Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania: Taifa linalokataa chanjo dhidi ya Corona
Kwa miezi kadhaa sasa serikali ya Tanzania imekuwa ikisisitiza kuwa hakuna ugonjwa wa Covid-19 - na hivyo hakuna mipango yoyote ya kuwachanja wananchi wake.
BBC imezungumza na familia moja ambayo inaomboleza kifo cha mume na baba ambaye anadhaniwa kuwa alipata maambukizi ya corona. Hofu iliyopo ni kuwa, japo serikali inakanusha uwepo wa janga, watu wengi wanapoteza maisha kutokana na mlipuko wa virusi hivyo.
Peter - si jina lake halisi - alirejea nyumbani akitoka kazini huku akiwa amepoteza ladha ya chakula na kifua kikavu, baada ya wiki moja ya kuugua nyumbani alipelekwa hospitali ambapo baada ya saa chache alipoteza maisha. Peter hakufanyiwa vipimo vya corona. Kuna upimaji wa kiwango cha chini ambao unafanyika Tanzania ukulinganisha na nchi nyengine.
Ni vigumu kukadiria ni kwa kiasi gani mlipuko wa corona ulivyopenya Tanzania na ni maafisa wachahce tu wa ngazi ya juu serikalini ambao wanaruhusiwa kuzungumzia hilo. Hata hivyo, kauli mbalimbali ambazo zimetolewa katika siku za hivi karibuni zimetoa taswira ambayo ni tofauti kabisa na uhalisia unaokabiliwa na baadhi ya wananchi, kama mke wa Peter, ambao wanaomboleza kwa ukimya vifo vya wapendwa wao ambao wanadhaniwa kufariki baada ya kuambukizwa virusi hivyo.
Familia kadhaa nchini Tanzania zinapitia kipindi kigumu kama familia ya Peter, lakini hata hivyo zimeamua kukaa kimya, zikiogopa madhara ambayo yanaweza kuwakuta kwa kuzungumza.
Serikali ya Uingereza imepiga marufuku wasafiri wote kutoka Tanzania, isipokuwa wenye vibali vya kazi, wakati ambapo Marekani imewaonya raia wake dhidi ya kutembelea Tanzania kutokana na corona.
Mzozo wa chanjo
Toka mwezi Juni mwaka jana ambapo rais John Magufuli alipotangaza Tanzania haina tena corona, yeye pamoja na viongozi wengine wamekuwa mstari wa mbele kukosoa baadhi ya njia za kupambana na corona na kusisitiza kuwa Tanzania haitatumia mbinu hizo.
Rais Magufuli pia ameonya - bila kutoa ushahidi - kuwa chanjo za Covid-19 zinaweza kuwa na madhara na badala yake amewarai Watanzania kujifukiza na kutumia dawa za asili, ambazo hakuna hata moja iliyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama tiba dhidi ya virusi vya corona.
Ni vigumu kujua kwa nini rais Magufuli amechukua msimamo huo dhidi ya chanjo lakini pia amesema Watanzania wasitumike kama sehemu ya majaribio.
"Kama wazungu wangekuwa na kinga, basi kusingekuwa na Ukimwi, kansa na Kifua Kikuu kufikia sasa," ameeleza Magufuli ambaye amejipambanua kama mtu anayepingana na ubeberu.
WHO hata hivyo inapinga msimamo huo.
"Chanjo zinafanya kazi na naishauri serikali ya Tanzania] kujiandaa na kampeni ya chanjo ya Covid," amesema Dkt Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO barani Africa, na kuongeza kuwa shirika hilo lipo tayari kuisaidia Tanzania.
Waziri wa Afya Dorothy Gwajima amesisitizia msimamo wa Bw Magufuli juu ya chanjo, akisema kuwa wizara yake "ina taratibu zake za kuagiza dawa na hufanya hivyo baada ya kujiridhisha juu ya ubora wake."
Dkt Gwajima aliyasema hayo mwanzoni mwa wiki alipokutana na waandishi wa habari ambapo wizara ya afya ilionesha namna gani ya kutengeneza kinywaji cha asili kwa kutumia tangawizi, vitunguu, ndimu na pilili - mchanganyiko ambao wanadai, bila Ushahidi, kuwa unasaidia kumkinga mtu dhidi ya maambukizi ya corona.
