Uchaguzi Tanzania 2020: Je umati wa watu hufuata nini kwenye mikutano ya kampeni?

Wafuasi wa CCM
    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

Watu sita tulikuwa tumekodoa macho kuangalia televisheni wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam Oktoba mwaka 2015.

Kulikuwa na umati mkubwa wa watu ambao pengine haujapata kuonekana katika miaka ya karibuni. Kulikuwa na nyuso mbili tatu za wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizokuwa zimefadhaishwa na picha zile.

Kwa bahati nzuri, miongoni mwa waliokuwa katika chumba kile alikuwa mmoja wa viongozi wa juu wa CCM wakati ule. Nadhani aliona fadhaa ile katika nyuso za watu na akatamka maneno haya; "Hapo hakuna kitu. Mwaka 1995, Augustine Mrema alikusanya watu 200,000 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja".

Alikuwa anamaanisha idadi sawa na mara nne ya Uwanja wa Benjamin Mkapa uliojaa watu. Wote katika eneo dogo kama Mnazi Mmoja. Nilisikia sauti ya watu wakipumua baada ya kauli ile ya kigogo wa CCM.

Fadhaa ile ya wana CCM walioona Edward Lowassa wa Chadema amejaza watu Jangwani, ndiyo fadhaa pia ambayo wana Chadema wanaipata wanapoona mikutano ya CCM imejaza watu pomoni.

Edward lowassa

Uzoefu hapa Tanzania na katika maeneo mengi duniani, unaonyesha kwamba kujaza watu wengi katika mikutano hakumaanishi ushindi kwa mgombea au kupendwa kwa mgombea. Kuna vitu vingi vinavyofanya watu wajae viwanjani.

Watu wanafuata nini kwenye mikutano?

Miaka michache iliyopita, chama cha siasa tajiri cha Kuomintang cha nchini Taiwan, kilishuhudia watu wakipungua kwenye mikutano yake ya hadhara.

Wakaja na mbinu ya kuvutia mashabiki kwenye mikutano yao. Wakatangaza kwamba chama kitatoa kiwango sawa na shilingi elfu tano ya Tanzania kwa kila atakayehudhuria mikutano yao.

Wafuasi wa CCM

Chanzo cha picha, Empics

Haikuchukua muda, mikutano ya chama hicho cha KMT, ikaanza kujaza watu pomoni. Fedha ikafanya kazi yake ipasavyo.

Hapa Tanzania, kivutio kikubwa cha watu huwa ni wanamuziki mashuhuri. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatumia wanamuziki karibu wote mashuhuri nchini kuvutia watu kwenye mikutano yake.

Wagombeaji urais Tanzania

  • Anawania awamu ya pili na ya mwisho madarakani.
  • Kampeni yake imejikita kati mafanikio yake kwenye sekta za madini, ujenzi wa miundombinu, elimu bure na mapambano dhidi ya rushwa.
  • Awamu yake ya kwanza pia imekosolewa kwa ukandamizaji wa haki za binadamu.
  • Ni mgombea wa chama tawala ambacho kipo madarakani toka uhuru, hivyo anatarajiwa kushinda uchaguzi huu.
  • Magufuli, 60, alichaguliwa Bungeni mara ya kwanza 1995 na kupata umaarufu akihudumu katika wizara ya ujenzi alipopata jina la utani la tingatinga.
  • Alimiminiwa risasi na wasiojulikana Setemba 2017, japo amenusurika shambulio hilo limemuacha na majeraha ya kudumu.
  • Alirejea Tanzania mwezi Julai 2020 baada ya miaka mitatu ya ughaibuni ili kugombea urais kupitia chama kikuu cha upinzani Chadema.
  • Kampeni yake imejikita kwenye kuheshimu haki za binadamu na kukuza uchumi wa watu.
  • Mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010 na 2015 na kuhudumu kama mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani.
  • Alituhumiwa ndani ya CCM kuwa alikuwa na mipango ya ‘kumhujumu’ Magufuli kwenye uchaguzi wa ndani ya chama 2020.
  • Sasa ni mgombea wa ACT, ambacho kimeweza kukua kutoka kuwa chama kidogo mpaka moja ya mihimili ya upinzani kwa kipindi kifupi.
  • Kachero mstaafu, alihudumu kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya rais mstaafu Jakaya Kikwete toka 2007 mpaka 2015.
  • Mwanasiasa mwandamizi wa upinzani ambaye amegombea urais katika chaguzi zote kasoro mwaka 2015.
  • Alikuwa kinara wa upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 na 2005.
  • Ushawishi wake ndani ya upinzani umepungua baada ya migogoro ya ndani ya CUF iliyolazimisha kundi hasimu kwake kujitoa chamani.
  • Profesa Lipumba ni moja ya wasomi maarufu wa uchumi nchini Tanzania ambapo alisoma shahada zake za juu kutoka chuo kikuu maarufu cha Stanford, Marekani.

