Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gaurav Agrawal : 'Jinsi picha yangu ilivyoharibu simu za Android'
Gaurav Agrawal, mwanasayansi na mpiga picha aishiye San Diego , hakuamini mara alipoanza kuona kwenye taarifa za habari picha aliyoipiga kipindi kilichopita cha majira ya joto.
Aliipiga picha hiyo kwenye ziwa la St Mary , Montana, siku moja jioni mwezi Agosti mwaka 2019.
Aliiweka picha hiyo katika mtandao wa picha wa Flickr na kisha hakuifikiria zaidi.
Hata hivyo, dosari ikawa picha hiyo ikiwekwa kwenye kioo cha simu ya Android simu zinajizima.
Simu zinajizima na kuwaka kwa kujirudia, hali inayosababisha kuhitaji simu kuwekwa tena data zake upya baada ya kupotea.
Juma lililopita, ujumbe wa twitter ulisambaa mitandaoni- na bwana Agrawal aliwasiliana na mwandishi wa teknolojia wa BBC.
''Sikufanya chochote kwa kukusudia,'' alisema ''ninasikitika kuwa watu wameishia kupata matatizo.''
Inaonesha tatizo hilo kuwa kwa aina fulani za simu si aina zote za Android. Haishauriwi kujaribu.
''Ilikuwa jioni moja ya maajabu,'' Bwana Agrawal aliiambia BBC kuwa alikuwa na mkewe alipopiga picha hiyo. Ilikuwa ni safari yao ya tatu katika eneo hilo, wakiwa na nia ya kupiga picha nzuri.
''Ilikuwa hali ya giza giza na mawingu, na tukafikiria kuwa hakutakuwa na muonekano mzuri wa jua kuzama. Ilikuwa karibu tuondoke tuliposhuhudia mambo yakianza kubadilika.''
Anasema walipiga picha ya mandhari hiyo kwa kamera aina ya Nikon, na kisha aliihariri kwa kutumia programu ya kuhariri Lightroom.
Lightroom hutoa aina tatu ya rangi za picha za kuchagua kabla ya kuipakia kwenye kablasha la kuhifadhia picha- na aina aliyochagua kuipamba picha hiyo ndio inayoonekana kuzivuruga baadhi ya simu za Android.
Hakuwa akijua chochote kuhusu matukio ya simu kuzima kwa sababu hakuijaribu hiyo picha kwenye simu yake.
''Sikujua kama mtindo niliochagua wakati wa kuitengeneza picha ungesababisha yote haya,'' alisema. ''Ninatumia Iphone na kioo cha simu yangu kina picha ya mke wangu wakati wote.''
Bwana Agrawal ana wafuasi zaidi ya 10,000 katika mtandao wa picha wa Flickr na kazi zake za picha zimechapishwa katika jarida la Kijiografia.
''Nilitumaini picha yangu itasambaa sana 'kwa sababu iliyo njema, lakini labda kwa wakati mwingine,'' alisema.
''Nitatumia programu nyingine ya kuhariri kuanzia sasa.''
Kwa wale wasiojua kuhusu tukio hili, Ken Munro na Dave Lodge kutoka shirika la usalama la Pen Test wana maelezo ya tatizo hilo:
''Kwa kuimarika kwa ubora wa picha za kidigitali, simu zinahitaji kuangalia picha 'rangi' gani inayofaa ili iweze kukaa vizuri kwenye simu.
''Simu inafahamu namna ya kuonesha kwa uzuri aina ya rangi, kwa mfano ya kijani.
''Kuna namna nyingi za kuelezea muunganiko wa rangi. baadhi ya mpango wa rangi hizo huwa zina matumizi katika kubuni michoro, hivyo wakati mwingine utaona picha haziko katika muundo wa kawaida.
Hivyo inawezekana kutengeneza picha ambazo zina rangi ambazo baadhi ya simu zinaweza kuzimudu.
''Kilichotokea hapa ni namna ambavyo baadhi ya simu zimeshindwa kufanya kazi hiyo.
''Simu huharibika kwasababu haijui namna ya kushughulika ipasavyo na picha zinazowekwa, na watengeneza programu wanakuwa hawajafikiri kama jambo hili linaweza kutokea.''