Rais Samia: Nini kilikosekana katika hotuba ya jana?

Samia Bungeni

Chanzo cha picha, IKULU, TANZANIA

Maelezo ya picha, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

Nilitazama hotuba ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan nikiwa nyumbani na mke wangu na wakati niliposema kitu kimoja ambacho sikuvutiwa nacho kuhusu hotuba ile - mke wangu alinijibu kwa sentensi moja tu: "huo ndiyo wivu wenu ninyi wanaume".

Kuondoa maudhui mengine yote katika hotuba ya Rais Samia bungeni jijini Dodoma jana - jambo kubwa kuliko yote katika tukio hilo lilikuwa kwamba historia mpya ilikuwa inaandikwa kwa wanawake wengi nchini Tanzania - wakishuhudia kwa mara ya kwanza mwenzao akihutubia Bunge kama Mkuu wa Nchi: kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo.

Wakati hotuba ya kwanza ya Rais Jakaya Kikwete bungeni mwaka 2005 itakumbukwa kwa kauli yake kuhusu tabasamu lake huku ya hayati Rais John Magufuli ikikumbukwa kwa ahadi yake ya kutumbua majipu - ya Samia inaweza isikumbukwe kwa chochote alichozungumza bali kwa ukweli kwamba hatua kubwa katika kuvunja vikwazo dhidi ya wanawake nchini ilikuwa imepigwa.

Hotuba ya Rais Samia ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na wengi kujua nini utakuwa mwelekeo wake katika kipindi cha miaka yake minne ya urais wake kuanzia sasa hadi mwaka 2025. Tofauti na watangulizi wake wote ambao waliingia madarakani kwa kupigiwa kura, Samia amepata nafasi hiyo kufuatia kifo cha Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu.

Rais Samia na Spika Ndugai

Chanzo cha picha, IKULU

Wengi walitaka kujua kama ataendeleza nyayo za mtangulizi wake ambaye walifanya naye kazi kwa karibu katika Awamu ya Tano au atafuata mwelekeo wake binafsi. Hotuba yake ya jana imetoa picha ya nini hasa Watanzania na dunia kwa ujumla itarajie kutoka kwake.

Mwendelezo wa utawala wa Awamu ya Tano

Katika hotuba yake ya jana iliyochukua takribani dakika 90, Rais Samia aliweka wazi kwamba ataendeleza karibu mipango yote iliyokuwa imepangwa kutekelezwa na mtangulizi wake huyo na kwamba hakuna kitakachobadilika.

Kwa aliyeisikiliza hotuba ile tangu mwanzo, hatapata shida kubaini kwamba kulikuwa na 'mkono' usioonekana katika sentensi, matamshi na msisitizo wa chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM); karibu katika maeneo yote ya kimsingi kwenye hotuba hiyo.

Kwa mara nyingine, Rais Samia aliwaambia Watanzania kwamba yeye na Magufuli ni kitu kimoja; sentesi ambayo ni tata kwa sababu inawapa raha watu wanaoamini katika iliyokuwa staili ya uongozi ya Rais Magufuli lakini inawakera wale wanaoamini kwamba mtangulizi huyo wa Samia si mtu wa kufuatwa au kutamani kufananishwa naye katika masuala ya uongozi.

Hotuba hiyo ya Samia pia iliweka wazi kwamba ataendeleza miradi yote mikubwa ya miundombinu iliyoachwa na mtangulizi wake na kuahidi kulilea Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) - jambo lingine linalohusishwa moja kwa moja na utawala wa mtangulizi wake.

John Magufuli (R) and his deputy Samia Suluhu Hassan in 2019

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Samia Suluhu Hassan alihudumu kama makamu wa Rais Magufuli tangu mwaka 2015

Rais Samia aliahidi pia kuendeleza utaratibu wa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule ya msingi lakini akatangaza pia kwamba suala lililo moyoni mwake ni kupambana na vifo vya akinamama wajawazito wakati wa kujifungua. Hili ni jambo aliloanza kulishughulikia tangu akiwa Makamu wa Rais kupitia kampeni yake maalumu ya Jiongeze.

Nini atakifanya tofauti na mtangulizi wake

Hotuba ya Rais Samia pia iliweka bayana kwamba kuna mambo ambayo atayafanya tofauti na mtangulizi wake. Kwa mfano, ingawa alisema serikali itaendelea kulilea Shirika la Ndege, lakini kuna uwezekano wa kulifumua kwa kuweka watendaji wenye weledi na watakaoweza kulifanya lijiendeshe kwa faida.

Eneo ambalo alionyesha atakwenda tofauti kabisa na Magufuli lilikuwa ni kwenye namna ya kujikinga na ugonjwa wa Corona, ambapo alisema ameunda timu itakayoishauri serikali hatua za kuchukua kwenye kujikinga na ugonjwa huo uliopoteza maisha ya mamilioni ya watu duniani kote.

Kama Samia angebadili staili ya kupambana na ugonjwa huo kwa ghafla na haraka, angeweza kuonekana ametofautiana na Magufuli mapema - jambo ambalo huenda lingewaumiza wafuasi wa mtangulizi wake huyo, lakini hakuna ambaye atamwona vibaya au kumchukia kwa sababu ya kufuata ushauri wa kitaalamu.

