Virusi vya Corona: Jinsi ugonjwa usio wa kawaida aina ya kawasaki unavyoathiri watoto

Chanzo cha picha, PA Media
Watoto wengi nchini Uingereza na Marekani wameathirika na ugonjwa usio wa kawaida unaosababisha uvimbe wenye kuhusishwa na virusi vya corona.
Kwa baadhi ya watoto ugonjwa huo unaweza kusababisha matatizo makubwa huku wengine wakihitaji kupata huduma za chumba cha wagonjwa mahututi.
Hadi watoto 100 nchini Uingereza wameathirika na utafiti unaonesha kwamba dalili kama hizo zimeonekana kwa watoto wa sehemu nyengine barani Ulaya.
Hilo huenda linasababishwa na kuchelewa kufanyakazi kwa mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya virusi sawa na ilivyo kwa ugonjwa wa Kawasaki.
Nchini Uingereza watoto wanane wameugua huku mmoja wa miaka 14 akiaga dunia.
Wote walikuwa na dalili zinazofanana walipolazwa katika hospitali ya Evelina London Children's Hospital, pamoja na kiwango cha juu cha joto, vipele, macho kuwa mekundu, mwili kuvimba na maumivu mwili mzima.
Watoto wengi hawakuwa na matatizo makubwa ya kupumua ingawa saba kati ya hao waliwekwa kwenye mashine ya kusaidia kupumua kuimarisha mzunguko wa damu na moyo.
Madaktari wanaeleza ugonjwa huo kama mpya unaofanana na ugonjwa Kawasaki - hali isio ya kawaida ambayo inaathiri watoto chini ya umri wa miaka 5. Dalili zake ni pamoja na vipele, kupata uvimbe kwenye shingo na midomo kukauka hadi kupasuka pasuka.
Lakini ugonjwa huu mpya pia unaathiri watoto wakubwa hadi umri wa miaka 16, wengi wao wakipata dalili mbaya.
Dkt. Liz Whittaker, mhadhiri wa chuo cha udaktari aliyekita katika magonjwa wa kuambukiza kwa watoto na kinga ya mwili kutoka Imperial College London, amesema ukweli wa kwamba ugonjwa huo unatokea wakati janga la virusi vya corona likiendelea, kuna uhusiano wa magonjwa hayo mawili.


"Ugonjwa wa Covid-19 umefika kilele, lakini wiki tatu au nne baadae ugonjwa mpya nao unafika kilele chake na kutufanya tufikirie kwamba ni wa baada ya maambukizi," amesema.
Hii inamaanisha huenda ikawa ni ugonjwa wenye uhusiano na kujega kinga ya mwili baada ya maambukizi.
'Ugonjwa usio wa kawaida'
Prof Russell Viner, rais wa Royal College wa magonjwa watoto na afya yao, amesema watoto wengi waliopata ugonjwa huo wanaendelea vizuri baada ya kupata tiba na wameanza kuruhusiwa kurejea nyumbani.
"Ugonjwa huo sio wa kawaida," amesema.
"Hilo halistahili kufanya wazazi wasiwaruhusu watoto kutoka nje," Profesa Viner ameongeza.
Alisema kuelewa zaidi ugonjwa huo unaosababisha uvimbe kunaweza kusaidia kufahamu kwanini watoto wanaumwa sana wanapopata ugonjwa wa Covid-19, huku wengi wao wakiwa hawajaathirika sana au hawaoneshi dalili".
Idadi ya watoto walioathirika na virusi vya corona inasemekana kuwa asilimia 1-2, ikiwa ni chini ya 500 idadi ya walioalazwa hospitali.
Michael Levin, profesa wa magonjwa ya watoto, ameelezea kwamba watoto wengi hawakuonyesha kuambukizwa virusi vya corona lakini wakaonesha wamepata maambukizi kupitia kinga ya mwili.
"Kwahiyo tuna imani kwamba ugonjwa huo kibaolojia, unahusisha hali isiyo ya kawaida kwa kinga ya mwili dhidi ya virusi," alisema.
Inaonekana watoto wanaathirika hadi wiki sita baada ya kupata maambukizi ya virusi vya corona, jambo ambalo linaweza kuelezea kujitokeza kwa ugonjwa huo mpya wiki kadhaa baada ya maambuki nchini Uingereza kufika kilele.
Hali ilivyo kwengine duniani?
Ugonjwa kama huo umeripotiwa Marekani, Uhispani, Italia, Ufaransa na Uholanzi.
Karibia majimbo 15 nchini Marekani wanafuatilia ugonjwa huo mpya, kulingana na gavana wa New York Andrew Cuomo.
Kati ya wagonjwa 82 waliobainika katika mji wa New York, 53 walikuwa watoto na walionesha kupata maambukizi ya Covid-19.
Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani kinatarajiwa kutoa tahadhari na ufafanuzi zaidi juu ya ugonjwa huu mpya kwa wahudumu wa afya wiki hii.
Wakati huohuo, kulingana na utafiti uliofanywa na madaktari kaskazini mwa Italia, watoto 10 wameambukizwa ugonjwa huu.
Watoto wote 10 waliojumuishwa kwenye utafiti walikuwa wamelazwa eneo la Bergamo - mji ambao umeaathirika zaidi na mlipuko wa virusi vya corona - katikati ya Februari na Aprili na wote wakapona.
Watoto hao ambao umri wao wa wastani ulikuwa ni miaka saba, walionesha kuwa na dalili mbaya kama vile ugonjwa wa moyo na hali inayosababishwa na sumu ya bakteria.
Pia walihitaji matibabu ya tembe za steroidi.
Wataalam wa afya ya watoto nchini Uingereza wanasema huenda ugonjwa ukawa unaathiri hata watu wazima wala sio watoto peke yao.
Kwa sasa wanashirikiana na watafiti kutoka Marekani na maeneo mengine ya Ulaya kufahamu zaidi kuhusu ugongwa huo.













