Tundu Lissu: Nini maana ya kurejea kwake Tanzania?

Na Ezekiel Kamwaga

Tundu Lissu

Imesadifu kwamba mwanasiasa mashuhuri wa Tanzania, Tundu Antipas Lissu, anarejea kufufua maisha yake ya kisiasa nchini kwake katika wakati wa msiba wa kiongozi aliyemfanya afahamike kwa Watanzania wote.

Uhusiano wa hayati Benjamin Mkapa; Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Tanzania na Lissu unaanza takribani miongo miwili iliyopita mwanasheria huyo akiwa mwanaharakati machachari anayepinga sera mbovu za madini za utawala huo.

Lissu alijipatia umaarufu mkubwa baada ya kuwa mtetezi wa haki za wachimbaji wadogo na wananchi wanaoishi katika maeneo ambako kampuni kubwa za uchimbaji madini zilikuwa zimepewa leseni za uchimbaji kutokana na mabadiliko ya kisera yaliyofanywa na utawala wa Mkapa.

Kilele chake kilikuwa ni suala la mgodi wa Bulyanhulu ambako Lissu na wanaharakati wengine walidai kuwa kulikuwa na wachimbaji wadogo waliofukiwa ardhini ili kupisha uchimbaji wa kampuni kubwa kutoka nje.

Leo hii, Benjamin Mkapa ametangulia mbele ya haki baada ya kifo chake cha ghafla Julai 23 mwaka huu. Kwa upande wake, Lissu amekanyaga ardhi ya Tanzania kwa mara ya kwanza baada ya takribani miaka mitatu kutokana na shambulizi dhidi yake.

Hakuna aliyetarajia kwamba Lissu atakuwa hai baada ya shambulio lile la Septemba 07, 2017 jijini Dodoma lililofanywa na watu ambao hadi leo hawajajulikana. Gari lake lilishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na kama kuna mtu anaweza kujisifu kwamba ana maisha mengi kuzidi paka, basi mtu huyo ni Lissu.

Lissu mpambanaji

Jambo moja ambalo utalipata kuhusu Tundu Lissu kutoka kwa watu wake wa karibu ni kwamba ni mtu ambaye siku zote hakuwahi kuwa mpole au mwenye kufanya mambo yake kimyakimya.

Baadhi ya wafuasi wa chama cha upinzani Chadema waliomlaki bwana Lissu

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Baadhi ya wafuasi wa chama cha upinzani Chadema waliomlaki bwana Lissu

Hadithi za matukio yake akiwa mwanafunzi katika shule za Ilboru (shule ya wanafunzi wenye vipaji maalumu kiakili) na baadaye Umbwe, zinamuelezea kama mwanafunzi mtundu, mahiri katika mijadala na ambaye uwezo wake kitaaluma darasani haukuwahi kutetereka kutokana na matukio yake mengi ya nje ya madarasa.

Lissu ana nguvu kubwa mbili za kuzaliwa ambazo hakuna shule inayoweza kumfundisha mtu; ujasiri na umahiri wa kuzungumza. Kwa Lissu, vyote viwili amejaliwa kuwa navyo tangu utotoni na katika maisha yake ya utu uzima -kama mwanaharakati na mwanasiasa, amevitumia vitu hivyo kwa ufanisi mkubwa.

Ni ujasiri wake ndiyo uliompa umaarufu kwa kupambana kama mwanaharakati dhidi ya vyombo vya dola vya utawala wa Mkapa vilivyomweka jela, kumpiga na kujaribu kumnyamazisha kwa mbinu 2 tofauti.

Ni ujasiri wake ndiyo uliompambanua na wanasiasa wengine katika miaka ya mwanzo ya utawala wa Rais John Magufuli. Watanzania, kwa ujumla, ni wenye woga dhidi ya mamlaka na yeye alijipambanua kwa kuikosoa serikali hadharani; hata katika wakati ilipoonekana ni hatari kufanya hivyo.

