Rajini Chandy: Muigiza wa kike India, 69, apata umaarufu kwa picha zake za kuvutia

Rajini Chandy

Chanzo cha picha, Athira Joy

Rajini Chandy alipoweka picha zake za kuvutia kwenye mtandao ya Facebook hivi karibuni, hakutarajia kuwa zitasambaa na kuvutia wengi zaidi.

Picha hizo zinamuonesha mwanamke mwenye umri wa miaka, 69, ambaye sasa hivi ni muigizaji akiwa amevaa nguo zake maarufu nchini India aina ya sari, magauni yake marefu, suruali ya jeans na gauni fupi.

Kwenye picha zingine amejipamba maua kama taji ambayo ameyatoa katika bustani yake.

Mama huyo alielezewa kama "mrembo" na vyombo vya habari vya eneo kusini mwa India katika jimbo la Kerala ambako anaishi.

Nguo alizovaa kulingana na picha hizo, zimesababisha mjadala kwasababu wanawake wengi bado huvaa nguo za kitamaduni aina ya sari au sketi ndefu.

Wazo la kuvaa nguo aina hiyo ni la mpiga picha Athira Joy, 29, Chandy amezungumza na BBC.

Bi Joy alisema kile kinachomvutia yeye kwa muigizaji huyo wa kike ni vile alivyotofauti kabisa na kina mama wengine.

"Wanawake wa India," anasema, "maisha yao yote huwa wamejifungia katika mfumo wa ndoa na kulea familia. Wengi huachana na maisha ya kisasa wanapotimiza umri wa miaka 60 kwasababu wanakuwa na wajukuu."

Mama yake, 65, anasema, "mwanamke wa India mwenye matatizo ya kila aina ya kiafya yaani uso wake huonekana ana umri wa miaka 60 na zaidi".

"Lakini Rajini ni tofauti - Anajitunza vizuri, unene wake uko sawa, ana ujasiri, ni mzuri na pia mitindo yake ni ya kisasa. Ana umri wa miaka 69, lakini katika akili yake ana umri wa miaka 29, kama tu mimi."

Rajini Chandy

Chanzo cha picha, Athira Joy

Maelezo ya picha, Rajini Chandy anasema kupiga picha hizo ilikuwa ni kujifurahisha

Katika jamii ya Keralan, Bi. Chandy amekuwa wa kipekee.

Aliporejea Kerala mwaka 1995 baada ya kuwa Mumbai kwa miongo kadhaa ambapo mume wake alikuwa akifanyakazi na benki moja ya nje ya nchi, alifanya wengi kuumiza shingo zao pale alipotoka akiwa amevaa jeans yake. Anasema kuna wakati aliwahi kukemewa na watu kwasababu ya kuvaa blauzi ya mikono mifupi.

Miaka michache iliyopita, aligonga vichwa vya habari kwa uvaaji wake wa kisasa - mwaka 2016, akiwa na umri wa miaka 65, alianza kujitokeza kama muigizaji katika mchezo wa kuigiza wa vichekesho.

Tangu wakati huo ameonekana kwenye filamu nyingine mbili na pia ameshiriki katika sehemu ya pili ya kipindi cha 'Big Boss' mwaka jana.

Bi. Chandy anasema alishiriki mchezo wa kuigiza kuonesha watu wazima kwamba bado wanaweza kujiamini na kufurahia maisha yao.

"Wanandoa wengi wenye umri mdogo huwa wanatumia muda wao kulea familia. Huacha kufuatilia waliotamani na muda si muda wanajiona wamekuwa wazee kuanza kukimbizana na ndoto zao kwasababu wana wasiwasi hawajui jamii itawachukuliaje. Naamini kwamba ni sawa kufanya unachotaka almradi hakuna unayemdhuru," amesema

"Nimetimiza majukumu yangu yote ya kifamilia na kijamii na sasa ninafanya kile ambacho kinanipa furaha moyoni mwangu. Najifunza kupiga ngoma, sio kwamba ninataka kuwa mzoefu sana, lakini najifurahisha nafsi yangu."

Dhamira ya kupiga picha ilikuwa ni kujifurahisha tu.

"Disemba, Athira aliniuliza kama ningependa kupigwa picha na kama nilikuwa na kuzuizi chochote cha kuvaa nguo za nchi za magharibi. Nikasema, hapana. Nilikuwa nikizivaa wakati nikiwa kijana. Nikaongeza kwamba nina picha niliopiga nikiwa na nguo za kuogolea," Bi. Chandy amesema.

Rajini Chandy with photographer Athira Joy

Chanzo cha picha, Athira Joy

Maelezo ya picha, Mpiga picha Athira Joy anasema Rajini Chandy "anatia moyo" wanawake wengine

Alisema kwamba amependezwa na pendekezo lake kwasababu amekuwa akivutiwa na wazee waliovaa vizuri.

"Lakini nikamwambia kuwa nitafanya hivyo ikiwa mume wangu ataniruhusu. Kwahiyo akamuomba ruhusa na kusema: 'Ni maisha yake. Ikiwa anataka kufanya hivyo, mimi sina pingamizi."

Bi. Chandy anasema mara ya kwanza alipoona nguo ambazo Athira alikuwa amezichukua kwa kukodi katika duka la nguo lililo karibu, alishikwa na butwaa".

"Sikuwa nimewahi kuvaa nguo za kuvutia namna hiyo kwa kipindi kirefu. Lakini punde tu nilipozivaa nilikuwa sawa."

Bi.Chandy alipigwa picha 20 akiwa nyumbani kwake huko Kochi mwishoni mwa mwaka jana.

Watu wengi katika mitandao ya Facebook na Instagram wakaanza kuzisifia na vyombo vya habari vya eneo vikachukulia suala hilo kuanzia hapo.

Rajini Chandy

Chanzo cha picha, Athira Joy

Maelezo ya picha, Rajini Chandy anasema alipiga picha hizo kutia wazee moyo

Kulikuwa na maoni mengi ya kutia moyo - watu waliandika wakisema "umethibitisha kuwa umri ni nambari tu"; wengi walimuelezea kama "mkakamavu", "anayependeza", na "mzuri"; na wengine walizungumzia "kujiamini kwake"; na waliopendezwa zaidi na mavazi yake walimtumia ujumbe kwenye mtandao wa WhatsApp au kumpigia simu kumuambia kuwa "Shangazi umependeza".

Lakini muda si muda, akaanza kukosolewa.

"Mwingine aliniita kahaba. Mwingine akaniuliza, 'Yaani wewe bado hujafariki dunia?' Mwingine akapendekeza kaa nyumbani na usome bibilia. Huu ni umri wako wa kuomba, wala sio kuonesha mwili wako'. Huku mwingine akisema hata nikifanya nini, bado mimi ni mzee tu."

Rajini Chandy

Chanzo cha picha, Rajini Chandy

Maelezo ya picha, Rajini Chandy hivi karibuni aliweka picha yake ya kitambo akiwa amevaa nguo ya kuogelea na mmoja akamjibu 'unatatizo gani wewe katika huu umri wako'?

Kilichokasirisha watu ni picha mbili moja inamuonesha akiwa amevaa jeans inayombana na amejitanua. Na ya pili, ni ile ambayo amevaa nguo fupi.

"Mbaya zaidi ni kwamba inaonesha miguu yangu," anasema. "Lakini nina miguu mizuri, kwahiyo hilo halikuwa tatizo," anacheka.

Hata hivyo dakika kidogo baadaye, akakubali kuwa maoni hayo yana muumiza moyo.