Uvamizi wa Bunge Marekani: Wabunge wapiga kura ya kumshitaki rais Donald Trump

Baraza la wawakilishi nchini Marekani limepiga kura ya kumshitaki rais Donald Trump kwa kuchochea ghasia zilizosababisha uvamizi wa majengo ya bunge kwenye jumba la Capitol wiki iliyopita.
Wabunge 10 wa chama cha Republican walishirikiana na wenzao wa chama cha Democrat kupitisha kura hiyo ya kumshtaki rais kwa 232 dhidi ya wabunge 197 waliopinga hatua hiyo.
Ni rais wa kwanza katika historia ya Marekani kupigiwa kura hiyo mara mbili na baraza hilo la Congress.
Rais Trump ambaye ni mwanachama wa Republican sasa atakabiliwa na kesi katika Bunge la Seneti ambapo iwapo atapatikana na hatia huenda akapigwa marufuku kushikilia wadhifa wowote wa ofisi ya umma.
Bwana Trump ataachia rasmi madaraka tarehe 20 mwezi Januari kufuatia kushindwa kwake katika uchaguzi mkuu mwezi Novemba dhidi ya Joe Biden.
Bunge hilo linalodhibitiwa na wabunge wengi wa Democrat lilipiga kura siku ya Jumatano saa kadhaa baada ya mjadala mkali huku wanajeshi wakiimarisha usalama ndani na nje ya jumba la bunge.
Shirika la kijasusi nchini Marekani FBI limeonya kwamba kuna uwezekano wa kuzuka kwa maandamano katika majimbo yote 50 kabla ya kuapishwa kwa rais mteule Joe Biden wiki ijayo.

Katika kanda ya video iliyotolewa baada ya kura hiyo kupigwa, bwana Trump aliwataka wafuasi wake kuwa watulivu lakini hakuzungumzia juu ya kushtakiwa na bunge.
"Ghasia na uharibifu hauna nafasi katika taifa letu…hakuna mfuasi wangu ambaye angependelea kufanyika kwa ghasia za kisiasa."
Je Trump ameshtakiwa kwa makosa gani?
Trump ametuhumiwa na Congress kwa kuchochea ghasia zilizosababisha uvamizi wa bunge kufuatia hotuba yake aliyoitoa Januari 6 katika mkutano wa hadhara nje ya Ikulu ya White House.
Aliwataka wafuasi wake kuandamana kwa amani na uzalendo ili sauti zao zisikike, lakini pia kukabiliana na uchaguzi ambao alidai kwamba ulikumbwa na udanganyifu mkubwa.
Kufuatia matamshi hayo ya rais Trump , wafuasi wake walivunja kingo na kuingia bungeni na kuwalazimu wabunge kuahirisha kikao cha kuidhinisha ushindi wa rais mteule Joe Biden na baadaye kujificha.
Jumba hilo lilifungwa kwa muda na watu watano wakafariki wakati wa ghasia hizo.
Hati ya mashtaka dhidi ya bwana Trump aliyarejea mara kadhaa matamshi yake akidai kwamba matokeo ya uchaguzi huo wa urais yalikuwa yamekumbwa na udanganyifu na kwamba hayafai kukubaliwa.
Kwa mujibu wa mashtaka hayo, Trump aliyarejea matamshi hayo mara kadhaa na kutoa wito kwa wafuasi wake, hatua iliyowachochea na kusababisha ghasia bungeni na vifo.
Je wabunge walisema nini wakati wa mjadala?
Wabunge wa Congress walitoa taarifa zao wakiunga mkono na kupinga kura hiyo katika bunge hilo hilo ambapo walijificha chini ya viti na kuvalia barakoa wakati ambapo waaandamanaji walijaribu kuingia ndani wiki iliyopita.
Spika wa Bunge Nancy Pelosi kutoka Democrat alisema: ''rais wa Marekani alichochochea ghasia na uasi dhidi ya taifa letu. Lazima aondolewe. Yeye ni mtu hatari kwa taifa hili ambalo sote tunalipenda.''
Mbunge wa chama cha Democrat Julian Castro alimuita rais Trump "kama mtu hatari zaidi kuwahi kushikilia ofisi ya rais".