Kwenye kampeni zilizopita za Uchaguzi Mkuu wa Marekani mwaka 2016, Hillary Clinton, alivutia watu 40,000 kwenye mkutano mmoja na ilikuwa idadi kubwa sana kwa Marekani.

Hata hivyo, pamoja na yeye kuwa mzungumzaji mkuu, alifanya juhudi za kuhakikisha mwanamuziki Jon Bon Jovi anapiga muziki wake siku hiyo.

Mikutano ya Yoweri Museveni na chama chake cha NRM inajulikana kwa kuchukua watu kutoka hadi mikoa mingine na kuwaleta alipo.

kampeni Uganda

Chanzo cha picha, Yoweri Museveni/Twitter

Kwa hiyo, wakati mwingine, idadi kubwa ya watu kwenye mikutano haina uhusiano na watu kukipenda chama au mgombea. Watu wanakuja kwa sababu kuna kitu kingine kinawavutia kuhudhuria mikutano na wala si siasa.

Wakati mwingine, kundi hili la wanaofuata mengine kwenye mikutano unakuta hata kura hawapigi. Si ajabu kwa wagombea wanaoonekana kujaza watu kushindwa kwenye uchaguzi kama maelfu ya wanaokuja, wanachotaka ni hela ya nauli, posho au kumuona Diamond na Ali Kiba jukwaani.

Ukosefu wa ajira

Tanzania ni taifa lenye vijana wengi. Mojawapo ya matatizo makubwa yaliyopo nchini sasa ni ukosefu wa ajira na waathirika namba moja ni vijana.

Mikutano ya hadhara inayoendelea sasa hutoa fursa kwa kundi hili la vijana kupata jambo la kuwapotezea muda. Wakati mwingine, wanakwenda kwa ajili ya kupata matumaini kutoka kwa wagombea kwamba mambo yatakuja kuwa mazuri zaidi huko mbeleni.

Hawa si lazima wawe wameelewa sera au wanamkubali mgombea. Hawa wanatafuta mahali pa kupotezea muda ili siku iishe. Si lazima wawe wapiga kura.

Upya wa mgombea huvutia watu

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba mgombea mpya anayefika mahali anaweza kuvutia watu zaidi kuliko yule aliyezoeleka.

CCM wamekuwa na utaratibu wa kubadilisha mgombea kila baada ya miaka 10. Chadema wamekuwa wakijitahidi kubadili wagombea kila unapoingia uchaguzi ili kuwe na mwendelezo.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Chadema kimemsimamisha Tundu Lissu ambaye mwaka 2017 alipigwa risasi na watu ambao hadi leo hawajulikani na kunusurika kifo.

Kwa hiyo, kwenye mikutano yake ya hadhara inayoendelea hapa nchini, wapo watu ambao shida yao ni kumwona mtu ambaye kweli 'amefufuka' kutoka katika wafu.

Kwa hiyo, kuna watu wanataka kumwona Lissu katika mwili na nyama ili waamini miujiza iliyotokea ya mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki.

Kundi hili likimuona tu mgombea huyo kwao inatosha. Si lazima waende kumpigia kura ya Urais ili ashinde na kuboresha maisha yao.

