Joshna Maharaj: Mpishi maarifu atoboa siri kuwa hakuwa na uwezo wa kunusa harufu yoyote kwa miaka mitano

Joshna Maharaj akiwa amesimama jikoni

Chanzo cha picha, MEL YU VANTI

Maelezo ya picha, Joshna Maharaj akiwa amesimama jikoni

Mwezi Januari, mpishi Joshna Maharaj alitoboa siri-hakuwa na uwezo wa kunusa kwa karibu miaka mitano.

Sasa anafanya juhudi ya kurejesha hali hiyo aliyoipoteza.

Kupoteza kwake uwezo wa kunusa kulikuwa kwa taratibu lakini kulikuwa na hali ya tahadhari wakati hali hiyo ilipokuwa ikiendelea

Kwanza, alikuwa anaunguza vitu. Vyakula vitamu alivyokuwa anavipika vilikua vinatoka jikoni vikiwa vyeusi kwa kuungua.

Siku moja alienda kwenye mgahawa wa chakula na marafiki zake na yeye pekee ndiye hakuweza kunusa harufu ya moshi wa nyama iliyokuwa jikoni.

Mpishi huyu mzaliwa wa Toronto, mwanaharakati wa masuala ya chakula na mwandishi wa vitabu amefanya kazi na taasisi kubwa za Umma, kuanzia vyuo vikuu mpaka hospitali kufanya maboresho ya namna ya kupata chakula, kupika na kukitenga kwa ajili ya mlo.

Sasa anepoteza uwezo wa kunusa harufu kabisa

Akawa makini sana katika kuweka muda wa kuivisha kila kitu, kuwa makini ikiwa pua yake itamsaliti.

Mapishi yake yalifanya chakula kuwa ''na ladha zuri sana''.

Joshna Maharaj akiwa kazini jikoni

Chanzo cha picha, JOSHNA MAHARAJ

Maelezo ya picha, Joshna Maharaj akiwa kazini

Kupoteza uwezo wa kunusa, kitaalamu Anosmia kunaweza kuwa na sababu kadhaa, maambukizi ya kawaida, jeraha kwenye ubongo.

Hivi karibuni, watafiti wamegundua kuwa kupoteza uwezo wa kunusa ni dalili ya maambukizi ya virusi vya corona.

Hali ya Bi. Maharaj ilisababishwa na uvimbe kwenye pua.

Kupoteza uwezo wa kunusa na kuonja ladha 'kunaweza kuwa dalili ya kuathirika na virusi vya corona'

Kupoteza uwezo wa kunusa kunakuwaje?

Kwa miaka kadhaa, alipambana mno dhidi ya hali hii.

''Nilijaribu kila kitu-dawa za kichina, nilibadili mlo, kuchomwa sindano

Mwaka 2019, alifanyiwa upasuaji ndani ya pua.Mwezi Agosti alianza kuwa na uwezo wa kunusa.

Kwa mara ya kwanza alinusa harufu ya embe akiwa safarini kwenda Bangalore. Pua yake tena ilinusa harufu ya maua hotelini. Lakini baada ya wiki mbili alipoteza tena uwezo wa kunusa.

Rafiki yake pia alimwambia kuhusu uhusiano kati ya harufu na fikra, akimueleza kuhusu utafiti ulioleza kuwa hali ya kutonusa inahusishwa na ongezeko la msongo wa mawazo, hofu na hisia za kutengwa.

Mwezi Januari, aliandika kwenye ukurasa wa Instagram, akibainisha tatizo linalomkabili na kueleza kuwa ameanza '' mazoezi ya kunusa ili kurekebisha njia kati ya pua yangu na ubongo wangu''.

Alipata msaada wa shirika la Abscent lenye makao yake makuu Uingereza ambalo hutoa elimu kuhusu kupambana na tatizo la kupoteza uwezo wa kunusa na mazoezi ya kunusa ambayo yanaweza kusaidia kurejesha hali kama kawaida.

Maua haya hutumika sana wakati wa mazoezi a kunusa, sambambana mikaratusi, ndimu na karafuu

Chanzo cha picha, GETTY CREATIVE STOCK

Maelezo ya picha, Maua haya hutumika sana wakati wa mazoezi a kunusa, sambambana mikaratusi, ndimu na karafuu.

Hali ya kupoteza uwezo wa kunusa inaaminika kuathiri karibu 5% ya watu wote -ingawa hayo ni makisio tu, anaeleza mwanzilishi wa taasisi Chrissi Kelly.

Watu wanapomtafuta daktari au ushauri kutoka kwenye taasisi kama yake , sababu ni kuwa ''wako katika hali mbaya sana''.

Tafiti zinasema kuwa mafunzo ya kunusa hayawezi kuwa tiba kwa mtu aliyepoteza uwezo wa kunusa lakini inaweza kumsaidia mtu kwa kumpa uwezekano wa kupona kwa kusisimua neva, zinazopeleka taarifa kwenye mfumo wa neva.

Ni kama mazoezi ya pua, anasema Bi Kelly.

Wazo jepesi tu

Chukua manukato ya aina nne tofauti- hasa ya maua na matunda na utumie sekunde kama 20 kwa kila manukato kila siku mara mbili, ukizingatia si tu kupata harufu lakini pia uzoefu wake.

Bi Maharaj alichagua mafuta yenye harufu ya mikaratusi, aina ya rose, ndimu na karafuu.

Kwa wiki kadhaa , hakuweza kuhisi chochote alipofungua chupa za manukato. Kisha mwezi Machi alianza kupata hisia za harufu. Si kuwa harufu za mikaratusi au karafuu, lakini kitu fulani.

Ilikuwa kama kupambana kutamka neno wakati ulimi ni mzito- hakuweza kupata harufu yenyewe. Muda mfupi baadae uwezo wake wa kunusa ulianza kurudi. Ndani ya majuma machache, alipoteza tena uwezo wa kunusa.

Shirila la Abscent nchini Uingereza linaonya kuwa huchukua muda si chini ya miezi minne kufanya mazoezi ili kurejesha uwezo wa kunusa- na uwezo wa harufu unaweza ukarudi kwa kiasi kidogo.

Pamoja na kutokuwa na hali ya ukamilifu Bi Maharaj anasema ana furaha kuanza '' kupata ladha tena ....kufanyia kazi uwezo wa kunusa'' baada ya miaka kadhaa kupika kwa mazoea.