Shambulio la al Qaeda Kenya 1998: Wakenya waathiriwa wakasirishwa na hatua ya Marekani kutowafidia

Diana Mutisya ameungua majeraha ya maisha tangu shambulio hilo
Maelezo ya picha, Diana Mutisya ameungua majeraha ya maisha tangu shambulio hilo

Mtumishi mmoja wa serikali nchini Kenya Diana Mutisya amekatishwa tamaa baada ya kubaini kuwa hatapokea fidia kama itakavyokuwa kwa raia wa Marekani waliojeruhiwa wakati wanamgambo wa al-Qaeda walipolipua kwa bomu ubalozi wa Marekani mjini Nairobi miaka 22 iliyopita.

Alikuwa benki iliyokuwa karibu na ubalozi huo nchini Kenya mlipuko huo ulipotokea.

Watu wengine wanne aliokuwa nao kwenye chumba kimoja kipindi kile walifariki dunia. Yeye alipoteza fahamu kabisa na kusafirishwa hadi nchini Afrika Kusini kwa matibabu ambako vyuma 15 vilitumika kushikilia tena uti wake wa mgongo.

Mwezi uliopita, ilitangazwa kuwa Sudan imelipa dola milioni 335 kama fidia kwa waathirika wa mashambulizi hayo yaliyotekelezwa dhidi ya maeneo ya Marekani yaliyokuwa yamelengwa.

Lakini sharti la msingi lililowekwa na Marekani dhidi ya Sudan kuondolewa kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi - ni kulipa fidia kwa familia za waathirika au wale waliojeruhiwa ambao ni raia wa Marekani ama wafanya kazi wa ubalozini.

Watu karibu 5,000 waliokadiriwa kujeruhiwa na mashambulizi mawili ya mabomu kwenye balozi za Marekani jijini Nairobi na Tanzania jijini Dar es Salaam yaliyotokea Agosti 7 mwaka 1998 hawatapata chochote.

Na pia hakuna familia yoyote ambazo ni zaidi ya 200 za wenyeji waliofariki dunia katika mlipuko huo itakayopokea fidia.

"Nilisikia vibaya [nilipopata taarifa hizo]… Tuliathirika kwasababu ya uhasama kati ya Marekani na washambuliaji. Wanafaa kutuorodhesha katika orodha ya wanaolipwa fidia," Bi. Mutisya amezungumza na BBC.

"Wamarekani sio kuwa wao ndio wenye nguvu, sote ni binadamu... Na zaidi ni kwamba sisi hatuna hatia yoyote, mlipuko huu ulitokea kwasababu yao. Washambuliaji walikuwa wanalenga ubalozi wakijua kuwa raia wa Marekani wanafanya kazi huko."

Imemchukua miaka mingi mfanyakazi huyo wa serikali kusahau kilichotokea siku ile na kuendelea na maisha yake - lakini ukweli ni kwamba kilichomtokea hawezi kukisahau kabisa.

Moja ya mapafu yake hayafanyi tena kazi. Leo hii anaweza kutembea lakini si kwa muda mrefu na pia anatumia kiti cha magurudumu kwenda kazini.

"Ninatumia zaidi ya shilingi 80,000 za Kenya sawa na ($750; £545) kila mwezi kwa matibabu ya viungo vya mwili pekee," amesema - kiasi hicho kikiwa ni kiwango kikubwa tu cha mshahara wake.

Kila mwathirika wa Marekani au familia za waliokuwepo wakati shambulizi hilo linatokea atapokea dola milioni 3, huku wafanyakazi wa maeneo wakipokea dola 400,000, vyombo vya habari vya Marekani vimesema. Kwa ujumla, manusura 85 au familia za waathirika zitafidiwa.

'Pesa hazikufikia waathirika'

Lakini kwa wengi hakuna ukurasa mpya watakaofungua licha ya Marekani kusema imetoa mamilioni ya madola kama usaidizi wa kibinadamu kwa waathirika wa Kenya wa shambulizi hilo la bomu.

"Nilihusika katika mchakato wa kushinikiza bunge la Marekani kuidhinisha dola milioni 47 kwa raia wa Kenya," Douglas Sidialo, ambaye alipoteza uwezo wake wa kuona baada ya kutokea kwa mlipuko huo amezungumza na BBC.

