Mzozo wa Tigray: Habari ghushi zinazoenezwa kuhusu mzozo Ethiopia

- Author, Na Peter Mwai
- Nafasi, BBC Reality Check
Tahadhari: Makala hii ina picha ambazo zinaweza kuwakera baadhi ya watu
Serikali ya Ethiopia inapoendelea na operesheni ya kijeshi katika jimbo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo, baadhi ya watu mtandaoni wametumia fursa hiyo kueneza habari ghushi.
Baadhi wanatumia picha au video ambazo hazina uhusiano wowote wa mzozo huo, ambapo baadhi zimehaririwwa kuzifanya zionekane za kuaminika zaidi.
Tumeangazia baadhi ya taarifa hizo.
Mfumo wa kujikinga dhidi ya makombora

Baadhi ya watu wamekuwa wakisambaza picha wanazosema zinaonyesha mfumo wa kujikinga dhidi ya makombora wa S-400 ambao hutengenezwa na Urusi.
Wanadai Tigray inamiliki mfumo huo na inautumia kujikinga dhidi ya mashambulizi ya ndege za kivita za Ethiopia.
Wanadai pia kwamba mfumo mwingine wa kisasa wa kurusha mizinga na roketi ambao pia hutumiwa kujikinga unatumika.
Ujumbe ulioambatanishwa na picha hizo unasema: "Silaha hizi unazoziona pichani, Ethiopia yenyewe haizimiliki kama taifa."
"Lakini watu wa Tigray wanautumia kujikinga dhidi ya mashambulizi ya kutoka angani."
Picha hizo zinaonyesha pia mwanajeshi anayeonekana kuwa na sare rasmi za vikosi maalum vya Tigray, akiwa amesimama hapo karibu.
Lakini picha hizo zimehaririwa, na wanajeshi hao kuongezwa.
Ukitazama kwa makini utagundua kwamba vivuli vya wanajeshi hao vinaelekea upande tofauti na vivuli vya vitu vingine kwenye picha, au vivuli hivyo vimekolea sana.
Katika moja ya picha, mwanajeshi aliyebandikwa hapo anaonekana kuwa mkubwa sana ukilinganisha na vitu vingine pichani.
Uchunguzi wa picha hizo mtandaoni umebaini kwamba picha hizo zimetoka kwa mazoezi ya kijeshi yaliyofanyika katika jimbo la Astrakhan, kusini mwa Urusi.
Video iliyochapishwa na mtandao wa lugha ya Kirusi iliyopakiwa mtandaoni Septemba, inaonyesha mfumo huo ukifanya kazi.
S-400 ni mfumo wa kisasa wa kujikinga dhidi ya makombora ambao ni mataifa machache sana duniani wanaumiliki.
Na Ethiopia si moja ya mataifa hayo.
"Ethiopia haijawahi kununua mfumo wa S-300 au S-400 ... wa kujikinga dhidi ya makombora, na mataifa yanayopakana na taifa hilo hayana pia," anasema Justin Bronk, kutoka Royal United Services Institute (Rusi), jijini London.
Ndege iliyodunguliwa si ya Ethiopia

Mamia ya watu kwenye Facebook wamekuwa wakisambaza picha ambayo inadaiwa kuonyesha ndege ya kivita ya jeshi la Ethiopia ikiwaka moto ardhini baada ya kudunguliwa.
Ujumbe mmoja unasema: "Vikosi maalum vya Tigray vilishambuliwa kutoka angani.
"Vimeharibu ndege moja ya kivita [ya Ethiopia] na kuwaua wanajeshi wengi maalum [makomando wa Ethiopia]."
"Mapigano bado yanaendelea."
Lakini baada ya uchunguzi wa picha mtandaoni tumebaini picha hiyo si ya kutoka Ethiopia.
Picha sawa na hiyo inapatikana:
- Katika taarifa ya Julai 2018 kwenye runinga ya Iran ya Press TV ambapo walizungumzia kuhusu ndege ya Saudia iliyodunguliwa na waasi wa Houthi, Yemen
- na katika ujumbe kwenye Twitter uliochapishwa Mei 2015 kuhusu ndege ya kivita aina ya MiG-25 iliyodunguliwa karibu na jiji la Zintan, Libya.
Picha ya ajali ya ndege ya Ethiopian Airlines

Baadhi wamekuwa wakieneza picha za ajali ya ndege ya abiria ya shirika la Ethiopian Airlines iliyoanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege Addis Ababa Machi mwaka jana. Watu zaidi ya 150 walifariki kwenye ajali hiyo iliyohusisha ndege aina ya Boeing 737 Max 8.
Picha moja inadai kwamba mifuko ya kubebea maiti inayoonekana kwenye eneo hilo ni karibu na eneo la Tigray na kwamba inaonyesha miili ya wanajeshi kutoka jimbo la Amhara waliouawa wakishambulia Tigray.
Lakini baadhi ya watu wameeleza kwa njia sahihi kwamba picha hizo hazihusiani na mapigano yanayoendelea.
Baadhi ya watu baadaye walifuta picha hizo.
Waziri wa Ethiopia hakuwahimiza wanajeshi wavalie barakoa

Picha za unaodaiwa kuwa ujumbe uliochapishwa kwenye na Waziri wa Afya Lia Tadesse zimekuwa pia zikisambaa, akionekana kubezwa kwa kutoa ushauri wa kuzuia kusambaa vya virusi vya corona kwa wanajeshi wanaopigana.
Ujumbe huo unasema: "Msikaribiane, mtumie vitakasa mikono na mvalie barakoa kwa njia sahihi, nawasihi nyote mnaohusika mchangie kukamilika kwa vita hivi kwa amani."
Lakini ujumbe huo umeghushiwa.
Ujumbe huo wa Twitter haupatikani kwenye ukurasa wa waziri huyo kwenye Twitter.
Ukutazama kwa makini machapisho ya waziri huyo kwenye Twitter utabaini pia kwamba huchapisha kwa kutumia simu aina ya iPhone - na sio simu ya Android kama inavyoonyeshwa kwenye ujumbe huo wa kughushiwa.













