Matukio ya 'wasiojulikana' yaliyoibua gumzo nchini Tanzania

Kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu

Chanzo cha picha, TUNDU LISSU

Maelezo ya picha, Kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA Freeman Mbowe alivamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo wakati akirejea nyumbani kwake jijini Dodoma.

Kiongozi huyo wa Chadema anaendelea kupata matibabu katika moja ya hospitali zilizopo jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika amevieleza baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania kuwa shambulio hilo lina sura ya kisiasa. Mnyika hata hivyo amesema kuwa taarifa zaidi zitatolewa baadae.

Tukio hilo limeibua hisia mbali mbali kwenye mitandao ya kijamii, wengine wakihusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa

Matukio ya kutekwa, kushambuliwa na kuuawa yamekuwa yakiripotiwa kutekelezwa na watu wasiojulikana, watu ambao mpaka sasa wengi wao hawajabainika kuwa watekelezaji wa vitendo hivyo.

Mauaji ya Kibiti mwaka 2017

Viongozi wa CCM, askari zaidi ya 10 na wananchi karibu 40 katika eneo la Kibiti walishambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana.

Polisi ilisema uchunguzi wao umebaini wauaji walikuwa wanalipa kisasi kwa kile alichodai hisia za kutotendewa haki na baadhi ya watendaji wa serikali na maofisa wa jeshi hilo.

Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro alisema alipozungumza na kituo cha redio nchini Tanzania, Radio one alisema ilichukua muda mrefu kwa jeshi hilo, kukabiliana na wahusika wa mauaji hayo kutokana na wauaji kujipenyeza ndani ya jamii ya wilaya hizo kwa karibu muongo mmoja, hivyo kuwa sehemu ya wakazi maeneo husika.

Katika mahojiano hayo, IGP Sirro alisema uchunguzi wao umebaini kikundi hicho hakina sifa za kigaidi isipokuwa "ni cha kijambazi tu".

Kuuawa kwa Kiongozi wa Chadema wa kata, Daniel John

11 Februari, 2018 Kiongozi wa Chadema Daniel John alitekwa na kisha aliuawa kikatili wakati wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni. Mwili wake ulipatikana mnamo 14 Februari.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kiongozi wa chama hicho katika Kata ya Hananasif, Daniel John alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema hakuwa taarifa hizo lakini anawasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni.

Mbowe alisema John ambaye alikuwa katibu kata alitoweka akiwa na Reginald Mallya ambaye alijikuta yupo ufukweni mwa bahari.

Mbowe alisema walitoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa John na kwamba, walipokwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) walielezwa kuna mwili ulipelekwa na polisi. Alisema mwili huo ulitambuliwa na

mkewe John na ukiwa na michubuko inayoashiria alikabwa, ukiwa na jeraha la panga kichwani na upande mmoja wa kichwa ukiwa umebonyea kuashiria alipigwa na kitu kizito.

Mwanamuziki wa Bongo fleva, Roma Mkatoliki

Chanzo cha picha, Roma Twitter

Kutoweka kwa Roma Mkatoliki na wenzake

Aprili 2017, Mwanamuziki Roma Mkatoliki na wenzie wawili walitekwa na watu wasiojulikana na kuachiwa baada ya siku 3.Msanii wa muziki wa bongo Fleva kutoka Tanzania Ibrahim Musa maarufu Roma

Mkatoliki alitoweka baada ya kudaiwa kukamatwa jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa alichukuliwa katika studio moja katika mji huo pamoja na mtayarishaji wake.Ripoti nyingine zilisema kuwa vifaa vyake vya kurekodi pia vilichukuliwa.

Joff Msumule, rafikiye mzalishaji huyo amesema kuwa maafisa wa polisi walikuwa wanatafuta ushahidi wa kuwashtaki wanamuziki hao.

''Sikuwepo lakini naeleza kwamba kulikuwa na wimbo uliotayarishwa ambao inadaiwa hautoi ujumbe mzuri kuhusu serikali'', alisema Msumule

Habari hiyo ilijiri wiki kadhaa baada ya msanii mwingine wa Bongo Fleva Ney wa Mitego kukamatwa kwa wimbo uliodai kuwa serikali inakandamiza uhuru wa kujieleza, hatua ilioonekana kutusi serikali ya Rais John Pombe Magufuli.

Baadaye aliachiliwa huru, lakini akaambiwa kuuboresha wimbo huo ili kujumuisha masuala mengine yanayoathiri Tanzania.

Habari hizo za kupatikana kwa Roma Mkatoliki zilithibitishwa na mmiliki wa studio za kurekodi muziki, Tongwe ambapo msanii huyo na wenzake wawili walidaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana.

Hata hivyo mmiliki huyo J Mada alisema kuwa hakuna maelezo ya kutosha kuhusiana na wapi walipokuwa na ni akina nani waliokuwa wakiwashikilia.

Shambulio dhidi ya Tundu Lissu

Mnamo 7 Septemba, 2017, Mnadhimu Mkuu wa upinzani bungeni, mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Area D Mkoani Dodoma. Bw Lissu pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika.

FREEMAN MBOWE

Chanzo cha picha, CHADEMA

Rais wa Tanzania John Magufuli kupitia kwenye Twitter alisema amesikitishwa sana na kushambuliwa kwa mbunge huyo.

Ameandika: "Nimepokea kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi Mh. Tundu Lissu, namuombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona haraka. Aidha, vyombo vya dola viwasake wale wote waliohusika na tukio hili la kinyama na kuwafikisha katika mikono ya sheria."

