Virusi vya corona: Kenya yasema 'adui si Tanzania ni Corona'

Chanzo cha picha, Dan Kazungu/Twitter
Balozi wa Kenya cnhini Tanzania Dan Kazungu, ametetea hatua ya Kenya kufunga mpaka na majirani zake akisema kuwa haiwalengi Watanzania.
"Uamuzi ambao Kenya imechukua kuhusu safari za mipakani sio kwasababu ya Tanzania bali adui yetu ni kirusi", amesema Balozi Kazungu.
Katika mazungumzo yake na wanahabari jijini Dar es Salaam Balozi Kazungu alisema Kenya na Tanzania ni nguzo ya uchumi katika kanda ya Afrika Mashariki na kutoa wito kwa raia wa chi hizo mbili kuwa na subira na kudumisha uhusiana mwema kati yao.
Balozi huyo alichukuwa fursa hiyo kuelezea hali ya corona nchini Kenya ambayo iliifanya Kenya kuweka mikakati kudhibiti maambukizi.
Kufikia sasa Kenya ina jumla ya watu 912 walioambukizwa virus via corona.
Tamko lake linakuja siku mbili baada ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kufunga kwa siku 30 mipaka ya chi hiyo na Tanzania na Somalia ili kudhibiti maambukizi ya corona.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika hotuba yake kwa taifa Rais Uhuru Kenyatta alisema hatua hiyo inajumuisha udhibiti wa safari za watu kutoka mataifa hayo kuingia nchini Kenya.
Hatahivyo alisema usafirishaji wa mizigo utandelea kati ya Kenya na mataifa hayo mawili.
Wakati huo pia aliweka masharti sawa na hayo kwa taifa jirani la Somalia.
Siku ya Jumanne Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martin Shigela alipiga marufuku magari yanayobeba shehena ya mizigo kutoka Kenya kuingia nchini Tanzania.
'' Hatuwezi kuwa na bidhaa na watt wanakaa hapa wiki nzima laafu wanaambiwa wana coron'' alisema Bw. Shigela.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa madereva 19 wa malori kutoka Kenya wamepatikana na corona.
Amesema Katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo hawanabudi kuweka utaratibu katika maeneo yao ya mpakani.
Utaratibu huo hata hivyo haujumuishi madereva wa malori wanaosafiri kupitia mipaka ya Tanzania kuenda Rwanda, Burundi Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa zaidi kuhusu virusi vya corona

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira naye mwishoni mwa wiki alitangaza kuzuia magari ya mizigo kutoka Kenya kuvuka katika mpaka wa Holili na badala yake magari hayo yatalazimika kupakua mzigo huo mpakani na kuchukuliwa na magari ya Tanzania.
''Malori yote yanayobeba mizigo na yanayomilikiwa na raia wa Tanzania, na yangependelea kuingia Tanzania ama yanamilikiwa na raia mwingine wa kigeni lakini bidhaa hiyo iliagizwa na Mtanzania , tafuta lori jingine ili kusafirisha mizigo hiyo inakoelekea.''
Malori kutoka mataifa mengine hayataruhusiwa kuingia'', alisema. Bi Mghwira

Alisema kwamba serikali ya Tanzania haitakubali mazingira ya kibiashara kuwekwa katika hali ya ambayo haihusiani na ambayo inaleta utata mkubwa. 'Tusiendelee kuharibiana biashara na kuweka mazingira ya kiabiashara katika hali ambayo inaleta utata'. Alisema Bi.Mghwira
Maelekezo hayo ya Mghwira yalichukuliwa katika mkanda wa video ambao ulisambaa mitandaoni nchini Kenya na Tanzania. Mkuu huyo wa mkoa ameithibitishia BBC kuwa ni kweli ametoa maelekezo hayo.
Kufungwa kwa mipaka baina ya Tanzania na Kenya kumepelekea malalamiko ya wafanyabiashara wa pande mbili wanaodai kuwa imezorotesha shuguli za kibiashara baina ya nchi hizo mbili za Afrika Mashariki. Kinachosubiriwa ni iwapo hatua ya hivi sasa ya Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu kufafanua msimamo wa Kenya juu ya mipaka yake kunaweza kuondoa kukaondoa wingu la mvutano wa kidiplomasia baina ya nchi mbili ulioibuka kutokana na janga la Covid-19.
Taarifa za hivi punde kuhusu virusi vya corona nchini Kenya:
Idadi ya watu walioambukiza virusi vya corona imefikia hadi 963 baada ya watu wengine wapya 51 kupatikana na virusi katika kipindi cha saa 24 zilizopita
Katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne, Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe amesema kuwa idadi ya watu waliopona virusi pia imepanda na kufikia 358 baada ya wagonjwa 22 waliokua hospitalini kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Waziri huyo pia ametangaza kuwa Mombasa ina viwango vya juu vya Covid-19 ikirekodi visa 27, ikifuatiwa na Nairobi 20 na kaunti za Siaya, Bomet na Kiambu zina maambukizi ya mtu mmoja mmoja.
Unaweza pia kutazama:













