Tundu Lissu aomba msaada kwa mawakili wa kimataifa kuhusu haki zake

Mwansiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu kwa sasa anazungumza na mawakili wa kimataifa ili kupigania kile alichokielezea kama haki zake kabla ya kurudi nyumbani, limeripoti gazeti la The Citizen nchini Tanzania
Bwana Lissu, ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu alipigwa risasi mara nyingi mjini Dodoma yapata miaka miwili iliyopita , na sasa anapanga kurejea nyumbani.
Septemba 7, 2017, Bwana Lissu alishambuliwa kwa silaha na watu wasiojulikana nje ya makazi yake Dodoma.
"Nilipigwa risasi ndani ya makazi rasmi ya serikali kwasababu nilikuwa nahudhuria viako vya bunge. Lakini hakuna uchunguzi wa maana uliofanyika hadi sasa. Nilinyimwa matibabu nje ya nchi kama mbunge. Nilinyang'anywa kiti changu cha ubunge na bado mahakama zilininyima haki ya kuwasilisha kesi mahakamani ,"alieleza Bwana Lissu nakuongeza kuwa mawakili wataangalia jinsi hili linalindwa na sheria za kimataifa.

Kulingana na The Citizen Lissu, amewasiliana na kampuni ya sheria ya Amsterdam & Partners LLP - ambayo ni kampuni ya sheria iliyosajiriwa kimataifa inayojishugulisha na masuala hayo na yenye uwakilishi katika mataifa mbali mbali duniani.
Kama sehemu ya suala hili, Amsterdam & Partners LLP wataangalia hatua za kisheria katika sheria za kimataifa kubaini haki za Bwana Lissu za kimataifa na kuwashinikiza maafisa wa taifa wanaodaiwa kuhusika katika ukiukaji wa sheria.
"Tunatuma ujumbe wa wazi kabisa - kutakuwa na athari kwa ukiukaji wa maadili ," Bwana Lissu anaripotiwa kuwaonya maafisa wa ngazi ya juu wa serikali.
Hivi karibuni kampuni hiyo ya mawakili iliwawakilisha Robert Kyagulanyi (Bobi Wine),mbunge wa upinzani wa Uganda pamoja na rais wa zamani wa Zambia, Bwana Rupiah Banda, serikali ya jimbo la Kaduna (Nigeria), Bwana Nasir El-Rufai, na gavana wa zamani wa Akwa Ibom (nigeria), Bwana Godswill Akpabio.
"Kuna viongozi wachache sana siku hizi wanaoonyesha ujasiri na maadili dhidi ya wanapokabiliwa na hali isiyoridhisha. Kwa hiyo tunajivunia kufanya kazi na Tundu Lissu kusaidia kutoa uelewa wa hali yake na kampeni ya ukiukaji wa sheria kuzuwia haki na uhuru wa kisiasa uliopo sasa nchini Tanzania," alisema Bwana Robert Amsterdam, muasisi mwenza wa kampuni ya Amsterdam & Partners LLP.

Chanzo cha picha, BUNGE TANZANIA
Mwezi uliopita Mahakama Kuu nchini Tanzania ilikataa maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema,Tundu Lissu kuhusu kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliofuta ubunge.
Mahakama kuu ilisema mwanasheria mkuu huyo wa Chadema hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo.
Akisoma uamuzi huo wa mahakama, Jaji Sirillius Matupa alisema kama maombi yake yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja.
Lissu alifungua maombi chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai ambaye amempa mamlaka ya kisheria kumuwakilisha, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.
Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu aliomba kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika ya kukoma kwa ubunge wake.
Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu alitangaza kupinga kupinga mahakamani uamuzi wa kumuondolea sifa ya ubunge kwa kile alichodai kuwa ni kinyume cha sheria.
Katika waraka wa salamu alizozitoa kwa marafiki zake, Lissu alisema tangu alipopoteza ubunge, "sijasema maneno mengi sana, zaidi ya kusema kwamba tutaenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo."