Tundu Lissu

Kama mgombea ni mpya na habari zake zimeanza kusikika, kuna watu ambao watakwenda kwenye mkutano kumsikiliza na kufanya uamuzi kama wampigie kura au la.

Katika kundi hili, wapo watakaoona anafaa na kuamua kumpigia kura na kuna watakaoona kwamba hafai na wakaamua kutompigia kura.

Jambo moja la muhimu kukumbuka hapa ni kwamba wote hawa walikuwa wamehudhuria mkutano wa hadhara wa mgombea.

Kwenye hili la mgombea mpya, linahusu pia mgombea anayeibuka na jambo lililozua mjadala. Katika uchaguzi wa mwaka huu, mgombea wa Chama cha Chauma, Hashim Rungwe, alianza kuvutia watu baada ya kutangaza kwamba atakuwa akigawa "ubwabwa" - chakula maarufu kwa Watanzania kwenye mikutano ya hadhara.

Mzee Rungwe alipata bahati mbaya ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumkataza kugawa chakula kwa madai kwamba ni rushwa lakini kama angeruhusiwa, ni wazi angepata mashabiki wengi.

Nguvu ya umati kwenye uchaguzi

Kama sasa inafahamika kuwa wingi wa watu kwenye mikutano ya hadhara haina maana kwamba mgombea atashinda, kwa nini wanasiasa wanang'ang'ania umati?

Utafiti uliofanywa miaka saba iliyopita na taasisi ya AEI ya Marekani, ulisema kwamba umuhimu wa umati kwenye siasa unatokana na ukweli kwamba wingi wa watu huwa na athari kwenye saikolojia ya mashabiki.

Mwanzoni mwa makala haya, nilieleza kuhusu tukio la mwaka 2015. Kama kigogo yule wa CCM asingetupa picha ya mwaka 1995, sisi wengine tulikuwa tumefadhaika.

John Pombe Magufuli

Wanachofanya wanasiasa wa Tanzania, hasa kuanzia mwaka 2015, ni kuhakikisha kwamba wapenzi na wanachama wao wanakuwa na hamasa ya kudumu na matumaini kwamba watashinda uchaguzi.

Si kila anayeangalia picha, na ujio wa mitandao ya kijamii umefanya picha zisambae kwa wingi zaidi, anajua waliofika walitumia njia gani na wametoka wapi.

Wakati Chama cha Wananchi (CUF), kikiwa katika ubora wake mwaka 2005, mikutano ya Tanzania Bara ilikuwa ikifanyika na chama kikitumia magari ya aina ya Fuso kutoa mashabiki sehemu za mbali kama Rufiji na kuwaleta Dar es Salaam.

Kwa hiyo, mchezo huu wa kusafirisha wahudhuriaji wa mikutano si mpya na hufanywa na vyama vyote; CCM na wapinzani.

Katika uchaguzi uliopita wa Uganda mwaka 2017, kuna tukio lilitokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kilolo. Kuna mzee alioneka akilia mara baada ya mkutano. Alipoulizwa ni kwa nini analia, alisema hajui atarudi vipi kwake na nauli hakuwa nayo.

Umati au Kura ya Maoni?

Mmoja wa wanasiasa mahiri wa Uganda, Aggrey Awori, anaamini kwamba wanasiasa wanatakiwa kuamini zaidi katika kupata taarifa kupitia kura za maoni kuliko wingi wa watu wa mikutanoni.

Kura ya maoni iliyofanywa kisayansi ina nafasi kubwa ya kukieleza chama na mgombea wake kuhusu matokeo na kinachoweza kutokea.

Bobi Wine

Lakini umati huu ambao tunauona na tutaendelea Tanzania ni kama upepo unaopita kwenye moto mkali.

Kama mkaa upo na moto wenyewe umeshawashwa tayari, moto utawaka vikali na kwa muda mrefu kadri ya wingi wa mkaa.

Umati mkubwa katika mikutano ya wagombea hausemi kila kitu kuhusu wapiga kura na siri walizonazo mioyoni mwao.

Unaweza pia kutazama:

Maelezo ya video, Uchaguzi wa Tanzania una umuhimu gani kwa nchi jirani?