Virusi vya Corona: Maelfu ya Waisraeli waandamana dhidi ya hali ngumu ya kiuchumi

Maelfu ya Waisraeli wameandamana mjini Tel Aviv kupinga hali ngumu ya kiuchumi inayosababishwa na jinsi serikali inavyokabiliana na janga la virusi vya corona.

Vijana wengi walimiminika katika katika viwanja vya Rabin wakiwa wamevaa barakoa lakini hawakutii agizo la kukaa mbali.

Wanasema malipo ya fidia ya serikali yanakuja polepole sana.

Tukio hilo lililoandaliwa na kundi dogo la wafanyabiashara, wafanyakazi waliojiajiri na makundi ya wasanii.

Watu wengi wanakumbana na changamoto za kiuchumi na wamekasirishwa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya virusi vya corona ambazo zimebadilisha mfumo wao wa maisha.

Wanasema fedha kidogo ambazo serikali ilikuwa imewahaidi hawajalipwa bado.

Wakati wafanyakazi waliajiriwa wanapokea mshahara wao kama kawaida, wale walioajiajiri wanasema inawabidi wasubiri miezi kadhaa kupokea msaada waliohaidiwa na serikali.

"Nina wafanyakazi 40 ambao hawana kipato na hawana fedha," Michal Gaist-Casif, makamu wa rais wa kampuni ya sauti na mwanga aliwaambia wakala wa habari wa Reuters.

"Tunahitaji serikali kutuwekea pesa mpaka hali itakaporudi kuwa kawaida.

Hatujafanya kazi tangu katikati ya mwezi Machi na sasa tupo Julai na mwezi Agosti hali inatarajiwa kuwa tete zaidi".

Waziri mkuu Benjamin Netanyahu alikutana na wanaharakati siku ya Ijumaa kujadili changamoto hiyo.

"Tutatimiza ahadi zetu ikiwemo kuharakisha malipo ambayo tunataka kuwapa," ofisi yake ilimnukuu akiwaambia waandamanaji.

Israel iliweka marufuku ya kutoka nje tangu katikati ya mwezi Machi na kuanza kupunguza amri hizo mwishoni mwa mwezi Mei.

Ongezeko la upungufu wa ajira limeongezeka kwa 21%.

Nchi hiyo imeripotiwa kuwa na visa vipya vipatavyo 1,500 siku ya Ijumaa.

Jumla ya watu 354 wamefariki kutokana na virusi vya corona nchini Israel, kwa mujibu wa takwimu ya chuo kikuu cha Johns Hopkins.