaa ili kujifunza biashara.

''Nilimuhudumia mwajiri wangu kwa takriban miaka minane. Mwajiri wangu alinipatia duka hili. Sikutarajia'' , alisema bwana Orie mwenyewe furaha.

Akiwa ni kijana aliyezaliwa na wazazi wakulima kusini mashariki mwa Nigeria, alisema kwamba alikuwa na nafasi ndogo kujinasua kutokana na umasikini kwasababu familia yake haikuweza kumpatia elimu aliyohitaji ili kuweza kupata kazi nzuri katika taifa ambalo ukosefu wa ajira ni mwingi hata miongoni mwa wale walio na shahada kutoka chuo kikuu.

Hivyobasi baada ya shule ya upili alijiunga pamoja na vijana wengine wa jamii ya Igbo ili kujifunza biashara chini ya mfumo huo wa biashara kwa jina 'Igba Boi', mpango ambao vijana wadogo , huondoka katika familia zao kwa lengo la kwenda kuishi na wafanyiabiashara matajiri waliofanikiwa.

Wavulana hao wanatarajiwa kuwahudumia waajiri wao, wakiwafanyia kila kitu , ikiwemo kuosha magari na kumfanyia kazi zake za nyumbani.

Badala yake wavulana hao hupata maisha mazuri na hufunzwa jinsi ya kusimamia biashara. Pia hupewa chakula na eneo la kuishi.

Kijiji cha kisasa cha Lagos

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kijiji cha kisasa cha Lagos

Mwisho wa muda walioafikiana , mwajiri wao huwapatia mtaji kuanzisha biashara zao wenyewe.

Mfumo wa biashara wa Igbo una mizizi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, kulingana na profesa mmoja ambaye chapishi lake kuhusu mfumo huo wa biashara linatarajiwa kuwasilishwa katika chuo cha Havard cha biashara baadaye mwizi huu.

Watu wa jamii ya Igbo , wakitoka katika vita walivyoshindwa kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 1967-70, walifanikiwa kujirudishia kile walichopoteza wakati wa vita hivyo baada ya miaka miwili.

Hii ni licha ya serikali ya Nigeria kuwapokonya akaunti zao za benki.

Baadaye walipatiwa £20 ($28) ili kuanza upya , huku wengine wakiona mali yao ikichukuliwa na majirani zao katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Klabu ya raia , klabu maarufu iliobuniwa katika mji wa Aba 1971, pia ina sifa ya kuanzisha mfumo huo wa Igbo.

Waanzilishi wa klabu hiyo wenye filisofia ya Igbo kwa jina 'usimwache ndugu yako nyuma' inaonekana kama muongozo wa mfumo huo.

Klabu hiyo ni vuguvugu la kiuchumi lenye maelezo kuhusu jinsi watu wa jamii ya Igbo wanaweza kujinasua kutoka katika athari za vita hivyo na kuanza mbinu nyengine ya kuishi, kulingana na Benedict Okoro, mwanzilishi wa utamaduni wa Odinala.

Wafanyabiashara katika soko la Aba

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wafanyabiashara katika soko la Aba

Mfumo huo wa biashara unawalenga wavulana na vijana kwa kuwa familia haziko tayari kuwaachilia wasichana wao kuishi na wafanyabishara kwa miaka mitano inayowachukua kujifunza biashara.

Badala yake wanawake hujifunza katika biashara zilizopiga hatua , ambapo hulipa ili kufunzwa kwa muda wa miezi sita hadi mwaka . Huku wakiendelea kuishi nyumbani.

'Sikupata kitu baada ya miaka saba'

Mfanyabiashara maarufu nchini Nigeria kama vile Tajiri innocent Chukwuma anayemiliki Innoson Motors na Cosmas Maduka wa kundi la kampuni za Coscharis ni miongoni mwa watu waliokuzwa na mfumo huo.

Katika mahojiano ya 2019 yaliofanywa na BBC Igbo, bwana Maduka alisema kwamba Naira 200 au dola 0.70 anazopewa na mwajiri wake mwisho wa mafunzo yake 1976, ziliweka msingi wa biashara yake ya mamilioni ya fedha.

Cosmas Maduka
Maelezo ya picha, Cosmas Maduka ni mmoja ya waliokuzwa na mfumo huu

Ufanisi wa mfumo huo unaonekana mashariki mwa miji kama vile Onitsha, Aba na Nnewi ambapo masoko yaliochipuka yanawavutia wafanyabiashara kutoka magharibi mwa Afrika.

Lakini mfumo huo pia haujakosa kukosolewa , kwa kuwa unategemea mwajiri kumuangalia mfanyakazi wake mwisho wa mafunzo hayo.

Ndubuisi Ilo, ambaye sasa anamiliki duka la vipuri katika eneo la Ladipo anasema kwamba hakupewa chochote baada ya kumhudumia mwajiri wake kwa miaka saba..

''Mwajiri wangu aliniita siku moja na kuaniambia kwamba hawezi kumudu kunilipa. Aliniombea na kuniambia nianze Maisha ya kutafuta kivyangu''.

'' Ilikuwa vigumu mara ya kwanza na nikalazimika kulala ndani ya gari , lakini sasa naangalia nyuma na kutabasamu'', anasema.

Map: Nigeria

Hatahivyo hatazami mafunzo aliyopata kama kupoteza muda, kwa kuwa alitumia mafunzo aliopata kuanzisha biashara.

Baahi ya wafanyabiashara hawataki kutimiza makubaliano kutokana na kiwango cha fedha kinachohusika kuanzisha biashara kwa mfanyakazi ambaye amekamilisha muda wake.

''Baadhi yao humshutumu mfanyakazi huyo kwa wizi ama kitu kingine na kukatiza makubaliano'', bwana Ilo anasema.

Makubaiano ya Igba Boi ni ya maneno na wakati mwajiri anaposhindwa kutimiza , wafanyakazi huwa hawana mbadala wa kuomba usaidizi wa kisheria..

Kuna udugu katika jamii ya Igbo na baadhi ya tofauti husuluhishwa katika mikutano ya vijiji

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kuna udugu katika jamii ya Igbo na baadhi ya tofauti husuluhishwa katika mikutano ya vijiji

Na kwasababu waajiri wengi huwa watu unaousiana nao , familia kawaida hujaribu kutatua mzozo wowote na wanaposhindwa , wakaazi wa vijiji vya pande zote mbili huingilia kati na kujaribu kutatua tatizo hilo.

Mara nyingine matatizo hutatuliwa vizuri, na mara nyingine haiwezekani , na hivyobasi kumuacha kijakazi kujitafutia baada ya miaka kadhaa ya kufanyakazi bila malipo.

'Mfano wa Bwana Okoro anatafuta njia ya kuurasimisha mfumo wa Igba ili kupunguza hatari ya kutotimiza makubaliano.

''Mfumo uliofanywa kuwa rasmi utaungwa mkono na sheria na hautakuwa tu makubaliano kati ya wafanyabiashara, mfanyakazi na familia yake'', alisema. Mfanyakazi pia atapata cheti cha mafunzi ya biashara hiyo.

line

'Bora zaidi ya shahada ya chuo kikuu'

Data ya ajira nchini Nigeria inaonesha kuwa asilimia 33 ya wale wanaotafuta kazi hawawezi kupata.

Wengi wao ni mahafala wa chuo kikuu. Bwana Orie anasema kwamba hali yake ya kifedha ni bora zaidi ya wenzake waliokwenda chuo kikuu.

Pia alianza kufikiria kupata kijana mdogo kutoka kijijini ili kumfunza biashara kitu ambacho kipo katikati ya mfumo huo.