Waziri huyo pia amesisitiza juu ya usafi binafsi, kuosha mikono na maji tiririka na sabuni, kujifukiza, kufanya mazoezi, kula lishe bora pamoja na kutumia tiba asili ambazo zimejaa Tanzania.
Lakini hatua zote hizo si kwa kuwa Tanzania kuna corona. Waziri ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kuandaliwa kwa kuwa corona ipo nchi jirani.
Baadhi ya madaktari hawakubaliani na msimamo wa serikali.
"Tatizo ni kuwa serikali inawahakikishia wananchi kuwa tiba asili, ndio suluhisho pekee la kujikinga na corona. Pamoja na faida zake, zinaweza kusaidia kuinua kinga ya mwili na kadhalika, lakini tiba asili si kinga ya corona," daktari mmoja ameiambia BBC kwa sharti la kutotajwa jina na kuwataka wananchi wachukue tahadhari.
Hivi karibuni, Kanisa Katoliki lilivunja ukimya na kuwaonya wananchi kuchukua tahadhari zote.
"Covid haijaisha, bado ipo. Tusipuuze, inatupasa tujilinde, osha mikono yako na maji na sabuni. Pia inabidi turejee kuvaa barakoa," Askofu Mkuu wa jimbo la Dar es Salaam Dar es Salaam Yuda Thadei Ruwaichi aliwaambia waumini.
Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania Episcopal Conference, Dkt Charles Kitima, ameiambia BBC kuwa kanisa limeshuhudia ongezeko la vifo, hususani mjini.
"Tulizoea parokia za miji mikubwa misa ya mazishi moja ama mbili kwa wiki. Sasa kila siku kuna msiba. Tumeona hiki kitu si cha kawaida, kuna kitu hakiko sawa," Padre Kitima aliieleza BBC.
Waziri wa Afya hata hivyo alionya kuwa matamko yasiyo rasmi kutoka serikalini yamekuwa yakishtua watu. Lakini kutokuwepo kwa takwimu rasmi kutoka kwa serikali kunafanya hata mjadala wa hali ya mambo ulivyo kuwa mgumu.
'Vaa barakoa - lakini si kwa sababu ya corona'
Licha ya serikali kukanusha uwepo wa corona lakini kuna baadhi ya kauli za viongozi ambazo zinajenga picha tofauti.
Mwezi uliopita siku moja tu baada ya Kanisa Katoliki kutoa tamko lake na siku chache baada ya Denmark kutangaza kuwa wasfiri wawili kutoka Tanzania wamegundulika kuwa na virusi vipya vya corona, rais Magufuli aliwalaumu baadhi ya Watanzania walioenda kuchanjwa ughaibuni kwa "kuleta corona ya ajabu ajabu."
Ijumaa, gazeti la Mwananchi nchini Tanzania limemnukuu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Profesa Mabula Mchembe akisema kuwa uvaaji wa barakoa " si kwa sababu ya corona, kama baadhi ya watu wanavyodhani, lakini ni kwa kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya hewa."
Jambo moja ambalo limetia doa msimamo wa serikali ni tangazo kwa umma kutoka chama cha ACT Wazalendo kuwa mmoja ya viongozi wake wakuu, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar pamoja na mkewe na wasaidizi wake kadhaa wamekutwa na maambuzi ya corona.
Serikali mpaka sasa haijaongelea chochote juu ya hali ya Maalim Seif, pia haijajibu maombi ya BBC ya kutoa maoni yake kuhusu taarifa hii.
Januari 21, siku ambayo Peter alianza kuugua, kuna taarifa nyengine kuhusiana na corona iliokuwa ikiendelea mjini Moshi.
Uongozi wa shule moja maarufu ya kimataifa ulikuwa ukiomba radhi na kubadili taarifa kuwa moja ya wanafunzi wao alikutwa na corona na kusimamisha masomo ya ana kwa ana.
Wakati hali ya mambo ikiendelea kama kawaida nchini Tanzania, mke wa Peter amezongwa na majuto moyoni mwake kwa kuwa kama ilivyo kwa wananchi wengine yeye na mumewe hawakuchukua tahadhari yoyote kujilinda.
Kutokujilinda kwao pengine si jambo la kushangaza katika nchi ambayo raisi wake na viongozi waandamizi wamekuwa wakisisitiza kuwa "hakuna corona."
Pia unaweza kutazama: