Virusi vya Corona: Idadi ya wagonjwa Tanzania yafikia 88 baada ya wengine 29 kuthibitishwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Wagonjwa wapya 29 wathibitishwa kuwa na virusi vya corona katika mji wa Dar es Salaam nchini Tanzania.
Idadi hiyo inafikisha watu 88 walioambukizwa na Covid 19 kufikia sasa.
Kulingana na taarifa ya wizara ya Afya nchini humo wagonjwa 26 kati yao wapo katika mji wa Dar es Salaam huko wawili wakipatikana mjini Mwanza na mmoja akiwa katika eneo la Kilimanjaro.
Waziri wa Afya Ummi Mwalimu anasema kwamba ufuatilianaji wa watu waliokaribiana na wagonjwa hao unaendelea.

Hatahivyo waziri huyo ametangaza habari njema akisema kwamba hadi kufikia leo Jumatano takriban watu 11 wamepona virusi hivyo lakini akaongezea kwamba watu wanne walifariki.
Ongezeko hilo la wagonjwa linajumlisha wagonjwa wapya sita waliotangazwa na waziri wa Afya wa kisiwa cha Zanzibar.

Serikali hatahivyo imewasisitizia wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo.
Idadi ya wagonjwa wa Corona Zanzibar yaongezeka
Waziri wa Afya kisiwani Zanzibar Hamad Rashid Mohammed alitangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona kisiwani humo.
Kulingaana na waziri huyo mwathiriwa ni mwanamume mwenye umri wa miaka 63 mwenyeji wa kijiji cha kijichi aliyefariki Jumamosi iliopita na kuzikwa saa chache baadaye.
Aidha pia alitangaza wagonjwa wengine sita wapya wakiwemo wanaume watano na mwanamke mmoja wote raia wa Zanzibar.
Wote wamethibitishwa kukosa historia ya kusafiri nje ya nchi.
Dar es Salaam yabuni vituo vya kukusanya sambuli za corona.

Chanzo cha picha, AFP
Wakati huohuo vita dhidi ya maambukizi ya corona vimeimarishwa baada ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kutangaza vituo vya Afya na hospitali ambapo wakaazi watepeleka sampuli zao za ili kupimwa virusi vya corona.
Mkuu huyo anasema kwamba lengo la vituo hiyo ni kuzuia maabukizi ya virusi hivyo hususan wakati huu ambapo kumekuwepo na ongezeko la wagonjwa.
Makonda amesema kwamba hatua hiyo inajiri baada ya wakaazi walio na dalili za virusi kuingia katika vituo vya Afya na kujichanganya na wengine bila kujua.
Baadhi ya vituo vilivyochanguliwa katika wilaya ya Kinondoni ni Hospitali ya Mwananyamala, Kituo cha Afya cha Mgomeni, Kituo cha Afya cha Mikoroshoni, kliniki ya IST Masaki, Hospitali ya TMJ Mikocheni pamoja na Hospitali ya Rabininsia eneo la Wazo.
Katika Wilaya ya Ilala vituo hivyo ni Hospitali kuu ya Amana , Hospitali ya Mnazi mmoja, Hospitali ya Buguruni, Hospitali ya Regency, Hospitali kuu ya Muhimbili, Hospitali ya Aga Khan, na Hospitali ya Hindu Mandal.
Katika Wilaya ya Temeke, wakaazi watapeleka sampuli zao katika hospitali kuu ya Temeke.
Mbagala Hospitali ya Rangi Tatu. Kituo cha Afya cha Yombo, na Hospitali ya TOHS Chan'ombe.
Wilaya ya Ubungo wakaazi wametakiwa kwenda katika hospitali ya Sinza , Kituo cha afya cha Kimara, Hospitali ya Bochi na hospitali maalum ya Mloganzila.
Nao wakaazi wa Wilaya ya Kigamboni watapeleka sampuli zao katika kituo cha Afya cha Vijibweni, Hospitali ya Aga Khan na kituo cha Afya cha Kigamboni














