Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini Phillip Mpango?
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
Dkt. Philip Isidory Mpango aliyetangazwa kuwa Makamu wa Rais mteule wa Tanzania ni mchumi wa kiwango cha juu lakini ni mtu aliyeingia kwenye siasa kwa bahati mbaya.
Kiti cha Makamu wa Rais wa Tanzania kilikuwa wazi kufuatia kifo cha Rais John Magufuli mnamo Machi 17 mwaka huu kilichofanya aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aapishwe kuwa Rais.
Dk. Mpango hana tabia za kawaida unazoweza kuzihusisha na wanasiasa wa Afrika. Mpango ni msema kweli, mwadilifu, mcha Mungu na mtu ambaye anaamini katika vitendo kuliko maneno.
Sababu hizo, pamoja na uwezo wake kama mchumi, ndizo zilizomfanya abaki kuwa Waziri wa Fedha katika muda wote wa miaka sita ya utawala wa Rais Magufuli.
Jambo hilo si dogo kwa sababu wizara hiyo ilikuwa ikiangaliwa kwa jicho la karibu na Rais Magufuli ambaye alijulikana kwa kutovumilia wateule wake ambao walionekana kutokidhi matarajio yake.
Dk. Mpango ni mwanasiasa wa bahati mbaya kwa sababu katika utumishi wake wa takribani miaka 40 serikalini, mara zote alitumika kama mtaalamu na aliingia kwenye siasa kwa kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na baadaye waziri miaka sita iliyopita.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ulikuwa ni mara yake ya kwanza kuwania ubunge - bila shaka kwa kutosubiri tena kupata huruma ya Rais Magufuli ya kuteuliwa.
Nini kimesukuma uteuzi wake?
Katika mazungumzo yangu na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali, inaonekana kwamba serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kumpa Makamu wa Rais kazi kubwa ya kusimamia uchumi.
Kutokana na uzoefu wake wa kuwa Waziri wa Fedha wakati wote wa Magufuli, ushiriki wake katika kutengeneza Mpango wa Taifa wa Maendeleo, uelewa wake wa serikali na ubobezi wake kama mchumi, nafasi hiyo imepata mtu hasa aliyetakiwa.
Kufuatia vifo vya wachumi mashuhuri wa Tanzania kama Profesa Benno Ndullu na Dk. Servacius Beda Likwelile, Mpango anatajwa kuwa mmoja wa wachumi bora wa Tanzania walio hai.
Kuna kipindi, wakati wa Utawala wa Rais Kikwete, jina la Mpango lilikuwa likitajwa kama mmoja wa watu ambao walipendekezwa kuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) baada ya kifo cha Dk. Daudi Balali mwaka 2008.
Umakamu Rais wa Mpango pia unaweka sawa baadhi ya kanuni ambazo haziandikwi lakini zimezoeleka katika desturi na utamaduni wa kisiasa wa Tanzania.
Yeye anatoka katika Mkoa wa Kigoma - mojawapo ya mikoa ya pembezoni ya Tanzania ambayo haijawahi kutoa Rais, Makamu wa Rais wala Waziri Mkuu. Uteuzi huu umetoa fursa kwa eneo ambalo halijawahi kutoa mmoja wa viongozi wakuu watatu wa Tanzania, kupata fursa hiyo.
Kwa Tanzania, mara nyingi, nafasi ya Rais na Makamu wake hushikwa na watu kutoka dini mbili kubwa za Tanzania; Wakristo na Waislamu - ingawa imetokea kwa Rais na Makamu kuwa dini moja; mara nyingi hii ikitokea wakati Rais wa Tanzania anapokuwa Mwislamu kutoka Bara kwa vile Makamu hutakiwa kutoka Zanzibar ambako asilimia 99 ni Waislamu.
Uteuzi wa Mpango umeweka tena uwiano huo wa kidini ambao ni sehemu ya utamaduni na desturi ya siasa za Tanzania.
Kuepusha matatizo yasiyoonekana
Uteuzi wa Mpango pia, utakuwa umezingatia tabia yake. Kwa sababu anajulikana kwa kutokuwa na tamaa ya madaraka, sifa hiyo ni muhimu katika mazingira ambayo Rais Samia ndiyo kwanza anaweka mizizi yake kama mtawala wa Tanzania.
Endapo nafasi hiyo angepewa mwanasiasa anayefahamika kwa kuwa na matamanio makubwa ya kisiasa, jambo hilo lingeweza kuleta shida katika siku za mbele kwa Rais na Makamu wake kushindana kupata umaarufu.
Mapungufu na lawama kwa Mpango
Pamoja na sifa zote hizo, Mpango hatarajiwi kuwa mtu atakayesababisha CCM kushinda katika chaguzo zijazo kwa sababu si mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika jamii.
Kwa sababu ya kuchelewa kuingia kwenye siasa, kutojihusisha sana katika mambo ambayo Watanzania wengi wanayapenda, Mpango si aina ya wanasiasa unaoweza kuwaita vipenzi vya watu.
Hata hivyo, kama uchumi wa Tanzania utafanya vizuri katika kipindi ambacho Samia yuko madarakani, CCM itapanda katika ushawishi wake. Kama ambavyo Rais wa zamani wa Marekani alipata kusema; It is the economy, stupid...
Katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na janga la ugonjwa wa Corona, Mpango alikosolewa na wengi kutokana na kitendo chake cha kufanya mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma akionekana mgonjwa.
Ingawa kulikuwa na uvumi kuwa amepata maambukizi ya Corona na huenda amefariki dunia, Mpango alifanya mkutano huo akiwa hajavaa barakoa - na akikohoa mbele ya watu ambao hawakuwa wamevaa barakoa.
Kitendo hicho - kwa wakosoaji wake, kilimweka katika kundi la viongozi wanaobisha uwepo wa janga hilo hapa nchini - ingawa wanaomfahamu wanataja huo kama ushahidi wa udhaifu wake mwingine - utii usio na shaka kwa mamlaka.
Mpango amesoma uchumi kwa kiwango cha uzamivu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Lund cha Sweden.