Jakaya Mrisho Kikwete: Magufuli alikua chaguo langu

Kikwete

Kumekuwa na madai kuwa huenda uhusiano kati ya aliyekuwa rais wa awamu ya nne wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete na mrithi wake Hayati Dkt John Pombe Magufuli ulikuwa na doa hususan kutokana na mitindo yao tofauti ya uongozi.

Hatahivyo wakati wa mazishi ya hayati Magufuli Jakaya Kikwete aliweka wazi kwamba mahusiano yao yalikuwa mazuri.

Alisema Magufuli ndiye aliyekuwa chaguo lake la kwanza katika orodha ya watu 38 waliojitokeza kutaka kugombea urais kupitia chama cha CCM kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kikwete alielezea jinsi uhusiano wake na Magufuli ulikuwa mzuri kuanzia walipohudumu wote katika baraza la mawaziri na hata ndiye waziri pekee aliyekuwa akiweza kumfanyia utani.

'Kwa vile alikuwa mtano wangu yeye ndiye pekee aliyeweza kunitania kila tulipokutana ,wengine walikuwa hawawezi ..'

Kikwete aliyasema hayo siku ya ijumaa Chato wiki iliyopita baada ya ibada maalumu ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Magufuli aliyezikwa nyumbani kwake katika kijiji cha Mlimani wilayani humo.

Rais huyo wa zamani alikuwa miongoni mwa viongozi waliozungumza na waombolezaji katika shughuli hiyo ya mazishi.

Magufuli alifariki Machi 17 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo baada ya kulazwa kwa siku chache.

Alisema wakati wa utawala wake, alimteua Magufuli kuwa waziri katika wizara tatu tofauti ili akasawazieshe mambo kwa sababu wizara hizo hazikuwa zikifanya vizuri

Alisema alipoanza urais, alimteua Wizara ya Ardhi, kisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi na baadaye Wizara ya Ujenzi.

Bwana Jakaya Kikwete akizungumza katika mazishi ya Hayati Dkt john Pombe Magufuli
Maelezo ya picha, Bwana Jakaya Kikwete akizungumza katika mazishi ya Hayati Dkt john Pombe Magufuli

Kikwete alifichua jinsi Hayati Magufuli alivyompa kiwanja ili aweze kujenga nyumba huko Chato alipokuwa mbunge na waziri na hata aliongeza kiwanja hicho wakati alipokuwa rais . Kiongozi huyo wa zamani wa Tanzania alisema alitazamia kujenga nyumba ili Magufuli akistaafu waweze kupiga soga katika nyumba yake hiyo.

Rais huyo wa zamani aliongeza kwamba Magufuli alikuwa mmoja wa mawaziri wake ambao aliweza kuwaamini na kuwatumaini.

'Alikuwa jembe langu..ndio maana nilimuweka katika wizara tatu' alisema Kikwete

Akisumulia kilichotokea hadi Magufuli alipotunukiwa tiketi ya CCM kugombea urais , Kikwete alisema ;

"Katika majina matano niliyoyafikisha kwenye vikao vya juu vya chama… Tulikuwa na watu 38, kazi yangu ilikuwa ni kuwapunguza wale 38 ili nipate watano, lakini sikuwa na tabu na Magufuli ndio alikuwa chaguo langu la kwanza halafu nikaongeza na wengine,"

Katika kinachooelezea uamuzi wa chama cha CCM kumpa Magufuli tiketi hiyo Kikwete alisema ;

"Nikawaambia jamani eeh, lazima sasa, mimi ndio ninayeondoka tukabidhi kizazi kwa wadogo zetu. Nilijitahidi na wakati mwingine ukiwa Rais na mwenyekiti, una nguvu. Tukakubaliana'.

Wakati wa mchakato huo, majina matano yaliyopitishwa na Kamati Kuu yalikuwa ni Bernard Membe, John Magufuli, Asha-Rose Migiro, January Makamba na Amina Salum Ali.

Baadaye majina matatu yalipitishwa na halmashauri kuu ya CCM kwenda kwenye mkutano mkuu, majina hayo ni Magufuli, Migiro na Amina Salum Ali.

Mkutano mkuu ulipiga kura na kumchagua Magufuli kuwa mgombea urais wa CCM.

Kutoka na historia ya urafiki wao kwa muda huo mrefu Kikwete alisema aliwashangaa watu waliokuwa wakisema hakumtaka Magufuli na kukana taarifa hizo.

"Ooh, JK anamchukia JPM, hee! Labda sio mimi. Unamchukiaje mtu uliyemkabidhi ilani ya uchaguzi na ameitekeleza kwa kiwango cha juu sana, wee utamchukia kwa sababu ipi? Lakini nikasema duniani waganga njaa wengi, wengine wanapata mradi wao kwa kuongopa," alisema.

Unaweza pia kusoma:

Kikwete pia alisifia uchapakazi wa Hayati Magufuli akisema hakuwa mtu wa kuvimilia uzembe ,ufisadi na ubadhirifu wa fedha. Hilo lilidhihirika na hatua nyingi alizozichukua wakati wa utawala wake ambapo aliwaachisha kazi wafanyikazi wa serikali waliopatikana na makosa ya ufisadi na uzembe kazini.

Kikwete aliahidi kuendelea kusimama na familia ya Hayati Magufuli akisema;

' Napenda niwahakikishie kwamba majonzi yenu ni yetu na uchungu wenu ni wetu pia tunaendelea kuwa karibu nanyi kama ilivyokuwa siku zote ninyi ni sehemu yetu nasi ni sehemu yenu'