Rais Samia alitangaza pia dhamira yake ya kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani kwa ajili ya kujadili mustakabali wa taifa kisiasa katika nyakati hizi.

Hayati Magufuli alikuwa akikutana na viongozi wa vyama vya upinzani katika matukio ya kijamii na katika masuala mahususi lakini hakuwahi kutangaza kwamba atakutana nao kwa ajili ya kujadili masuala ya uongozi wa nchi.

Kwa mara nyingine, Samia ameonyesha kwamba ataboresha mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania kwa kuondoa vikwazo vya kuingia mitaji kutoka nje na kufufua mazungumzo kuhusu mradi wa kuchakata gesi (LNG) uliopangwa kufanyika mkoani Lindi.

Rais Samia

Chanzo cha picha, IKULU

Ingawa hakuingia kwa undani, Samia alizungumza kuhusu suala la miradi ya uwekezaji katika maeneo maalumu ya kiuchumi - akionyesha uwezekano wa kurejea tena kwa mazungumzo kuhusu mradi wa Bandari ya Bagamoyo ambao sehemu yake kubwa ni ujenzi wa maeneo hayo ya uwekezaji.

Nini kilikosekana katika hotuba ya Rais jana?

Tangu ameingia madarakani, Rais Samia amekuwa na utaratibu wa kutotabirika nini atakifanya wakati akihutubia. Katika siku ambayo watu wengi walidhani ataitumia kuapisha viongozi, Samia alitangaza mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri.

Katika tukio la sala maalumu iliyoandaliwa na viongozi wa dini kwa ajili ya kumpongeza na kumtakia heri katika uongozi wake mjini Dodoma, Rais Samia alitumia nafasi hiyo kuwakosoa wabunge waliokuwa wakilumbana bungeni kuhusu urathi (legacy) wa utawala wa Magufuli.

Wengi walitaraji kwamba angeweza kutumia hotuba yake ya jana kuonyesha tofauti yake ya wazi na ya kwanza kubwa dhidi ya utawala uliopita. Ilitarajiwa angeweza kutoa msamaha kwa baadhi ya wafungwa, kukaribisha wanasiasa na wananchi wengine waliokimbia nchi kurejea, kufungulia vyombo vya habari vyote vilivyofungiwa na pengine kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya kisiasa.

Rais Samia hakutoa kauli yoyote kwenye mwelekeo huo, lakini - kama ambavyo ameanza kuonyesha wakati wa urais wake, alitumia fursa hiyo kutoa kauli kali dhidi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kupaka watu matope, kutoa taarifa za uzushi na zenye lengo la kufarakanisha watu.

President Suluhu inspects a guard of honour

Chanzo cha picha, Tanzania State House

Maelezo ya picha, Rais Samia akikagua gwaride la heshima baada ya kuapishwa kuwa rais wa sita wa Tanzania

Kuna makundi mawili ambayo aliyazungumza jana kwenye eneo hilo la mitandao - moja likiwa linaona kama limeguswa moja kwa moja na lingine likiwa kimya. Kundi linaloona limeguswa moja kwa moja ni lile la wanaharakati wanaofanya kazi zao kwa kuficha majina yao halisi ambao Samia alisema kuna siku siku watapatikana.

Kundi la pili aliloligusa ni la wale wanaozusha kwamba kifo cha Magufuli hakikutokana na ugonjwa uliotangazwa kwenye taarifa rasmi ya serikali bali vitu vingine ikiwamo kulishwa sumu.

Maneno ya namna hii yamekuwa yakisambazwa zaidi na kundi la watu wanaohusishwa moja kwa moja na utawala wa Rais Magufuli na ni kundi hili ambalo limeguswa lakini kutazamwa kwake kumepita chini ya rada.

Nini kinafuata kwa Samia?

Hotuba ya jana bungeni, ndiyo imefungua rasmi utawala wa Samia kama Rais wa Awamu ya Sita wa Tanzania. Inatarajiwa kwamba sasa ataanza rasmi utekelezaji wa ahadi zake ikiwamo kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uteuzi.

Kuna uwezekano kwamba huenda akatangaza uteuzi wa mwanamke katika mojawapo ya nafasi za juu za uongozi ambazo hazijawahi kushikiliwa na mwanamke katika historia ya Tanzania.

Na ili kukihakikishia chama chake nafasi ya kufanya vizuri katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025, Samia anatarajiwa kuanza kufanya mambo kadhaa yatakayosaidia kujenga imani ya wananchi kwake - yakiwamo mambo ambayo wengi walitaraji angeyatangaza jana lakini hakufanya hivyo.

Na ingawa alisisitiza jana kwamba yeye na Magufuli ni kitu kimoja; kwa tabia, makuzi, haiba na matamshi yake, haionekani kwamba Samia anaweza kukaribia kufanya mambo ambayo yamesababisha urathi wa Magufuli uwe jambo linalogawanya watu.

Na ingawa, watu wake wa karibu wanasisitiza ana nia ya kufanya mabadiliko kwa haraka, anafahamu kwamba kuna dude moja kubwa linafuatilia na kuangalia kila anachofanya - CCM.