Tofauti kubwa; baina ya Lissu na wanasiasa wengine ilikuwa kwenye uwezo wake wa kujieleza. Mbunge huyu wa zamani wa Singida Mashariki ana uwezo wa kujenga hoja na kuzieleza vizuri - kipaji kilichoungwa tangu enzi zake akiwa mwanafunzi wa Ilboru.

Wakati anachaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) miaka mine iliyopita, ilikuwa wazi kwamba wanasheria wa Tanzania walikuwa wanatafuta mtu ambaye angeweza kuiambia ukweli serikali waziwazi pasipo kuogopa.

Urais wake TLS ulikatishwa ghafla na tukio lile la Dodoma. Nchini Tanzania kuna matukio mawili ambayo watu wazima wengi hukumbuka walikuwa wapi wakati yakitokea; siku alipofariki Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999 na siku Lissu alipopigwa risasi mwaka 2019.

Kwa wachambuzi wengi wa Tanzania, tukio lile lilikuwa mojawapo ya siku za huzuni zaidi katika historia ya Tanzania.

Nini maana ya kurejea kwa Lissu?

Lissu anarejea Tanzania miezi michache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Chama chake cha Chadema kinakutana mwanzoni mwa mwezi ujao kuchagua mgombea wake wa urais katika uchaguzi huo.

wafuasi wa Lissu wakisherehekea kurudi kwake Tanzania

Tayari wagombea watatu wa Chadema wamepitishwa kwa ajili ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa chama hicho ili kupata mgombea mmoja. Wagombea hao ni Lazaro Nyalandu, Mayrose Majinge na Lissu.

Inajulikana kwamba Lissu ndiye mgombea wa upinzani anayeonekana kuungwa mkono na wananchi wengi kuliko wengine. Utafiti uliofanywa kupitia mtandao wa twitter na mwanazuoni wa Kitanzania, Dk. Chambi Chachage, wiki iliyopita, ulionesha kwamba kama uchaguzi ungefanyika sasa, Lissu angeweza kupata kura mara mbili ya zile ambazo angepata Magufuli au Benard Membe, aliyechukua fomu kuwania urais kupitia Chama cha ACT Wazalendo.

Chadema pia ndiyo chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania na kwa vyovyote vile; mgombea kutoka chama hicho ana nafasi ya kufanya vizuri kuliko chama kingine - kama vigezo vingine vyote vitabaki kama vilivyo.

Mmoja wa viongozi wa juu wa ACT Wazalendo aliyezungumza nami kwa masharti ya kutotajwa majina yake aliniambia kwamba hata chama hicho kingependa Lissu awe mgombea; endapo kutakuwa na makubaliano mengine kuhusu namna vyama hivyo vinavyoweza kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Katika siasa za vyama vingi kuna sifa kadhaa ambazo mgombea wa upinzani anatakiwa kuwa nazo; kujulikana, kuwa na hadithi, umahiri jukwaani na kukubalika na kundi kubwa la wapiga kura.

Lissu ni mashuhuri hadi vijijini hasa baada ya tukio la Septemba 07, 2017, tukio lake limetengeneza hadithi ambayo watu wanaifahamu na anakubalika na vijana; ambao ni zaidi ya nusu ya wapiga kura wote na anajua nini cha kuzungumza anapokamata kipaza sauti mkononi.

Kwa upinzani wa Tanzania na katika mazingira ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu; Lissu ni dhahabu.

Vikwazo

Wapo watu waliodhani kwamba huenda Lissu asingerejea Tanzania kufuatia tishio lililofanywa dhidi ya maisha miaka mitatu iliyopita. Hadi wakati naandika makala haya, saa chache kabla hajarejea nyumbani, wapo wanaoamini kwamba huenda atakamatwa kwa sababu zozote mara atakaporejea.

Mmoja wa viongozi waandamizi wa Chadema ameniambia kwamba tishio pekee walilonalo kuhusu Lissu ni wanahisi serikali inaweza ikafanya lolote kuhakikisha hawi mgombea wa upinzani.

" Baada ya yote tuliyoshuhudia, hatuna sababu ya kuamini kwamba serikali hii itamuacha Lissu azunguke nchi nzima kwa muda wa takribani siku 60 kuomba kura. Wanajua athari za kuruhusu hilo.