Msemaji wa chama cha waathirika nchini Kenya katika suala la usaidizi wa Marekani kwa waliojeruhiwa kwenye mlipuko wa bomu mwaka 1998 amesema:

"Tulidhania kuwa pesa hizi zinakuja kusaidia waathirika lakini naweza kukuambia kwamba asilimia 95 ya pesa hizi zilielekezwa kwenye uboreshaji wa majengo yanayozunguka ubalozi.

"Hazikuwahi kuwafikia kwa ajili ya kuboresha maisha."

Akiwa kama makamu wa rais, Joe Biden alitembelea Kenya mwaka 2010 na akakutana na baadhi ya waathirika wa shambulizi hilo la bomu mjini Nairobi na suala la fidia likaibuka.

Joe Biden na mkewe walitembelea eneo la shambulio hilo na kukutana na waathiriwa 2010

Chanzo cha picha, IMAGE COPYRIGHTGETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Joe Biden na mkewe walitembelea eneo la shambulio hilo na kukutana na waathiriwa 2010

image captionJoe Biden and his wife visited the site of the Nairobi bombing in 2010 and met survivors

"Nilimshika mkono wake kwa dakika moja. Nikazungumzia masuala haya na Joe Biden. Akajibu kuwa watalifuatilia. Imetuchukua zaidi ya miaka 10 sasa, na hatujawahi kusikia chochote kutoka kwake," Bwana Sidialo alisema.

"We want equal treatment just like Americans. We are not lesser beings."

"Tunataka tuchukuliwe sawa na Marekani. Haimaanishi kuwa thamani yetu ni kidogo kuliko binadamu wengine."

Shambulio la kigaidi lililotekelezwa Kenya na Tanzania

shambulio la kigaidi lililotekelezwa Kenya na Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, shambulio la kigaidi lililotekelezwa Kenya na Tanzania

•Balozi za Marekani Afrika Mashariki zililengwa Agosti 9 1998 kupitia mashambulizi ya mabomu ya kujitoa muhanga

•Shambulizi la kwanza lilitokea Tanzania mjini Dar es Salaam karibu saa 10:30 saa za eneo na mlipuko wa pili ukatokea dakika chache baadaye mjini Nairobi, Kenya

•Mjini Nairobi, ofisi kubwa karibu na jengo la ubalozi liliharibiwa na timu ya uokozi kutoka Israel ikawasili siku mbili baadaye na miili ya waliofariki dunia ikatolewa.

•Watu 224 waliuawa katika mashambulizi hayo ya mabomu ikiwemo Wamarekani 12 huku zaidi ya 5,000 wakijeruhiwa - mamia ya hao wakapoteza uwezo wao wa kuona baada ya kukuingiwa na vigae vilivyokuwa vinaruka

•Karibu maafisa 900 wa kijasusi waliwasili maeneo ya tukio kufanya uchunguzi na kubaini kwamba kundi la al-Qaeda ndio lilikuwa limehusika

•Zaidi ya watu 20 walishitakiwa kuhusiana na mashambulizi hayo. Baadhi wakihukumiwa kifungo cha maisha nchini Marekani; wengine ambao wahakuzuiliwa waliuawa kama vile kiongozi wa kundi la al-Qaeda Osama Bin Laden

Lakini manusura ambao wanapitia changamoto si haba wanachokilia ni haki itendeke.

Wameshirikiana na Kituo Cha Sheria - shirika lisilo la kifaida linalosaidia watu kesi zao mahakamani kwa maslahi ya umma.

Shirika hilo linadhamiria kupinga uamuzi wa Marekani katika mahakama ya juu na pia mazungumzo yanaendelea kufungua kesi katika mahakama ya Marekani.

Kwa Mutisya, ni muhimu kuendelea kupigania haki yao kabla ya manusura zaidi kuendelea kufariki dunia.

"Tukio hilo ni kama tu limetokea jana kwasababu tunaishi na machungu mengi mno.

"Tunauguza vidonda vingi na hivyo basi hatuwezi kutimiza uwezo wetu. Lakini bado tutaendelea kupigania haki hata kama tutasalia wachache tu."