Uchaguzi Tanzania 2020: Wanawake kuweka rekodi mpya mwaka huu?

- Author, Na Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
KUNA mchapo mmoja mashuhuri kuhusu wanawake na siasa za Tanzania. Ni hadithi inayohusu mazungumzo yaliyofanywa na Rais wa kwanza wa Tanzania, hayati Julius Nyerere, na mmoja wa wapigania Uhuru mashuhuri hapa nchini, hayati Bibi Titi Mohamed.
Mara baada ya Tanganyika kupata Uhuru wake mwaka 1961, Nyerere aliunda Baraza la Mawaziri la kwanza na hakukuwa na mwanamke hata mmoja aliyeteuliwa kuwa waziri kamili. Jambo hilo linadaiwa kumkera Titi.
Kwa ujasiri, Bibi Titi alimfuata Mwalimu Nyerere na kumhoji ni kwa vipi wanawake wamenyimwa nafasi ya kuwa mawaziri kamili na badala yake kupewa nafasi za unaibu waziri tu. Nyerere akamjibu kwamba amepata shida kupata wanawake "wenye sifa stahiki" kuteuliwa kuwa mawaziri.
Kwa mujibu wa mchapo huo, Titi alimuuliza Mwalimu swali moja tu; "Hao wanaume walio na sifa leo, walikuwa wapi wakati tukipigania Uhuru"?
Titi alikuwa mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya Uhuru. Kwa mujibu wa mwana historia wa mapambano ya kudai Uhuru wa Tanganyika, Mohamed Said, kuondoa Mwalimu, hakukuwa na mwanasiasa mwingine mashuhuri nchini kumzidi Titi Mohamed.
Yeye ndiye aliunganisha wanawake na Watanganyika kwa ujumla kwenye mapambano ya kudai Uhuru na mara zote akipanda jukwaani kabla ya Mwalimu Nyerere kuzungumza kwenye mikutano ya hadhara.
Uamuzi wa Mwalimu kuunda baraza la mawaziri lenye wanaume watupu ilikuwa kama kuwachoma kisu cha mgongoni wanawake na huo ukawa mwanzo wa upendeleo dhidi ya mfumo dume katika Tanganyika (Tanzania) huru.
Viti Maalumu
Baada ya uamuzi huo wa Mwalimu wa mwaka 1961, ilichukua miongo miwili kwa Tanzania kuweza kupata mbunge wake wa kwanza wa kuchaguliwa. Kwa miaka yote ya 1960 na 1970, wabunge wote wanawake waliokuwa bungeni waliingia kwa utaratibu wa viti maalumu.
Katika kesi maarufu ya Martha Wejja dhidi ya Kitwana Kondo kwenye miaka ya 1980, mwanamama huyo alishinda kesi baada ya kuthibitisha kuhusu maneno ya kejeli na udhalilishaji yaliyofanywa dhidi yake na mshindani wake kwa sababu ya jinsia yake.
Baada ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yaliyotokea mwanzoni mwa miaka ya 1990 -ukijumuisha na Mkutano wa Beijing kuhusu uwezeshaji wa wanawake, taratibu kibao kilianza kugeuka.

Chanzo cha picha, AP
Kwanza, kuruhusiwa mfumo wa vyama vingi kulimaanisha kutanuka kwa wigo wa wanawake kuwania nafasi za uongozi kupitia vyama vingine vya kisiasa.
Zaidi ya chama tawala cha CCM, wanawake sasa waliweza kujitokeza kuwania nafasi katika vyama vya upinzani na kupata fursa ambazo zisingekuwa rahisi kuzipata katika mfumo wa chama kimoja.
Kuruhusiwa kwa asasi za kiraia pia kulifungua njia kwa wanawake kuonyesha uwezo, maono na ujasiri wao kwenye kuhoji na kuishauri serikali kwenye mambo ya maslahi kwa taifa.
Wanawake mashuhuri wa miaka ya 1990 kama vile Leila Sheikh Khatib, Dk. Ananilea Nkya, Mary Rusimbi, Marie Shaba na wengine walipata umaarufu na heshima si kwa kutumia vyama vya siasa bali zaidi kupitia harakati zao kupitia asasi za kiraia.
Kama kuna jambo walilofanikiwa kulifanya wakati ule ilikuwan kuonyesha kwamba wanawake wanaweza kuwa viongozi pasipo kuwa wanasiasa kamili.
Matokeo yake ni kwamba mwaka 2010, Tanzania iliweza kupata wanawake wabunge 23 waliopata nafasi zao kupitia majimbo ya uchaguzi. Ukijumuisha na wale wa viti maalumu, Bunge la Tanzania likafikisha asilimia 29 ya wabunge wanawake -kiwango cha juu kabisa kwa wakati huo.
Mwaka jana, idadi ya wabunge wanawake ilikuwa imefikia kiwango cha asilimia 37; kikubwa katika historia ya Tanzania tangu Uhuru. Ni wazi kwamba kila wakati takwimu zinazidi kuwa za kuvutia kwa wanawake.

