Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je ni kwanini familia za watu hawa zinawakataa baada ya kutofanikiwa kwenda Ulaya?
Wengi miongoni mwa wahamiaji wa Afrika magharibi wanaoshindwa kufika Ulaya hatimae hurejea katika nchi zao za asili, lakini wakati mwingine kurejea kwao nyumbani kunaweza kuwa na machungu.
Nchini Sierra Leone, wanaorejea mara nyingi hukataliwa na ndugu na marafiki zao. Huonekana kama watu walioshindwa na maisha, na wengi huziibia familia zao pesa kulipia safari zao.
Baadhi ya wasomaji wanaweza kuhisi hadithi hii ni ya kusikitisha
Fatmata anaangua kilio akikumbuka miezi sita aliyoishi katika utumwa kama "mke" wa Mtuareg anayehamahama ambaye alimteka katika jangwa la Sahara.
"Walimuita Ahmed. Alikuwa na umbo kubwa na muovu sana," anasema. "Alisema , Wewe ni mtumwa, wewe ni mweusi. Nyie watu mnatoka kuzimu.' Aliniambia wakati mtu ana mtumwa, unaweza kufanya chochote unachokitaka.
Si yeye peke yake. Wakati mwingine alikuwa anawaambia rafiki zake, '' Mnaweza kuonja chochote ndani ya nyumba yangu. '' Walinitesa kila siku ."
Huo ulikuwa ni mwanzo tu wa maisha ya kutisha ya Fatmata, mwenye umri wa miaka 28, kutoka Freetown, Sierra Leone, aliyoyapitia alipokuwa akijaribu kuvuka bahari ya Mediterranean kwenda Ulaya.
Hatimae alifanikiwa kutoroka kutoka kwa Ahmed, lakini akakamatwa tena na wafanya biashara haramu ya kusafirisha watuambao walimshikilia katika gereza lao binafsi nchini Algeria.
Baada ya kutenganishwa na wahamiaji wenzake, Fatmata, alipatwa na msongo mkubwa wa mawazo, akaamua kuachana na ndoto zake za kutafuta maisha mapya katika bara la Ulaya, na kurudi nyumbani.
Alituma maombi katika shirika la kimataifa la Uhamiaji (IOM), ambalo hulipia gharama ya usafiri kwa wahamiaji wanaotaka kurejea nyumbani.
Mwezi Disemba mwaka jana , aliwasili mjini Freetown, kwa basi kutoka Mali - baada ya kuishi mbali na nyumbani kwa miaka takriban miwili.
Lakini hakukuwa na makaribisho ya furaha, hakukaribishwa wala kukumbatiwa. Karibu mwaka mmoja baadae, Fatmata hajamuona hata mama yake- wala binti yake, ambaye sasa ana umri wa miaka minane aliyemuacha.
"Nilifurahi sana kuudi nyumbani," anasema. "Lakini sasa natamani nisingerudi."
Wakati aliporudi nyumbani, alimuita kaka yake. Lakini majibu yake yalimuogofya. "Aliniambia, ' Haungepaswa hata kurudi nyumbani. Ungetakiwa ufie tu huko ulikokwenda, kwasababu haujaleta chochote nyumbani .'"
Baada ya hayo, anasema , "Sikuwa na moyo wa kwenda na kumona mama yangu."
Lakini familia yake haikumkataa kwasababu alishindwa kufika Ulaya. Alikataliwa kwasababu ya pesa alizoiba kwa ajili ya kulipia garama ya safari yake ya kwenda Ulaya.
Aliiba pesa za Siera leone-leones milioni 25 sawa na dola za kimarekani takriban $2,600 , pesa ambazo wakati huo zilikuwa na thamani kubwa kutoka kwa shangazi yake .
Zilikuwa ni pesa ambazo shangazi yake alikuwa amempatia amnunulie nguo, ambazo zingeuzwa katika duka lake la biashara. Shangazi yake alimuamini mara kwa mara kumfanyia shughuli hiyo.
"Nilikuwa ninafikiria tu namna ya kupata pesa na kuondoka," Fatmata anasema, ingawa anaongeza kuwa yeye si mbinafsi . "Kama ningefanikiwa kwenda Ulaya, nilikuwa nimepanga kulipa pesa hizo mara tatu, ningewatunza vema mama na shangazi yangu."
Lakini biashara ya shangazi yake Fatmata haikufanikiwa tena kwani alikosa pesa. Na -baya zaidi wizi huo umeleta uhasama kati ya mama yake Fatmata na shangazi yake , ambaye anamshutumu mama yake Fatmata, kupanga njama ya wizi na binti yake.
"Nina maumivu makubwa, maumivu makali!"alisema mama yake, alipotembelewa na BBC . "Siku nitakapomuona Fatma, ataishia kituo cha polisi - na nitakufa siku hiyo."
Hadithi hii inafanana na hadithi nyingine za raia wengi miongoni mwa Wasierra Leone 3,000 na zaidi ambao wamerejea nyumbani katika kipindi cha miaka miwili baad ya kushindwa kufika Ulaya.
