Chama cha ACT-Wazalendo chapendekeza jina kwa Rais wa Zanzibar

Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, marehemu Seif Sharif Hamad

Chama cha ACT-Wazalendo kimempendekeza mrithi wa aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.

Kiongozi wa chama hicho Zitto kabwe ameyasema hayo katika siku ya dua maalum ya kumuombea marehemu Maalim Seif jijini Dar es Salaam.

Akitoa shukrani kwa waliofika kumuombea Marehemu, Bw. Zitto amesema kuwa ;

"Tayari tumeshapendekeza jina kwa Rais wa Zanzibar la mtu ambaye atarithi majukumu ambayo Maalim Seif alikuwa anayafanya.

''Bahati nzuri, Maalim alikuwa ni Kiongozi. Alikuwa anajua ipo siku Mwenyezi Mungu atamchukua kwa sababu sisi sote lazima turejee kwa Mwenyezi Mungu kama tulivyoambiwa na mafunzo ya dini yetu na dini zote. Alisema Zitto Kabwe.Amesema kuwa marehemu aliacha maelekezo ya nini kitokee iwapo atakua ametangulia mbele ya haki.

''Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba viongozi wa Chama wamefuata yale maelekezo yake kwa namna ambayo Kiongozi wetu alituelekeza. Na sasa umebaki wajibu wa Rais wa Zanzibar kwa ajili ya kuyatekeleza hayo.'' alisema

Chama cha ACT kina imani kuwa huyo ambaye amependekezwa ataweza kusimamia maridhiano ya Wazanzibari na ataweza kusimamia haki za Wazanzibari, kama ambavyo Maalim Seif mwenyewe alikuwa akifanya.

''Kwa hiyo tayari tumeanza kutekeleza wajibu, tunawaomba muendelee kutuombea dua ili tusitoke kwenye mstari, tuweze kuendelea kupigania demokrasia, kupoiginania haki na kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa ya amani ili iweze kupata maendeleo ya watu." Alisema Bw.Zitto

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alifariki tarehe 17.02.2021 na kuzikwa tarehe 18 mwezi Februari mwaka 2021

Alizikwa nyumbani kwake katika kijiji cha Mtambwe Nyali mkoa wa Kaskazini Pemba.