Uchumi
Kuongezeka kwa nafasi za wanawake bungeni kunaenda sambamba na kuimarika kiuchumi kwa wanawake wa Kitanzania. Takribani wanawake wote wanaowania ubunge na kushinda, ni wanawake ambao wana uwezo mzuri kifedha.
Halima Mdee alikwenda kuwania ubunge na kushinda Kawe mwaka 2010 baada ya kuwa amehudumu kama mbunge wa viti maalumu kwa kipindi kimoja. Wabunge wengine maarufu wanawake kama Jenister Mhagama, Stella Manyanya, Esther Bulaya, Esther Matiko na wengine walienda kuwania majimboni baada ya kuwa kwanza wamewahi kuwa wabunge wa viti maalumu.
Hata katika uchaguzi wa mwaka huu, wabunge kama Ummy Mwalimu, Grace Kiwelu, Sofia Mwakagenda, Angellah Kairuki, Upendo Peneza, Anatropia Theonest na wengineo wameenda kujaribu bahati ya kupitishwa na vyama vyao kuwania ubunge kupitia majimbo ya uchaguzi baada ya kuhudumu kama wabunge wa viti maalumu.
Kwa maana hiyo, kwa kadri wanawake wanavyokuwa na hali ngumu kiuchumi, ndivyo hivyo hivyo uwezekano wa wao kuchaguliwa kuwa wabunge unakuwa mdogo. Idadi ndogo ya wanawake bungeni katika miaka ya nyuma, iliakisi pia hali ngumu ya uchumi ya wanawake hapa nchini.
Kama uchumi wa Tanzania unatoa fursa za kiuchumi zilizo sawa kwa wanawake na wanaume, uwezekano wa ushindani wa haki baina ya jinsia hizi mbili ni mkubwa kuliko kama jinsi moja ikiwa na ukiritimba wa kiuchumi.
Mitandao ya kijamii inasawazisha hali
Katika miaka ya karibuni, mitandao ya kijamii nayo imekuwa ulingo wa muhimu kwa wanawake kueleza hisia zao na kuonyesha uongozi.
Huko nyuma, wanawake walihitaji kuwa wabunge au mawaziri, waandishi wa habari - kama ilivyokuwa kwa akina Leyla na Ananilea huko nyuma, wajumbe wa Halmashauri Kuu au Kamati Kuu za vyama au wamilikiwa vyombo vya habari ili kupata jukwaa la kuelezea mawazo yao kuhusu mambo anuai.
Hili limebadilika katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. Kwa sasa, mwanadamu yeyote - mwanamke katika muktadha wa makala haya, anaweza kutoa maoni na kuchangia mjadala muhimu ili mradi awe na simu ya mkononi au kompyuta yenye mtandao wa internet. Kwa sasa, kuna wanawake ambao hawana nafasi zozote za uongozi lakini maoni yao yanasikilizwa kwa uzito unaostahili.

Katika muktadha wa Tanzania, kuna majina ya wanawake kama Maria Sarungi, Fatma Karume, Mwanahamisi Singano na wengine ambao sasa watu wanachukulia kwa uzito mkubwa mambo wanayoweka katika mitandao ya kijamii.
Na hili si jambo la Tanzania pekee. Katika nchi za Sudan na Belarus, wanawake waliojipatia umaarufu kupitia mitandao ya kijamii wamefanikiwa kuchangia katika kubadili serikali au kutoa shinikizo kwa serikali kandamizi ambazo wanaume wengi wanaogopa kuzikosoa hadharani.
Wanawake na uchaguzi 2020
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, wanawake wamejitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za kuchaguliwa kuanzia Urais, ubunge na udiwani.
Chama cha upinzani cha ADC kimempitisha mwanamama Queen Sendiga kuwa mgombea wake wa nafasi ya urais katika uchaguzi huo.
Chama kikuu cha upinzani kimetangaza orodha ya wagombea wake wa ubunge ambako takribani wanawake 35 wamejitokeza kwenda majimboni kuwania ubunge. Idadi hiyo ni zaidi kidogo ya asilimia 20 na ndiyo kiwango kikubwa cha wagombea wanawake kupitishwa na chama hicho kuwania ubunge tangu kuanzishwa kwake.
Tofauti na vyama vingine vya upinzani, idadi kubwa ya wagombea hao wanawake wa Chadema ni wanasiasa mashuhuri waliowahi kuwa wabunge wa viti maalumu na majimbo; wakiwa na uzoefu na fedha za kufanyia kampeni.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, chama kinahitaji kupata walau asilimia tano ya kura kuweza kujihakikishia kupata wabunge wa viti maalumu na kwa idadi hii ya wagombea, Chadema inaweza kuvuna kura nyingi majimboni kupitia wanawake hawa.

Chanzo cha picha, Halima Mdee
Kufaulu au kutofaulu kwao katika uchaguzi wa mwaka huu kunategemea vitu vingi; vilivyo ndani ya uwezo wao na vilivyo nje ya uwezo wao.
Endapo uchaguzi utaendeshwa katika mazingira ya haki, wanawake hawa wa Tanzania wana nafasi sawa na katika maeneo mengine, na baadhi wanawazidi kwa mbali washindani wao wanaume.
Na hakuna tena hapa Tanzania mtu anayeweza kuwatazama usoni wabunge kama Halima Mdee, Esther Matiko na Bulaya na kuwaambia hawana sifa kama walizonazo wanaume wanaoshindana nao - kama Mwalimu alivyomwambia Titi takribani miaka 60 iliyopita.
Jibu lao litakuwa moja; hao wenye sifa walikuwa wapi wakati wao wakipambana?