Wakati mwingine ndugu huchanga pesa kumpeleka mtu fulani Ulaya , lakini kwa sasa si wengi wanaotaka kufanya hivyo kwasababu taarifa za kufungwa na vifo katika njia inayoelekea Ulaya zimeongezeka sana.
Sasa wengi wanaotaka kuwa wahamiaji hupanga mipango yao kwa siri, na kuchukua pesa wanazoweza kupata, wakati mwingine hata huuza vibali vya ardhi za familia.
Katika makao makuu ya Kikundi kinachotetea maslahi ya wahamiaji haramu Advocacy Network Against Illegal Migration, kikundi ambacho hujitolea huwasaidia wahamiaji wanaoamua kurejea nyumbani kujenga upya maisha yao, wahamiaji wote waliorejea walikuwa wameiba pesa kutoka kwa familia zao.
Jamilatu, mwenye umri wa miaka 21, ambaye alitoroka pamoja na Fatmata kutoka kwenye gereza la wafanyabiashara haramu ya kusafirisha watu nchini Algeria, alichukua mfuko wa plastiki wa pesa zenye thamani ya dola $3,500 kutoka katika chumba cha mama yake alipokuwa nje ya nyumba. Pesa haikuwa hata ni ya mama yake.
Alikuwa amekopeshwa na majirani zake kama sehemu ya mfumo wa kukopeshana.
Baada ya Jamilatu kuondoka, majirani wenye hasira waliomkopesha waliizingira nyumba ya mama yake huku wakitishia kumuua iwapo hatarejesha pesa hizo. Alilazimika kuutoroka mji wa Freeton na kwenda kujificha katika mji wa Bo, uliopo umbali wa saa tatu , kusini mwa nchi, na watoto wake wengine watatu pamoja na baba yao.
"Mama yangu hataki kuongea na mimi, kwasababu ya pesa," anasema Jamilatu. "Kwa hiyo tangu niliporejea sijamuona. Na ninataka kumuona mama yangu-ni zaidi ya miaka miwili sasa sijamuona."
Mama yake Maryatu alitembelewa na BBC katika makazi yake mapya katika mji wa Bo, na baada ya mazungumzo ya muda mrefu alisema angependa kukutana tena na Jamilatu, licha ya masaibu aliyoyasababisha.
Lakini walipokutana siku chache baadae, hakuna aliyemuongelesha mwenzake . Walikumbatiana kimya kimya. Halafu Jamilatu akapiga magoti mbele yake, akiomba msamaha. Hakuna aliyemuangalia mwenzake machoni.
Baadae , Jamilatu alirudi mara moja mjini Freetown.
"Mimi ni mwanamke mwenye furaha zaidi duniani leo kwasababu nimemuona mama yangu ," anasema. Lakini haonekani mwenye furaha. Mama yake amemwambia kuwa hawawezi kuishi katika nyumba moja tena hadi pale atakapotafuta pesa aliyoiiba irejeshwe kwa waliomkopesha.
Ni vigumu pesa hizo kupatikana. Jamilatu, sawa na Fatmata, hana ajira. Wote wanategemea msaada kutoka kwa Shirika linalowasaidia wahamiaji haramu.
Shirika hilo lilianzishwa na Sheku Bangura, ambaye binafsi ni muhajiaji aliyerejea, ambaye hufanya juhudi za kuishawishi serikali ya Sierra leone kuwasaidia wahamiaji wanaorejea nyumbani - hadi sasa kuna usaidizi rasmi mdogo sana na hujaribu binafsi kutoa usaidizi anaoweza mwenyewe .
Hutafuta makazi ya wale ambao hawana mahala pa kusini, kuomba usaidizi wa polisi pale wanaorejea wanapopata matatizo , na kuandaa usaidizi wa ushauri wa kimsingi wa kisaikolojia.
"Nimekuwa na wahamiaji wengi wenye matatizo ya kiakili ," anasema. "Hawa vijana, wako mitaani, hawana sehemu ya kulala. Hali sio rahisi kwao kabisa."
Mmoja wa watetezi wa wahamiaji ni Alimamy mwenye umri wa miaka 31- ambaye aliweza kuondoka Sahara miaka mitatu iliyopita, baada ya kuiba na kuuza mashine ya gharama kubwa ya usindikaji wa maji ya mjomba wake.
Mmoja wa watu waliosafiri nae alikufa kutokana na njaa jangwani. Wapili alizama alipokuwa akijaribu kuvuka bahari ya Mediterranean. Alimamy aliishia kwenye mahabusu ya kambi ya wahamiaji nchini Libya.
Aliokolewa tu mwezi Novemba mwaka 2017 wakati shirika la uhamiaji IOM lilipoanza kuandaa safari za ndege kutoka Tripoli kuelekea Afrika Magharibi kwa wale waliotaka kurejea nyumbani.
Kutokana na mateso na uchovu aliokuwanao, alikubali apewe tiketi ya ndege ya kurejea nyumbani, lakini alihofia mapokezi ambayo angeyapata atakapowasili.
