Ni kwanini Wanigeria hawa waliamua kufunga ndoa mtandaoni?

Chanzo cha picha, COURTESY OF THE COUPLE
Ayokunle Sulaiman na mchumba wake Reme Olotun walikua wanahesabu siku kuelekea siku yao ya sherehe ya harusi ambayo walipanga kuifanya tarehe 18 April katika ukumbi wa Hoteli ya Sheraton mjini Lagos Nigeria.
Lakini janga la virusi vya corona lilishika kasi na ikawa dhahiri kwamba Reme, ambaye alifanya kazi na kuishi nchini Canada, asingeweza kurejea nyumbani Nigeria kuoana na Ayokunle.
''Lilikua ni jambo la kusikitisha sana kwangu," aliiambia BBC. "Nilikua tayari nimenunua gauni langu la harusi, viatu na kila kitu kilikua tayari.
Unaweza kutazama namna ndoa inavyofungwa mtandaoni
Lakini kwa upande wake, wazo la kuahirisha harusi halikua jambo ambalo Ayokunle angelikubali . Kwa hiyo alifikiria jinsi anavyoweza kufanya mpango uendelee.
Hatimae, wawili hao waliamua kufanya sherehe yao ya kidini tarehe 18 Arili wakiongozwa na mchungaji kupitia mtandao wa video wa Zoom.
"Ilitufanya tutoke katika hali ya huzuni na kujihisi vibaya na kutufanya tuwe wenye hisia za matumaini chanya na tukaacha hasira, na badala yake tulikua wenye matumaini juu ya hali ," anasema Reme.
"Unaonekana kuwa na kitu cha kuusisimua moyo kila wakati ,"anakumbuka akimwambia mume wake siku ile.
Je ndoa za mtandaoni zinakubalika kisheria?
Nchini Nigeria hakuna kipengele cha sheria cha ndoa za mtandaoni.
Sheria ya nchi hiyo ya ndoa inasema kuwa wanandoa wanaweza kuchagua aina mbili za ndoa. Ndoa ya serikali inayofungwa katika ofisi ya msajiri wa serikali, au ndoa ya kidini inayofungwa katika eneo la kuabudu lenye kibali .
Lakini kwasababu ya masharti ya amri ya kukaa nyumbani kuhusu mikusanyiko, mwanasheria Abisola Ogunbadejo anasema kuwa watu wanaopanga harusi wamekua wakimuomba ahalalishe kisheria sherehe za harusi za mtandaoni.
Aliamua kutengenezavideo ya YouTube akitoa ushauri.
Bi Ogunbadejo anasema kwamba ingawa baadhi wanaweza kuhisi kuwa sherehe za harusi za kidini za mtandao zinatosha , ni muhimu kufuata sheria za ndoa haraka iwezekanavyo ili uwe umejikinga na matatizo ya baadae juu ya mali na urithi yanayojitokeza baadae.
Kwa upande wao , Ayokunle na Reme wanapanga kuendelea na mpango wa kufunga ndoa ya kiserikali wakati Rem atakaporudi Nigeria, kabla ya wawili hao kuhamia Canada.
Lakini kwa sasa wawili hao wanajifunia uamuzi wao wa kufunga ndoa mtandaoni. Na hata kama hawajaoana kisheria, sherehe ya mtandaoni imewafanya waimarishe uhusiano wao kwa namna ya kipekee.
Nitakua ninaisherehekea siku ile kama siku yangu ya harusi ," Ayokunle anasema. " Ninafikiri kwamb Reme ni mke wangu na nimekwishaanza kumuita mke wangu kwa hiyo hilo ndilo muhimu ."
Reme pia anasema awali hakua na uhakika juu ya sherehe ya mtandaoni, lakini ni wazo na utashi wa Ayokunle vilivyomshawishi .
"Alikua mbunifu na nilihisi kumpenda sana kwasababu alijaribu kuhakikisha kwamba kile tulichokipata kinafanana na kile ambacho tungekuwa nacho katika harusi yetu."
Kwahiyo wawili hao walifunga pingu zao za maisha , wakimsikiliza mchungaji akihubiri juu ya mambo muhimu ya ndoa, wakasikia risala kutoka kwa marafiki zao, na hata walidensi pamoja japo walikua mbali.
"Umesalia kuwa wa kipekee sawa na siku ya kwanza tulipokutana…Maisha yangu yasinge kamilika bila wewe," Ayokunle alimwambia Reme.
Walifanya mambo kwa namna yao ya kipekee
Kwa Wanaigeria wengi, harusi huwa ni tukio kubwa matukio ya kifahari na baadhi ya familia hutumia mamilioni ya dola kugarimia sherehe hizo na zawadi za bei.
Lakini kulingana na Reme, kuwa na harusi ya mtandaoni ulikua ni uamuzi sahihi.
"Wakati umefika tuanze kuwa na mtizamo wa mambo kwa ajili yetu wenyewe kile tunachokitaka sisi - watu lazima watakua na kitu cha kusema wakati wote ," anasema.
Harusi ya mtandao ilimaanisha kuwa wapenzi hao waliweza kupuuza shinikizo za kijamii na badala yake wakaangalia kile kilicho muhimu kwao.
"Haingekuwa na maana kuahirisha harusi eti kwasababu ya virusi vya corona ," Akokunle aliongeza
" Ilikua ni zaidi ya tukio-ilikuwa ni kuhusu vitu ambavyo sote tulitaka kufikia, maamuzi ya maisha yetu ambayo tulihitaji kuanza kama mke na mume."













