Biden amaliza mgogoro juu ya mwanamke wa kwanza mwafrika kuongoza WTO

Utawala wa Biden umemaliza mgogoro uliokuwa umetokea juu ya uteuzi wa mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) kwa kumuunga mkono aliyekuwa waziri wa fedha nchini Nigeria.

Ngozi Okonjo-Iweala alikuwa anaongoza miongoni mwa waliokuwa wanawania wadhifa huo hadi mwezi Oktoba, utawala wa Trump uliposema kuwa haumuungi mkono badala yake unataka mwanamke mwingine wa Korea Kusini, Too Myung-hee kuchukua uongozi wa shirika hilo.

Bi. Yoo sasa amejiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Ikiwa itathibitishwa, Dkt. Okonjo-Iweala atakuwa mwanamke wa kwanza na mwafrika wa kwanza vilevile, kuongoza shirika la WTO.

Dkt. Okonjo-Iweala Ijumaa alimsifu mpinzani wake kwa ujumbe wake aliotoa na kusema: "Kuna kazi muhimu mbele yetu inayohitaji ushirikiano wetu pamoja."

Kamati ya uteuzi ya WTO mnamo mwezi Oktoba ilipendekeza wanachama wake 164 kumteua Dkt. Okonjo-Iweala kuchukua nafasi ya kiongozi anayeondoka wa shirika hilo Roberto Azevedo; na msemaji wa kamati hiyo akasema wote wameidhinisha uteuzi huo isipokuwa mmoja tu.

Rais Donald Trump - aliyeelezea WTO kama shirika "baya" na lenye kupendelea China - na alimtaka Bi. Yoo, waziri wa biashara nchini Korea Kusini kuchukua wadhifa huo.