" Nilikuwa ninafikiria kuwa sipaswi kurudi Sierra Leone, kwasababu nilifahamu fika kuwa mjomba wangu alikuwa ni mtu mwenye hasira sana," alisema.
Tangu arejee, Alimamy amekuwa akiishi na marafiki zake. Kaka yake mkubwa Sheik Umar, ambaye ni mchezaji soka wa zamani wa kulipwa, anasema: "Tunasiki yuko mjini Freetown, anahangaika. Na bado hajapata ujasili wa kuonana na mtu yeyote katika familia yetu "
Sheik Umar anasema kuwa alikuwa mgtu wa karibu sana na kaka yake, lakini ikiwa atamuona sasa, atahakikisha "anakamatwa, ashtakiwe na kupatikana na hatia".
"Kama atafia gerezani, haitanisikitisha. Ninauhakika hakuna mtu yeyote wa familia ambaye atajutia kwa hilo, kwasababu ya aibu aliyetuletea sote ."
Anasema biashara ya kusindika maji ambayo Alimamy alikuwa amepewa kuiendesha na mjomba wake ingezalisha pesa za kutosha kuisaidia familia nzima.
"Lakini alitumia vibaya fursa aliyopewa na sisi sote kwa pamoja tuko katika shinda … Kokote ninakoenda sasa watu wananicheka. Mama yetu anaumwa, amehamia . Biashara ile ulikua ni mwanzo wa matumaini yetu. Lakini Alimamy amemaliza matumaini yote."
Alimamy mwenyewe anahasira na hajui afanye nini . " Nimerudi nyumbani, hakuna cha maana nilichofanya, sina chochote," anasema ." Mahali ninapoishi , nikama kuzimu . Jinsi watu wanavyoniangalia, Sijihisi kuwa mwenye furaha . Wananiangali kana kwamba mimi sio binadamu."
Shirika la IOM huwasaidia wahamiaji wanaorejea nyumbani Afrika kwa utashi wao kwa "kuwapatia pesa za marupurupu kidogo ya kuwawezesha kurejea tena katika maisha ya kawaida " yenye thamani ya euro 1,500 (£1,270). Pesa hizo hutoka katika mfuko wa euro milioni 347 unaodhaminiwa zaidi na Muungano wa Ulaya. Lakini pesa hizo hazitolewi kama pesa taslimu.
Kama zingekuwa zinatolewa hivyo watu wengi wangezitumia kuwalipa ndugu zao. Kwa hiyo IOM hulipia bidhaa na huduma ambazo muombaji anaweza kuthibitisha wanazihitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara fulani.
Alimamy alipata pesa hizo za marupurupu kwa ajili ya kununua pikipiki ambayo angeikodisha kwa waendesha pikipiki wengine kama teksi. Lakini baada ya miezi minne, mmoja wa madereva aliiba na kuondoka nayo. Alimamy pia akawa muathiriwa wa wizi.
Fatmata na Jamilatu wao hawakupokea marupurupu hayo kutoka kwa IOM, kwasababu walirudi kutoka Mali katika wakati ambapo Wasierra Leone wengine walikuwa wakikiuka utaratibu kwa kupanda basi hadi Mali, wakidanganya kuwa wangepitia jangwa la Sahara na kudai marupurupu hayo. Kwa hiyo kila mtu aliyerudi kutoka Mali hakuyapata akiwemo Fatmata na Jamilatu.
Kwasasa, wote watatu wanashiriki katika "tukio la kuboresha uelewa '' lililoandaliwa na shirika la kuwatetea wahamiaji (Advocacy Network). Wanatembea kwenye mitaa na mabango pamoja na vipazasauti wakiwaonya vijana juu ya hatari za uhamiaji haramu na kuwasihi wabakie katika " Sierra Leone tamu".
Lakini kwao, nyumbani sio patamu tena. Wote watatu wamejawa na hisia za kutokuwa na thamani.
Fatmata anasema: "Sina lolote la kusaidia, Sina lolote la kuonyesha. Siwezi hata kwenda kumuona binti yangu, Ninaona picha tu, kwasababu sina kitu cha kumpatia nitakapofika pale, kwa hiyo siwezi''
Alimamy anasema "unyanyapaa" anaoupata unamlazimisha kufanya kile anachokisema kwenye mitaa. Anataka kujaribu tena kufika Ulaya.
"Kwangu mimi Kuishi hapa ni kama kuishi kuzimu ," anasema. Alipokumbushwa masaibu aliyopitia alipojaribu mara ya kwanza kwenda Ulaya mkiwemo mateso, na utumwa alisema: ''Nimepitia yote hayo, na nina uhakika ninaweza kuyavumilia''
Unaweza pia kusoma:
Azis Hanna, Kutoka Iraq, alikuwa amekaribia kuwalipa wafanyabiashara haramu ya binadamu kuiwezesha familia yake kuingia kupitia mifumo ya Uingereza kwa njia ya boti isiyo salama . Lakini wakati marafiki zake waliponusurika na kifo ilibidi afikirie tena.