Yafahamu mataifa ya Mashariki ya Kati yanayoongoza kwa adhabu ya kunyonga

Mataifa manne yanayoongoza katika orodha ya yaliyotoa hukumu ya kunyongwa mwaka 2020 yalikuwa ni kutoka Mashariki ya Kati, shirika la Amnesty International limesema.

Nchi za Iran, Misri, Iraq na Saudi Arabia zilichangia asilimia 88 ya visa 483 vya hukumu ya kunyongwa kote duniani, kulingana na ripoti ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu.

Shirika hilo liliwashutumu kwa kuonesha "ukatili" wakati maitaifa mengine mengi duniani yalikuwa yanaangazia zaidi kunusuru watu kutokana na janga la virusi vya corona.

Kwa ujumla, idadi ya walio hukumiwa kunyongwa dunia ilikuwa ya chini katika kipindi cha miongo kadhaa lakini haikujumuisha China.

China inaaminika kuwahukumu kunyongwa maelfu ya watu kila mwaka lakini data yao kuhusiana na suala hilo ni siri kubwa ya serikali.

Usiri huo pia ulishuhudiwa Korea Kaskazini na Vietnam na kufanya iwe vigumu kuthibitisha taarifa zizo hizo za mataifa hayo mawili.

Hukumu ya kunyongwa kwa watu 483 katika nchi 18 iliripotiwa mwaka 2020 ikiwakilisha kupungua kwa visa hivyo kwa asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo matukio 657 yaliripotiwa na kupungua kwa asilimia 70 tangu wakati idadi hiyo ilipofikia kilele chake ya 1,634 mwaka 2015, Shirika la Amnesty International limesema Jumatano katika ripoti yake ya kila mwaka ya utumiaji wa adhabu ya kifo.

Mashariki ya Kati, jumla ya idadi hiyo ilipungua kutoka 579 mwaka 2019 hadi 437 mwaka 2020. Hilo lilichangiwa pakubwa na kupungua kurekodiwa kwa visa hivyo kwa asilimia 85 Saudi Arabia ambako watu 27 walinyongwa, na asilimia 50 ya visa hivyo nchini Iraq ambayo ilirekodi visa 45.

Hatahivyo, ripoti hiyo inasema kupungua kwa hukumu hiyo kulizidiwa na nchi ya Misri ambako visa hivyo viliongezeka kwa asilimia 300, huku watu 107 wakihukumiwa kifo na kuwa taifa la tatu duniani lenye kutekeleza hukumu hiyo mara kwa mara.

Asilimia 23 ya watu hao walihukumiwa kwa kesi zenye kuhusishwa na ghasia za kisiasa baada ya kile shirika la Amnesty limesema ni hukumu za kuonewa zenye kuambatana na "kukiri" kwa kulazimishwa na ukiukaji mwingine.

Pia kulikuwa na ongezeko la visa 57 vya hukumu ya kunyongwa mnamo mwezi Oktoba na Novemba kufuatia jaribio lililotibuka katika gereza la al- Aqrab ambapo maafisa kadhaa na wafungwa wa kesi za kifo waliaga dunia.

Iran ambayo ilitekeleza hukumu ya kuyongwa kwa karibu watu 246 bado ni ya pili duniani nyuma ya China.

Shirika la Amnesty limesema serikali ya Iran ilitumia sana hukumu ya kifo kama "silaha ya kuwakandamiza kisiasa" wapinzani wake na watu wa makundi madogo.

Pia ilinyonga watu watatu kwa uhalifu uliotokea walipokuwa na umri wa chini ya miaka 18, hatua ambayo ni ukiukaji wa sheria za kibinadamu kimataifa.

Shirika la Amnesty lilishutumu Qatar kwa "kurudi nyuma" na kuanza kutekeleza tena hukumu ya kunyongwa katika kipindi cha miaka 20. Mwanamume raia wa Nepali aliyehukumiwa kwa mauaji alipigwa risasi na kikosi maalum mnamo mwezi Mei.

Marekani, utawala wa Trump ulirejea hukumu ya kunyongwa baada ya miaka 17 na watu 10 wakahukumiwa kifo chini ya miezi sita.

India, Oman, Qatar na Taiwan pia zilirejelea hukumu ya kunyongwa.

"Wakati dunia imeelekeza nguvu zake kwenye kukabiliana na ugonjwa wa corona, serikali kadhaa zilionesha malengo tofauti na kuamua kutekeleza hukumu ya kifo na kunyonga watu," Agnès Callamard, Katibu Mkuu wa Shirika la Amnesty International alisema katika taarifa.

"Hukumu ya kifo ni adhabu inayochukiza na kutekeleza hukumu ya kunyongwa katikati ya janga kunaelezea zaidi ukatili uliopo."

Bi. Callamard alisema watu waliokuwa wanakabiliwa na hukumu ya kifo walishindwa kufikia wawakilishi wa kisheria na kwamba idadi kubwa ya waliotaka kutoa usaidizi walilazimika kuhatarisha afya zao.

"Utumiaji wa hukumu ya kifo chini ya hali kama hizo ni shambulio baya kwa kuzingatia haki za kibinadamu.