Virusi vya corona: WHO yaomba Tanzania kutoa takwimu ya walioambukizwa corona

Muda wa kusoma: Dakika 1

Shirika la Afya Duniani WHO, kwa mara nyingine tena limetoa wito kwa mamlaka nchini Tanzania kuanza kutoa takwimu za watu waliambukizwa ugonjwa wa Covid 19 likisema itasaidia kuwakinga Watanzania na wale wanaotangamana nao.

Hii sio mara ya kwanza WHO limetoa ombi hili tangu serikali ilipoacha kutoa takwimu ya maambukizi ya Covid 19 na idadi ya vifo vilivyotokana na ugonjwa huo.

Katika taarifa yake ya hivi punde kuhusu mwenendo wa Covid 19 nchini Tanzania, shirika hilo lilielelezea wasi wasi wake kuhusu idadi ya wasafiri wa Tanzania waliopatikana na kuwa na virusi vya corona.

Huku hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Tanzania Kasim Majaaliwa ametoa wito kwa watu kuchukua tahadhari dhidi ya kueneza virusi vya corona kwa kuzingatia muongozo wa afya uliyowekwa ikiwa ni pamoja na kuvalia barakoa.

Bw. Majaaliwa alisema hayo katika ibada ya mazishi ya katibu mkuu kiongozi mhandisi Balozi John Kijazi aliyefariki Jumatano kutokana na ugonjwa ambao chanzo chake hakikutajwa.

Leo ni siku ya mwisho ya maombi yaliyotangazwana Rais John Magufuli kupitia ombi alilotoa kwa viongozi wa kidini kufanya ibada maalum ya kulinda nchi dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona

Mapema mwaka jana, rais pia alitoa wito kama huo wa maombi ya siku tatu kwa taifa na baadaye kutangaza kuwa taifa limefanikiwa kukabiliana na Covid 19.

Pia unaweza kutazama: