Uchaguzi wa Tanzania 2020: Je nini kimewaangusha 'waunga mkono juhudi za Rais Magufuli' CCM?

Rais John Magufuli
Maelezo ya picha, Rais wa Tanzania John Magufuli
    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi wa Siasa Tanzania.

Katika siasa za Tanzania msemo huu 'waungaji mkono juhudi' umekuwa maarufu katika miaka mitatu iliyopita.

Ni msemo ambao hulenga kuwazungumzia wale wanasiasa waliokuwa upinzani wakahama vyama vyao na kwenda Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa madai ya kwenda kuunga mkono juhudi za maendeleo za Rais John Pombe Magufuli.

Wapinzani wanawatuhumu kwamba walijiunga na CCM baada ya kununuliwa, ingawa wenyewe wanaipinga tuhuma hiyo kwa nguvu zao zote. Hata viongozi wa chama walichohamia nao wanapinga madai ya kununua wanasiasa wa upinzani.

Siasa za kuhama chama zilishika kasi katika awamu hii inayomaliza.Wabunge, madiwani na hata wafuasi wa kawaida kutoka vyama vikubwa vya upinzani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) walihama kwa wingi sana.

Hadi mwezi Agosti 2018 jumla ya madiwani na Wabunge wapatao 138 walijiuzulu nafasi zao na kwenda chama tawala.

Kwa upande wa kundi la Wabunge hadi mwezi Februari mwaka huu Wabunge 12 walikuwa tayari wamehamia CCM kwenda kuunga mkono juhudi.

Kuelekea uchaguzi mkuu wanasiasa hao wameingia katika kinyang'anyiro cha kutangaza nia na kuchukua fomu kwa tiketi ya CCM. Bahati mbaya wengi wao wameangukia pua, kwa maneno mengine wameshindwa kufua dafu katika kura za maoni za chama hicho.

Ni wazi kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba ndio kilele cha maamuzi kuhusu nani atabaki na yupi atakwenda katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mintarafu hiyo kukosa kupita katika kura za maoni ni dalili kuwa ndoto yao yakuelekea Dodoma inazidi kuwa ya Alinacha.

Mambo yalikuwaje majimboni?

Kwanza tuiangalie hali jumla katika mchakato wa kura za maoni za mara hii ndani ya CCM katika ngazi ya Ubunge.

Chama hicho kikongwe barani Afrika, kimeandika historia ya kupokeawachukua fomu wengi mno, ni zaidi ya chaguzi zilizopita. Kwa nafasi hiyo pekee wachukua fomu walifikia 10367.

Wanachama wa CCM

Katika ngazi nyengine ikiwemo udiwani na uwakilishi kwa upande wa Zanzibar utitiri wa watu ulikuwa mkubwa vile vile. Ilikuwa'mpata mpatae'.

Hata watu ambao hawana uzoefu na siasa wala hawajawahi kuonekana katika medani za kisiasa mwaka huu ulikuwa ni wao. Nao walikuwa ni miongoni mwa waliotangaza nia.

Kulikuwa na vichekesho vikubwa katika mchakato hasa pale wachukua fomuwalipokuwa wakitangaza sera na kuomba kura. Baadhi ya sera zilizohubiriwa ziliwafanya Watanzania kuangua vicheko au kubaki midomo wazi kwa mshangao.

Yote tisa, lililokuwa bora katika kinyang'anyiro hicho ni ule uwazi wakati wa kuhesabiwa kura kama alivyoagiza Mwenyekiti wa chama, Rais John Pombe Magufuli.

UCHAGUZI
UCHAGUZI

Kura nyengine zilihesabiwa mubashara kupitia vituo vya runinga ama mitandao ya kijamii. Kwa ufupi kila mchukua fomu alivuna haki yake, hata kama ni kura sifuri.

Wapo walioamini wangebebwa na umashuhuri wao kupitia mitandao ya kijamii, wengine wakiamini kuhama kwao na kutangaza utiifu kwa CCM kungewasaidia kuteleza hadi Dodoma. Lakini mambo yameenda nje ya matarajio ya wengi wao.

Kipi kimewaagusha?

Mchakato wa kusaka kura za maoni ili uwakilishe chama chako daima zinahitaji mizizi na ushawishi katika chama hicho. Watangaza nia waliohama upinzani na kwenda chama tawalahawakuwa na mizizi ya muda mrefu katika CCM. Na hilo ndilo rungu lililowaadhibu, wakaambulia kura chache.

Ule mpango wa kuteuliwa na kupitishwa bila kupingwa walipokuwa wanagombea tena nyadhifa zao kupitia CCM baada ya kuhama vyama vyao vya upinzani, haukuwepo wakati wa kura za maoni. Kila mtangaza nia alipambana kwa nguvu zake na ushawishi alionao mbele ya wajumbe.

Mchakato wa kupita bila kupingwa uliowapitisha waungaji mkono juhudi ulifanyika makusudi kwa maslahi ya kisiasa. Ilikuwa ni moja ya mbinu ya kuwavuta viongozi wengine wa upinzani wajiunge na CCM pindi watakapoona njia isiyo na vigingi ya kurudi tena Bungeni kupitia chama hicho.

Muungaji mkono juhudi anapofika hatua ya kukosa nafasi kupitia CCM na hana uwezo wala nafasi ya kurudi kule upinzani alikotoka, kilichobaki ni kusubiri huruma ya Rais atakaye chaguliwa ikiwa atamteuwa katika viti maalum vya Ubunge au nyadhifa nyegine ya kiserikali. Lakini akikosa hayo yote hapo huanza kufutika polepole katika ramani ya kisiasa.

UCHAGUZI

Lipo swali la kisiasa linalohoji kuhusu mwanasiasa anayehama chama chake cha upinzani kwenda chama tawala kuunga mkono juhudi za Rais.

Je, ikifika wakati ule upinzani unashika dola na kuongoza nchi, atahama tena kurudi chama cha zamani kwa minajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo za Rais mpya?

Swali hilo ndilo linalowatia shaka wapiga kura si tu wale wanaopiga kura za maoni na hata wapiga kura katika uchaguzi mkuu, ikiwa wanasiasa wa aina hiyo ni wa kuaminika kupewa nafasi ya kwenda kuwawakilisha katika ngazi za kiuongozi.

Baadhi ya vigogo wa kisiasa walioanguka katika mchakato huu wa awali ni David Silinde aliyepata kura 18 katika jimbo la Tunduma. Maulid Mtulia aliyekuwa mbunge Kinondoni,aliambulia kura 11 kati ya 403.

Majina mengine makubwa yaliyokuwa katika siasa za upinzani ni Abdallah Mtolea, aliyekuwa Mbunge Temeke, Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki na Dk Vicent Mashinji, kuwataja wachache.

Dk Mashinji alikuwa Katibu Mkuu wa Chadema, amevunja rikodi miongoni mwa waungaji mkono juhudi kwa kuambulia kura mbili katika jimbo la Kawe.

Dk Godwin Mollel jimbo la Siha na Mwita Waitara jimbo la Tarimo Vijijini ndio waunga mkono juhudi ambao wameongoza katika kura za maoni kwenye majimbo yao.

Maelezo ya video, Zitto aeleza makosa yaliyofanywa na muungano wa UKAWA katika uchaguzi uliopita

Siasa hazitabiriki lakini anguko hili linatoa sababu ya kuamini siasa za kuhamahama zilizoshika kasi kati ya 2016 hadi 2020 huenda zitapungua au kuondoka kabisa kwa miaka kadhaa ijayo. Hesabu za wahamaji ilikuwa ni kamari ya kisiasa ambayo wengi wao wameambulia kuliwa.

Mchakato huo ni wa awali, kuanzia tarehe 30 Julai CCM itakuwa na vikao vya kamati za siasa za majimbo kwa ajili kuwajadili wagombea na kufanya mapendekezo kwa kamati za siasa za mikoa.

Historia inaonesha baadhi ya wagombea hukatwa, ingawa ni wa chache lakini mara hii mchakato huu umekuja na uwazi zaidi, bado ni kusubiri kuona uwazi huo utakuwa na maana gani itakapofika hatua ya mwisho ya wagombea kupitishwa.