Uchaguzi wa Tanzania 2020: Magufuli aidhinishwa rasmi huku Mwinyi akiahidi kupambana na rushwa

Rais wa Tanzania John Magufuli ameidhinishwa rasmi kuwa mgombea urais wa Chama CCM katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Hatua hiyo imefikiwa Jumamosi Julai 11, katika Mkutano Mkuu wa Chama cha CCM jijini Dodoma.
Rais Magufuli amepata jumla ya kura 1822 ambayo ni asilimia 100 ya kura zote.
Jumla ya wajumbe 1822 wamehudhuria kikao hicho.
CCM pia, imezindua ilani yake ya Chama ambayo kwa mujibu wa Katibu Mkuu wake Dkt Bashiru Ally imejikita katika maeneo kadhaa ikiwemo kuzalisha ajira milioni 8, lakini pia kuimarisha kilimo kwa lengo la kuongeza usalama wa chakula, pamoja na kudumisha huduma za kujamii kama vile Maji na umeme.
Kwa upande wake Dkt Hussein Mwinyi ambae ni mgombea urais upande wa Zanzibar amesema licha ya watu kumuita mpole lakini iwapo atashinda katika uchaguzi mkuu basi atakuja na staili ya Magufuli katika kupambana na rushwa na uzembe.

Humphrey Polepole ambae ni Katibu mwenezi wa CCM amesema mkutano huo pia umehudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka mataifa mengine ikiwemo viongozi wa vyama vya Ukombozi kutoka mataifa ya Afrika.
Dkt Hussein Mwinyi tayari ametangazwa kuwa mgombea urais kupitia CCM Kwa upande wa Zanzibar.

Baadhi ya nchi ambazo zimetuma wawakilishi wake katika mkutano wa leo ni pamoja na Vietnam, msumbuji, DRC, Burundi na Sudan Kusini.
Magufuli apitishwa kuwania awamu ya pili

Kikao cha siku ya Ijumaa kilimpitisha kwa pamoja rais John Pombe Magufuli kuwania awamu ya pili ya urais wa Tanzania.
Magufuli hakuwa na mpinzani katika mchakato huo kwa kuwa hakukuwa na mwanachama mwingine wa CCM aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo.
"Niwaombe wote tukashirikiane kutafute ushindi...wakati mwengine kunakuwa na hali ya kujiamini. Tukijiamini hatutashiriki ipasavyo, tukafanye kazi kwa nguvu ili tukapate ushindi wa kishindo," alisema Magufuli baada ya kupitishwa.
Kama ilivyo kwa jina la Mwinyi, jina la Magufuli linapelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ili lithibitishwe rasmi.
Bado haijabainika upinzani utamchagua nani kupambana na Magufuli katika kinyang anyiro cha uchaguzi wa rais.
Ingawa Magufuli anasifiwa kwa kuanzisha miradi kadhaa, wakosoaji wake ikiwemo makundi ya haki za binadamu wanasemma ametumia nafasi yake kukandamiza upinzani na uhuru wa habari.