Mbunge huyo kutoka chama cha upinzani cha CHADEMA, akikamatwa akikamatwa mara kwa mara na polisi akishutumiwa kufanya uchochezi.

Familia ya Tundu Lissu iliitaka serikali kuvishirikisha vyombo vya upelelezi vya kimataifa kama vinavyoshirikishwa katika mambo mengine ili kuongeza ufanisi katika upelelezi huo.Tundu Lissu alipigwa risasi zaidi ya thelathini na watu ambao mpaka sasa hawafahamiki.

Jeshi la polisi nchini Tanzania lilisema upelelezi wa tukio hilo unasuasua kutokana na dereva wa Mbunge huyo kutofika polisi kutoa ushahidi. Taarifa kutoka Chadema zilisema kuwa dereva wa mbunge huyo yuko nchini Kenya kwa ajili ya kupata matibabu ya kisaikolojia kutokana msongo wa mawazo alioupata baada ya kisa hicho.

Azory Gwanda

Chanzo cha picha, HRW

Kupotea kwa Azory Gwanda

Tarehe 21 Novemba, 2017 Mwandishi wa habari wa shirika la Mwananchi Communications Limited Azory Gwanda alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajapatikana.

Mtu wa karibu wa mwisho kumuona alikuwa mke wake Ana Pinoni. Bw Gwanda alikwenda shambani na kumkabidhi ufunguo wa nyumba Bi Pinoni na kumueleza kuwa anakwenda kazini.

Bw Gwanda alikuwa ameongozana na watu wanne waliokuwa kwenye gari ambayo Bi Pinoni anaitaja kuwa nia aina ya Toyota Land Cruiser yenye rangi nyeupe.

Toka hapo, Azory Gwanda hajaonekana tena mpaka hii leo.

Baadhi ya wadadisi wamedai kuwa watu waliomchukua mwanahabari huyo ni maafisa usalama, jambo ambalo serikali ya Tanzania imelipinga

Hili ni swali tata ambalo limekosa jibu ukielekea mwaka wa tatu. Imekuwa pia ni kampeni ya mashirika kadhaa ya kutetea haki za wanahabari na haki za binaadamu.

Mwezi Septemba mwaka huu, Azory Gwanda alitajwa kuwa miongoni mwa visa kumi vya dharura vya tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Orodha inayochapishwa kila mwezi na One Free Press Coalition, iliidhinishwa na muungano wa mashirika kadhaa likiwemo TIME kwa lengo la kuwalinda waandishi habari wanaoshambuliwa kutokana na kazi zao.

Bw Gwanda alikuwa akiishi na kuripoti kutoka mji mdogo uitwao Kibiti, ambao upo kilomita kama 130 hivi kusini mwa Dar es Salaam.

Alikuwa ni mmoja wa waaandishi wa kwanza kabisa kuripoti kwa kina juu ya mfululizo wa mauwaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana yaliyowalenga polisi na viongozi wa mji huo.

Abdul Nondo

Chanzo cha picha, Nondo Facebook

Kutoweka kwa Abdul Nondo

Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) ulisema mwenyekiti wake Mahmud Abdul Ormari Nondo hajulikani alipo na kulitaka jeshi la polisi kuhakikisha anapatikana akiwa salama kwa haraka.

Baba mdogo wa kiongozi huyo Mussa Mitumba akiwahutubia wanahabari pia alitoa wito kwa 'mwanawe' kurudishwa akiwa hai aendelee na kutafuta kutimiza ndoto zake.

Kiongozi huyo wa wanafunzi alionekana mara ya mwisho mnamo mwezi Machi tarehe 6 katika ofisi za shirika hilo eneo la Sinza, Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyokuwa imetolewa na shirikisho la vyuo vikuu nchini humo, Tahliso.

Muungano huo unasema baada ya kuondoka ofisi hizo, Bw Nondo alielekea chuoni na kuaga kuwa anaondoka kwenda nyumbani Madale.

Siku kadhaa baadaye Abdul Nondo aliripotiwa kuwa amepatikana akiwa hai eneo la Mafinga mkoani Iringa kusini magharibi mwa Tanzania.

Ilidaiwa kuwa alijikuta katika eneo hilo baada ya kuzinduka kutoka katika lindi la usingizi na kuwauliza wenyeji wa eneo alilo jikuta kuwa yuko wapi? ambao walimfahamisha kuwa yuko Mafinga mkoani Iringa na kisha akapelekwa kituo cha polisi kilichoko karibu.

Awali kabla ya tukio hilo mwanafunzi huyo alielezea kwamba alikuwa akifuatiliwa mara kadhaa watu asiowatambua na wenye nguo za kiraia wakijitambulisha kama watu wa usalama ambao wamekuwa wakimpatia vitisho.

Abdul Nondo alipandishwa mahakamani katika mahakama ya wilaya ya Iringa mjini ambapo alishtakiwa kwa kosa la kudanganya kuwa alitekwa na kudaiwa kutoa taarifa za uongo mtandaoni.

Kiongozi huyo alishinda baada ya hakimu katika maelezo yake kusema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha pasi na shaka tuhuma zilizokuwa zinamkabili Nondo.

Kutekwa kwa Mdude Nyagali

Mwanaharakati wa chama cha upinzani nchini Tanzania Mdude Nyagali alieleza tukio la kutekwa kwake ya kuokolewa mkoani Mbeya

Mdude ambaye aliokolewa na wanakijiji mkoani humo ambao walimpeleka katika hospitali ya eneo hilo . Alikutwa akiwa mchovu na akiwa na majeraha kutokana na kuteswa wakati wa kipindi chote cha utekaji wake.