Pervez Musharraf: Rais wa zamani wa Pakistan ahukumiwa kifo kwa uhaini

Chanzo cha picha, Reuters
Jenerali Pervez Musharraf, kiongozi wa zamani wa kijeshi nchini Pakistan amehukumiwa kifo katika mahakama maalum mjini Islamabad.
Mahakama hiyo ya watu watatu ilimuhukumu kwa kesi ya kiwango cha juu cha uhaini baada ya kuahirishwa tangu 2013.
Jenerali Musharraf alichukuwa mamlaka katika mapinduzi ya kijeshi 1999 na akahudumu kama rais wa taifa hilo kutokea mwaka 2001 hadi 2008.
Kwa sasa anaishi Dubai baada ya kuruhusiwa kuondoka nchini humo kwa matibabu 2016.
Mashtaka hayo yanahusiana na hatua ya jenerali Musharraf ya kuiahirisha katiba 2007, wakati alipoweka utawala wa dharura uliolenga kuongeza muhula wake.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 76 alitoa kanda ya video akiwa katika kitanda chake hospitalini mapema mwezi huu , akielezea kwamba kesi hiyo dhidi yake haina msingi wowote.
Jenerali Musharraf ni mtawala wa kwanza wa kijeshi kufanyiwa kesi nchini Pakistan kwa kusimamaisha katiba. Uamuzi huo ulitolewa Jumanne huku watatu hao wakipiga kura 2-1 kumhukumu.
Je kesi hiyo inahusiana na nini?
Mnamo mwezi Novemba 2007, Jenerali Musharraf alifutilia mbali katiba na kuweka utawala wa dharura - hatua iliozua pingamizi . Alijiuzulu 2008 ili kuzuia tisho la kushitakiwa.

Chanzo cha picha, Handout via Getty
Wakati Nawaz Sharif - mpinzani wake ambaye alimpindua 1999 alichaguliwa kuwa waziri mkuu 2013, alianzisha kesi ya uhaini dhidi ya jenerali Musharraf na mwezi Machi 2014, jenerali huyo wa zamani alishtakiwa kwa uhaini.
Jenerali Musharraf alisema kwamba kesi hiyo ilichochewa kisiasa na kwamba hatua alizochukua 2007 zilikubaliwa na baraza la mawaziri.
Lakini hoja yake ilifutiliwa mbali na mahakama na kushutumiwa kwa kwenda kinyume chas sheria.
Kulingana na katiba ya Pakistan , mtu yeyote anayepatikana na kiwango cha juu cha uhaini anaweza kukabiliwa na hukumu ya kifo.
Jenerali Musharraf amekuwa akiishi Dubai tangu 2016 na amekataa kujiwasilisha mbele ya mahakama hiyo , licha ya maagizo kadhaa.
Kulingana na katiba ya Pakistan , mtu yeyote anayeshtakiwa na uhaini anaweza kukabiliwa na hukumu ya kifo.
Kwa nini ni muhimu?
Kushtakiwa kwa jenerali Musharraf 2014 kwa uhaini ilikuwa hatua muhimu katika taifa ambapo jeshi limekuwa kwa kipindi kirefu katika historia ya uhuru wa taifa hilo.
Wanajeshi waandamizi nchini Pakistan wamelitawala taifa hilo moja kwa moja baada ya mapinduzi kama alivyofanya jenarali Musharraf ama walikuwa na ushawishi mkubwa katika utengenezaji wa sera wakati wa utawala wa raia.

Chanzo cha picha, AFP
Lakini Jenerali Musharraf alikuwa mwanajeshi wa kwanza mkuu akishtakiwa na uhalifu kama huo na inaaminika kwamba jeshi hilo lenye uwezo mkubwa limekuwa likifuatilia kesi hiyo kwa ukaribu mkubwa.
Wachanganuzi wanasema kwamba taasisi hiyo inajua kwamba mwelekeo wowote wa kesi unaweza kuwa mfano.
Je jenerali Musharraf ni nani?
Alichaguliwa kuongoza jeshi la Pakistan 1988.
Kuhusika kwa jeshi katika vita vya Kargil mwezi Mei 1999 kulisababisha mgogoro mkubwa kati yake na waziri mkuu Nawaz Sharrif , na jenerali huyo wa jeshi alichukua mamlaka kupitia mapinduzi 1999.
Akihudumu kama rais hadi 2008, Jenerali Musharraf alinusurika majaribio kadhaa ya mauaji wakati wa utawala wake.
Ni maarufu duniani kwa jukumu lake katika vita vya Marekani dhidi ya ugaidi, ambavyo aliviunga mkono baada ya shambulio la kigaidi la 9/11 licha ya kupata upinzani nyumbani.
Jenerali Musharraf aliondoka taifa hilo baada ya kuachilia uongozi wa tafa hilo 2008 , lakini akarudi 2013 kuwania urais , wakati ambapo alizuiliwa na mahakama kushiriki huku akikabiliwa na kesi kadhaa.
Alijiwasilisha mara mbili pekee katika kesi ya uhaini na mapema alikuwa akiishi katika kambi moja ya kiafya ama katika shamba lake mjini Islamabad.
Alielekea Karachi mnamo mwezi Aprili 2014 ambapo aliishi hadi alipoondoka miaka miwili baadaye.