" Kumbuka, hii ni serikali ambayo iliendesha uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 pasipo vyama vya upinzani na wala haikuona tatizo. Mtazamo wetu ni kwamba serikali hii inatamani pia kushinda uchaguzi huu wa Oktoba bila kutoka jasho. Hilo haliwezi kutokea katika mgombea wa Chadema ni Lissu. Ndiyo hofu pekee iliyopo," alisema kiongozi huyo.

Kikwazo kingine kwa Lissu kinatoka ndani ya chama chake chenyewe. Kwa asili, Chadema ni chama kilichojiegemeza katika itikadi ya kibepari na mgombea ambaye anabeba msingi huo vizuri ni Nyalandu. Lissu anajulikana kama muumini wa Ujamaa na harakati.

Kundi hili linaundwa na wanachama wenye nguvu ndani ya chama hicho na linaamini kuwa Lissu si aina ya mgombea ambaye Chadema inataka kuwa naye na linatamani bendera hiyo ibebwe na Nyalandu ambaye mawazo na matendo yake yanaendana na mtazamo huo.

Kikwazo kingine cha tatu kwa Lissu kinahusu ushirikiano wa upinzani. Viongozi wa ACT Wazalendo kuanzia Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe, Membe na Mwenyekiti wake, Maalim Seif, wamezungumza mara kwa mara -hadharani, kwamba wako tayari kwa ushirikiano na Chadema.

Pasi na shaka, ushirikiano huo utajengwa katika msingi wa nipe nikupe; kuna mambo ACT itataka kutoka Chadema kama sharti la kumuunga mkono Lissu. Je, Chadema itakubali masharti ya ACT ili wamuunge mkono Lissu endapo atapitishwa na Chadema?

Baadhi ya viongozi wa upinzani waliowasili kumlaki Tundu Lissu

Pamoja na nguvu yote ya kisiasa aliyonayo Lissu, pasipo ushirikiano na ACT Wazalendo, nguvu ya upinzani itagawanyika na wagombea wa CCM katika ngazi zote watashinda kwa sababu ya mgawanyiko wa upinzani.

Ili mpambano uwe wa kufa au kupona; Tundu Antipas Lissu ni lazima akae ulingoni yeye na John Pombe Magufuli peke yao.

Kwa hiyo, kuondoa kikwazo cha dola; Tundu Lissu ana mitihani miwili ya kuvuka - kushawishi vigogo wa Chadema kwamba atatekeleza sera na maslahi ya chama hivyo ipasavyo na namna atakavyochanga karata zake na wenzake wa ACT.

Bahati nzuri pekee ambayo Lissu anayo ni kwamba ana uhusiano mzuri binafsi kati yake na takribani viongozi wa juu wa ACT Wazalendo. Miaka miwili iliyopita, ndiyo kwanza waliokuwa viongozi wa CUF wakihamia ACT; mmoja wa viongozi waandamizi alinieleza kuwa kwao mgombea wa kipekee wa urais wa Tanzania ni Tundu Lissu.

CCM na Lissu

Tundu Lissu

Tatizo kubwa kwa chama tawala CCM dhidi ya Lissu ni kwamba tangu awali, Serikali, Bunge na vyombo vya dola kwa ujumla, vilishindwa kulishughulikia suala lake vizuri - kimawasiliano na kimkakati.

Hadi leo, hakuna mtu aliyekamatwa wala kufikishwa katika vyombo vya sheria kuhusiana na tukio hilo. Badala yake, Lissu alifutwa ubunge na kwa ujumla, ukiondoa Samia Suluhu Hassan, viongozi wa CCM na serikali hawakwenda hata kumtembelea; jambo lisilo la kawaida katika desturi na tamaduni za Kitanzania.

Kugombea kwa Lissu maana yake ni kwamba CCM itafanya kazi ya kujitetea katika muda wote wa kampeni na kuna hofu ya kutoneshwa na kuibua upya maumivu yaliyosababishwa na tukio la Septemba 07, 2017.

Na kama kuna mtu wa kutumia fursa hiyo vizuri, mtu huyo ni Tundu Antipas Lissu.