Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Rwanda yaorodheshwa miongoni mwa nchi 10 zinazokabiliana vyema na Covid-19 duniani
Taasisi ya utafiti ya Sydney nchini Australia imetangaza jinsi nchi 100 duniani zinavyokabiliana na Covid-19 ambapo Rwanda inashikilia nafasi ya 10 za kwanza katika kukabiliana na virusi hivyo.
Ripoti ya taasisi hiyo inasema hakuna nchi iliyoshinda mapambano dhidi ya janga la corona, na kwamba ripoti yake imezingatia mipango mbalimbali iliyowekwa na nchi husika katika kupambana na maambukizi hayo.
Katika orodha hiyo taifa la New Zealand linaongoza huku Brazil ikiwa ya mwisho katika juhudi za kupambana na Covid.
Marekani pia ni miongoni mwa nchi 10 za mwisho katika kukabiliana na corona.
Taasisi hiyo-Lowy inasema kuwa kwa kuzingatia vipimo mbalimbali hufanya utafiti huo kwa kulinganisha nchi, kiwango cha upimaji wa virusi kulingana na idadi ya watu, idadi ya watu wanaoambukizwa, na idadi ya wanaokufa na kutathmini taarifa zinazotolewa na vigezo vingine.
Ripoti hii inasema: "kwa kuzingatia vipimo hivi kwa pamoja, tunaweza kufahamu uwezo wa nchi zinazofanya vyema au vibaya katika kukabiliana na janga hili "
Baada ya nchi ya New Zealand - nchi ambayo imeweza kudhibiti kabisa janga la corona nchi nyingine 10 zinazofuata katika kudhibiti vyema corona kwa kuweka amri ya kukaa nyumbani ''lockdown'' na kupima mara kwa mara ni - Vietnam, Taiwan, Thailand, Cyprus, Rwanda, Iceland, Australia, Latvia na Sri Lanka.
Unaweza pia kusoma:
Mwezi Machi mwaka uliopita, Rwanda ilitangaza agizo la kukaa nyumbani (lockdown) kote nchini humo likiwa ni taifa la kwanza kuweka amri hiyo miongoni mwa nchi zilizopo kusini mwa jangwa la sahara, wakati huo Rwanda ilikuwa na wagonjwa wa Covid 17 pekee.
Baadhi ya wakosoaji wa serikali ya Rwanda, na baadhi ya watu binafsi walilalamika kuwa hatua zilikuwa kali sana na zingeweza kuleta athari mbaya kwa maisha ya raia wanaoishi kwa kutegemea pato la siku.
Miezi iliyofuata, uongozi wa Rwanda ulisifiwa na mataifa kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika kukabiliana na janga la corona. Idadi ya maambukizi na vifo iliendelea pia kuwa ya chini.
Hata hivyo wimbi la pili la maambukizi ya virusi vya corona liliongeza idadi ya wagonjwa pamoja na vifo duniani.
Rwanda haikusazwa, kwani mwezi huu pekee watu waliopatwa na maambukizi mapya walikuwa ni zaidi ya theluthi moja ya idadi ya watu 14,166 wote walliopatwa na maambukizi hadi sasa.
Waliokufa kutokana na corona mwezi huu pekee wamepita nusu ya watu 183 ambao ndio waliokufa kwa ujumla tangu kuanza kwa janga la corona, kulingana na takwimu za wizara ya afya.
Ripoti ya Lowy iliorodhesha nchi kwa kuzingatia vipimo mbalimbali na kutoa alama 100 kwa kila nchi , na Rwanda ina 80%, ambapo nchi ya pili ya Afrika kwenye orodha hii ni Togo ambayo iko katika nafasi ya 15.
Katika orodha ya nchi 98 zilizpfanyiwa utafiti huu, Brazil ilikuwa ya mwisho na alama ya 4%, huku Marekani ikichukua nafasi ya 94 na alama ya 7%.
Nchini Brazil Covid-19 tayari imewaua watu 220,000 huku ikiwauwa Wamarekani zaidi ya 430,000.
Katika kipindi hiki cha janga la Corona nchi hizi mbili zimekuwa na uongozi usiotilia maanani udhibiti wa janga. Marais Jair Bolsonaro na Donald Trump walipinga uvaaji wa barakoa na amri za kukaa nyumbani 'lockdown', na baadaye wawili hao walipatwa na maambukiz ya Covid-19.
Nchi kama vile China, Tanzania, Burundi haziko katika orodha hii kwasbabu ''hazina takwimu " kulingana na taasisi ya Lowy.
Ripoti hii inasema kuwa hakuna nchi iliyoshinda mapambano dhidi ya janga hili, lakini mbinu za kukabiliana kuwa tofauti.
Inasema : "Baadhi ya nchi zimekabiliana vizuri zaidi ya nchi nyingine - baadhi zilishindwa...Kwa ujumla nchi zenye raia wachache na taasisi thabiti zina fursa katika kupambana na janga hili."
Zaidi ya watu milioni 100 wamekwishapata maambukizi ya Covid-19 kote duniani , na wengine karibu milioni 2.2 wamekufa kutokana na janga hili.